• JOFLO HEALTH REFORMATION CENTER

    HII NI KWA WALE WOTE WANOSUMBULIWA NA MAGONJWA YA MOYO FIGO KISUKULI NK WASILIANA NASI KWA SIMU NO 0787426142,0655426142 AU TEMBELEA BLOG YETU www.jhrcenter.blogspot.com USIENDELEE KUTESEKA NA MAGONJWA

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimesema kuwa hutumia maiti 25 kwa kuwafundishia wanafunzi kila mwaka

  Viungo vya Binadamu ambayo hutumika kufundishia madaktari.


Dar es Salaam. Wakati sakata la kuokotwa kwa viungo vya binadamu likiendelea kutikisa nchi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimesema kuwa hutumia maiti 25 kwa kuwafundishia wanafunzi kila mwaka.

Pia chuo hicho hakijawahi kuagiza maiti kutoka nje ya nchi na kwamba ni mtu mmoja tu aliyewahi kutaka maiti ya mtoto wake itumike kufundishia.

Kauli hiyo ya MUHAS imekuja siku chache baada ya Serikali kuamua kuifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), baada ya kubaini kasoro kadhaa katika utendaji wake.

Juzi, Serikali ilifanya ukaguzi wa kushtukiza IMTU, baada ya hospitali hiyo kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Hata hivyo, wakati Tume ya Watu 15 iliyoundwa na Serikali kuchunguza suala hilo ikiendelea na kazi, Mkuu wa Kitengo cha Anatomy MUHAS, Profesa David Ngassapa amebainisha kuwa chuo hicho hutumia maiti 25 kwa mwaka.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Ngassapa alisema kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza hutumia maiti 20, huku madaktari wanaorudi chuoni hapo kwa ajili ya mazoezi wakitumia maiti tano.

“Sheria ya mwaka 1963 inatutaka baada ya matumizi tuondoe mwili kwa heshima zote na miongoni mwa vitu ambavyo wanafunzi wanasisitizwa ni kuhakikisha wanaiheshimu miili hadi hatua za mwisho,” alisema Ngassapa.

Alieleza kuwa pamoja na sheria kutoa ruhusa ya kutumia maiti katika mafunzo, bado imeweka vipengele vinavyowataka madaktari kuiheshimu miili ya watu, hadi hatua ya mwisho.

Ngassapa aliongeza: “Sheria inaruhusu kuhifadhi mabaki ya miili kwa njia mbili; kuizika na kuichoma moto, pia hospitali inaweza kuhifadhi mabaki hayo hata kwa miaka mitano.”

Hajawahi kuagiza miili kutoka nje
Akizungumzia utaratibu wa nchi kubadilishana maiti kwa ajili ya mafunzo, Profesa huyo alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 30 aliyokuwa katika kitengo hicho, hawajawahi kuagiza maiti kutoka nje ya nchi.

Alisema maiti zilizopo nchini zinatosha kufundishia wanafunzi wote wa udaktari kwa kuwa siyo Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH), pekee inayotegemewa kutoa miili hiyo.Alisema kuwa siku za nyuma, Serikali ilikuwa ikiagiza mifupa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo, lakini sasa kila kitu kinafanyika hapa nchini.

Ngassapa alisema kuwa miili iliyoharibika kwa ajali au magonjwa haifai kutumiwa kwa kuwa mwanafunzi anatakiwa kujifunza kwenye mwili uliokamilika.

Amkumbuka mtu aliyetoa maiti ya binti yake
Alisema kuwa historia ya Tanzania inaonyesha kuwa ni mtu mmoja pekee ndiye aliwahi kujitolea maiti ya binti yake ili itumike kufundishia.

“Alijitolea kwa kuwa binti yake huyo alianza kuugua akiwa na umri wa miaka miwili hadi alipofikisha miaka 12, muda mwingi akiwa amelazwa hospitalini hapa,” alisema.
“Alipofariki dunia mzazi alisema mtoto huyo ni wa hospitali na anamtoa kwa ajili ya matumizi ya hapa. Ibada ya mazishi ilifanyika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema Ngassapa.

Alifafanua kuwa hata baada ya kukabidhiwa maiti hiyo, waliendelea kumhifadhi kwa miaka minne, hadi walipojiridhisha kuwa wazazi hawatabadilisha mawazo.

Sheria inayotumika
Mkuu huyo wa kitengo kinachoshughulikia mwili na viungo vyake, alisema kuwa sheria ya Serikali ya mwaka 1963, ndiyo inayoruhusu chuo chochote cha afya kuchukua mwili kama umekaa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa siku 14 bila ndugu kujitokeza.

Ngassapa alifafanua kuwa licha ya sheria kuwataka kuchukua mwili uliokaa katika kipindi hicho, chuo huuhifadhi mwili huo kwa siku 30, ili kujiridhisha pasipo shaka kwamba hakuna ndugu anayejitokeza kuuchukua.

Alibainisha kuwa baada ya hapo, huuweka dawa ili usiharibike, kisha huuacha kwa wiki mbili au tatu zaidi wakisubiri kama ndugu wanaweza kujitokeza.

“Inapothibitika kuwa hakuna anayejitokeza, chuo huuchukua na kuutumia kwenye mafunzo,” alisema.


Alifafanua kuwa sheria pia inakitaka Kitengo cha Anatomy kuandika barua kwa mkuu wa chuo na Mahakama Kuu, kutaarifu kuwa wamechukua mwili kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia juzi aliliambia gazeti hili kuwa miili ni mali ya Serikali na kwamba chochote kinachofanyika kwa binadamu lazima kifuate sheria zilizowekwa na Serikali.

Pia alisema kwamba sheria inaruhusu nchi kubadilishana maiti, lakini hana uhakika kama jambo hilo limewahi kufanyika nchini, ingawa ana uhakika kuwa haiwezekani hospitali zikakosa maiti za kufundishia.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira akiwakilisha CCM, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, jana walitoana jasho katika mdahalo wa Katiba mya

 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Stephen Wassira akizungumza kwenye mdahalo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa Singida Mashariki(Chadema) Tundu Lissu na katikati ni Mwenyekiti wa CUF,  Profesa Ibrahim Lipumba.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira akiwakilisha CCM, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, jana walitoana jasho katika mdahalo wa Katiba ulioandaliwa na East African Business and Media Institute.
Mdahalo huo uliohudhuriwa na watazamaji wapatao 500, ulikuwa na mada inayosema: ‘Nani anakwamisha Upatikanaji wa Katiba Mpya.’ Kila upande ulitumia fursa hiyo kutupa shutuma kwa mwingine huku jazba na kelele vikitawala miongoni mwa waliohudhuria.
Hata hivyo, suala la muundano wa serikali ndiyo uliochukua nafasi kubwa katika mdahalo huo huku Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukiishutumu Serikali ya CCM kuwa ndiyo kikwazo cha upatikanaji wa Katiba Mpya nayo ikitupa mpira huo kwa Ukawa kwa kitendo chake cha kutoka katika Bunge Maalumu la Katiba.
Profesa Lipumba alisema wahafidhina wa CCM ndiyo waliomshauri Rais Jakaya Kikwete abadilike kimsimamo kuhusu upatikanaji wa Katiba Mpya.
“Rais Kikwete alikuwa na nia njema kabisa kuhusu Katiba Mpya lakini wahafidhina wa CCM wanaopenda madaraka walipoona muundo wa serikali tatu wakambana naye akabadilisha msimamo, tunamwomba abadilike, nchi hii ni yetu sote ili tupate katiba ya wananchi,” alisema.
Lissu aliongeza kwa kusema kuwa anayekwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya ni CCM ambao wanaweka maoni yao badala ya kujadili rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo maoni ya wananchi.
“Hatuwezi kurudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba kwenda kujadili rasimu ya CCM kwa sababu wanaonyesha hawana nia ya Katiba Mpya, bali wanataka kuwadanganya Watanzania, watawadanganya wananchi kwa kuleta Katiba ileile ila ikiwa na rangi tofauti,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema Ukawa hawawezi kushiriki katika udanganyifu wa aina hiyo na kwamba wameamua kuwaachia CCM ili wananchi waweze kuwahukumu kwa uovu watakaoufanya.
Alisema kati ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika Kundi la 201, wajumbe 166 ni wana CCM walioteuliwa ili kuongeza idadi ya watu.
“Humo kuna viongozi wa dini mashehe na maaskofu na waganga wa kienyeji ambao ni wana CCM ili wapitishe Katiba yenye masilahi yao binafsi,” alisema.
Hata hivyo, Wassira alisema hoja za Ukawa hazina mashiko na kumtaka Lissu kuwaomba radhi masheikh na maaskofu kwa kuwa hawakuteuliwa na Rais kutokana na kuwa wanachama wa CCM, bali ni mapendekezo ya taasisi wanazozitumikia.
“Namwomba Tundu Lissu akawaombe radhi masheikh na maaskofu kwa sababu kundi hili liliteuliwa kutokana na mapendekezo ya wahusika wenyewe pasipo shinikizo la Rais. Hapakuwa na uwezekano wa Rais kuwatambua wana CCM ili awateue wanaofaa. Kama ana ugomvi na Kingunge Ngombale Mwilu aseme.”

Alisema wanaokwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya ni Ukawa... “Katiba Mpya haiwezi kupatikana mitaani, bali kwa majadiliano na maridhiano kwenye Bunge Maalumu la Katiba, nawashauri warudi bungeni ili tuweze kupata Katiba Mpya.”
Alisema Bunge Maalumu la Katiba lina mamlaka ya kubadilisha vifungu kwenye rasimu ya Katiba na kwamba halipo kwa ajili ya kupitisha tu vifungu vilivyowekwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kauli hiyo ya Wassira ilifanya kila aliposimama kuzomewa na wananchi waliohudhuria mdahalo huo huku wafuasi wa Chadema na CCM wakitishiana kupigana hali iliyosababisha mabaunsa kuwatoa nje ya ukumbi baadhi yao walioshindwa kustahimiliana.
Wajumbe wawili waliokuwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole na Awadh Said, katika michango yao walitaka kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi ili kupata katiba itakayowafaa kwa muda uliokusudiwa.
Polepole alisema tatizo la wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ni masilahi binafsi na ya makundi katika utafutaji wa Katiba Mpya.
 
“Wananchi wasimamie masilahi ya taifa na wasiwaachie mchakato mzima wanasiasa ambao wana masilahi binafsi pamoja na yale ya kikundi yenye shinikizo la masilahi binafsi,” alisema Polepole.
Awadh alisema maoni yalikusanywa kutoka katika mabaraza ya katiba 170 na 600 ya taasisi na vyama vya siasa kutoka katika wilaya zote 43 za Zanzibar.
“Kwa nini juhudi zote hii zibadilishwe na wajumbe 629 peke yao kwenye Bunge Maalumu la Katiba?  Tufuate maoni ya wananchi kupitia tume ndipo tutakuwa tunawatendea haki Watanzania,” alisema.
Alielezea kusikitishwa na kitendo cha Serikali kufunga tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba akisema kimewanyima wananchi haki ya kupata taarifa mbalimbali za tume hiyo.

Abiria wote wa ndege ya Air Algerie wameangamia jangwani

Abiria wote wa ndege ya Air Algerie waliangamia jangwani

Abiria wote na wahudumu wa ndege ya Air Algerie AH5017 wameangamia jangwani.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametangaza kuwa majeshi ya ufaransa yamefaulu kupata mabaki ya ndege lakini hawakuweza kuokoa nafsi hata moja.

Aidha rais Francois Hollande ametangaza kuwa majeshi hao wamepata mtambo wa kunukuu sauti ''Blackbox'' huko Mali ilikoanguka ndege hiyo iliyokuwa ikielekea mji mkuu wa Algeria Algiers.

Abiria wote wa ndege ya Air Algerie waliangamia jangwani

Ndege hiyo ilikuwa imetoka mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadougou ikiwa na Abiria 110 na wahudumu 6 .
Abiria 51 waliokuwa ndani ya ndege hii walikuwa ni raiya wa Ufaransa.

Wengine walikuwa 27kutoka Burkina Faso, 8 kutoka Lebanon , 6 kutoka Algeria , 2 kutoka Luxembourg, 5 kutoka Canada, Wajerumani 4 .

Jamaa ya wahasiriwa wanakutana huko Ougadougu Burkina Faso

Abiria wengine walikuwa mmoja kutoka mataifa ya Cameroon , Ubeljiji ,Misri Ukraine Uswisi Mnigeria na mmoja kutoka Mali.

Waziri wa Usalama wa ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve alisema ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Algiers kutoka mji mkuu wa Burkina Faso , Ougadougou,ilianguka kutokana na hali mbaya ya anga
 
Habari na BBCswahili.com

Dk Titus Kamani: Nitakufa na wetendaji watakaochakachua Fedha za mirdi ya maji

 Dk Titus Kamani akikagua mradi wa maji jimbo la Busega

Na Antony Sollo   Busega
WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, amewaonya watendaji watakaotafuna fedha za miradi mbalimbali inayotekelezwa jimbo la Busega.


 Dk. Kamani, alitoa kauli hiyo jana akikagua mradi wa maji katika kijiji cha Nyangili Kata ya Igalukilo jimbo la Busega Mkoani Simiyu ambapo pamoja na mambo mengine Dk Kamani alikagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Kata hiyo.


Alisema,mradi huo umetumia fedha nyingi ambazo wala si bajeti ya Serikali bali ni juhudi zake binafsi kama mwakilishi wa wananchi hao lakini akiwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Marafiki ,wahisani pamoja na Benki ya Dunia, “nawaomba ndugu zangu  muulinde mradi huu  na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa bila kubaguliwa”

Mradi wa maji katika kijiji cha Nyangili Kata ya Igalukilo jimbo la Busega Mkoani Simiyu umetumia kiasi cha shilingi milioni 300,000,000.ikiwa ni fedha kutoka Benki ya Dunia.


Najua mmepata shida hii ya maji kwa muda mrefu hatimaye serikali yenu imesikia kilio chenu, hivyo kuuharibu au kuuchakachua mradi huu ni kutaka muendelee na shida iliyokuwa inawasumbua na ninaapa,nitakufa na watu watakaofuja fedha za miradi inayotekelezwa katika jimbo letu.


Dk Kamani ameitaja miradi inayotekelezwa katika kata ya Igalukilo kuwa  ni pamoja na mradi wa Umeme unapita katika kijiji cha Nyangili,Lunala na Mwamagigisi,na mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa Kituo cha Afya Igalukilo.


Upande wa ujenzi wa barabara,Dk Kamani alisema kuwa miradi ya barabara imetengewa shilingi milioni 300,000,000. Ambapo alisema barabara ya Mwamjulila na badugu itatengenezwa na itapitika kwa urahisi kuliko ilivyokuwa hapo awali kabla ya Uongozi wa Dk Kamani.


Baada ya kukagua miradi mbalimbali katika kata hiyo Dk Kamani alihutubia Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Malangale ambapo aliwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kumpigia kura na kumpa ushindi na kuwaahidi kuwa ataendelea kutimiza ahadi pamoja na kutekeleza ilani ya chama kwa kuwaletea maendeleo ya pamoja,badala ya kushughulika na mtu mmoja mmoja.


Dk Kamani aliguswa na Risala ya kikundi cha wananchi kinachojulikana kama fogong’ho ambacho kinafanya shughuli za kuchangiana na kukopeshana fedha kwa ajili ya kujinunulia mahitaji madogomadogo ambapo alitoa mchango wa shilingi laki tano500,000. kuunga mkono juhudi za wanakikundi hao.


Akihitimisha hotuba yake,Dk Kamani alitoa mpira kwa wachezaji wa timu ya Zege Malangale FC na kuwaasa kuwa,michezo ni Afya hivyo ili waweze kuwa na Afya njema wajitahidi kushiriki Michezo mbalimbali ikiwemo mpira wamiguu,riadha,mbio za baiskeli na michezo mingine ili kuzilinda Afya zo.


Akizungumzia watu wanaopita kufanya kampeni chafu jimboni Dk Kamani alisema,ndugu zangu wananchi wa Malangale, kuweni macho na watu wanaopita kuwarubuni,maendeleo hayatapatikana kwa kugawiwa fedha kwa mtu mmoja mmoja bali nawashauri kuwa fursa ziko nyingi hebu undeni vikundi vya ushirika ili Serikali iweze kuwapa ruzuku katika shughuli za Uvuvi.


“Serikali kwa sasa inatoa ruzuku ya asilimia arobaini ( 40 ) kwa wanaushirika wa vikundi vya Uvuvi ili ziwasaidie kununua mitumbwi na Nyavu kwa ajili ya shughuli za Uvuvi changamkieni fursa hii kwani mimi niko tayari kuwaonyesha njia ili muweze kunufaika na sekta hii ambayo iko katika eneo lenu.alisema Dk Kamani.

WANASAYANSI WANASEMA KUWA WAMEFANYA UGUNDUZI MKUBWA KATIKA JITIHADA ZA KUTIBU UGONJWA WA UKIMWI KWA KULAZIMISHA VIRUSI KUONDOKA KATIKA MAFICHO YAO MWILINI


Virusi vya HIV
Wanasayansi wanasema kuwa wamefanya ugunduzi mkubwa katika jitihada za kutibu ugonjwa wa Ukimwi kwa kulazimisha virusi kuondoka katika maficho yao mwilini.

Virusi vya HIV huganda na kujificha katika DNA ya mgonjwa na kuishi humo kwa miaka mingi bila ya kufanya chochote, hali ambao inatatiza juhudi za kupata tiba.
Awamu ya kwanza ya utafiti huo uliofanyiwa wagonjwa sita, ilionyesha kuwa matibabu ya chemotherapy ambayo hupewa wagonjwa wa Saratani, kwa kiwango kidogo yanaweza kuamusha virusi hivyo kutoka katika maficho yao.

Wataalamu wanasema matokeo haya ni ishara nzuri , lakini huenda isiwezekane kwa matibabau hayo kuangamiza virusi vya HIV kabisa.

Dawa za kupunguza makali ya HIV, zinaweza kupunguza idadi ya virusi kwenye damu , maana kwamba waathiriwa wa HIV wanaweza kuwa na maisha ya kawaida tu licha ya kuwa na virusi mwilini.

Lakini kuna tatizo moja hapa. Virusi vya HIV pia vinaweza kugandisa DNA yake kwenye DNA ya binadamu, na hapo inakuwa changamoto kwa matibabu kwani dawa haziwezi kivifikia.

Wakati mgonjwa anapoacha kutumia dawa zake, virusi hivyo huamka upya na kuanza kushambulia mwili.

Utafiti sasa unalenga kuangalia mbinu za kuondoa virusi hivyo kutoka katika maficho yao na kuviua.

'Chemotherapy'

Matibabu ya Chemotherapy

Kikundi cha madaktari kutoka chuo kikuu cha Aarhaus nchini Demark, walijaribu kutumia dawa inayotumiwa katika matibabu ya Chemotherapy, Romidepsin, ambayo hutumiwa kwa wagonjwa wa Saratani.

Wagonjwa sita ambao waliokuwa na kiwango kidogo sana cha virusi mwilini, walihusishwa katika utafiti huo
Wote walipatiwa dawa ya Romidepsin mara moja kwa wiki katika kipindi cha wiki tatu.

Katika wagonjwa watano, kiwango cha virusi mwilini kilipanda.Ishara kuwa virusi hivyo vilikuwa vinatoka katika maficho yao.

Mmoja wa madaktari waliohusika na utafiti huo,Dr Ole Sogaard, alisema kila hatua ya utafiti wa kutafuta tiba ya HIV ni muhimu kwake na humpa raha.

Alisema licha ya ugunduzi wao, baadhi ya watu wana shaka na matibabu hayo wakisema haitoshi kuua virusi.
"tumeonyesha tunaweza kuondoa virusi kutoka katika maficho yao , hatua itakayofuata ni namna ya kuua virusi hivyo, '' alisema daktari Ole Sogaard
"hatua itakayofuata ni kuchanganya dawa ya Romidepsin ili kuimarisha kinga ya mwili, na hii kwetu sisi itakuwa chanjo ya HIV. ''

athari zinazotokana na matibabu haya ya Chemotherapy,ni pamoja na uchomu mwilini.

Moja ya changamoto ya matibabu haya ni kwamba madaktari hawawezi kusema kiwango cha virusi vya HIV kinachotolewa kutoka katika maficho yao.

NEC Misungwi yaitaka TANROADS kutoa Elimu

Na Antony Sollo Mwanza.
July 22, 2014

MJUMBE wa mkutano Mkuu wa chama cha Mapinduzi Wilayani Misungwi Jackob Dalali Shibiliti amewataka wakala wa Barabara Nchini TANROADS Mkoa wa Mwanza kufika katika kijiji cha Misasi Wilayani Misungwi kuzungumza na wananchi kuhusu operesheni ya bomoabomoa ya nyumba zilizo ndani ya hifadhi ya barabara.

Akizungumza na Tanzania Daima Shibiliti alisema kuwa juni 6 mwaka huu  wakala wa barabara Mkoa wa Mwanza,walipita wakitangaza juu ya Operesheni hiyo ambayo itafanyika kupisha ujenzi wa barabara ya Mwanangwa Salawi lakini akishangazwa na uamzi usio shirikishi kwa wananchi kwa kuwa,hakuna mkutano wowote uliowakutanisha wadau na kujadili faida za ujenzi wa barabara hiyo.

Katika ufuatiliaji wake Mjumbe huyo wa NEC alikutana na watendaji wa TANROADS Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo ya kina huku akiwaomba wafike katika vijiji vinavyopitiwa na mradi huo kwa ajili ya kutoa Elimu kwa wananchi hao.

Shibiliti amevitaja vijiji vitakavyopitiwa na mradi huo kuwa ni Mwawile, Misasi, Kijima Busongo, kabala, Mwagiligili na Inonelwa na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupatiwa elimu hiyo ili kuweza kujua faida na hasara ya mradi huo.

Wakitoa maoni yao baadhi ya wazee wa maeneo ya Misasi akiwemo Msafiri Mchenya wameishauri Tanroads kuangalia uwezekano wa kuipitishia barabara pembeni mwa mji kwa ajili ya kuondoa usumbufu kwa wananchi na pia kuepuka matumizi mabaya ya fedha za umma kwa, kuwa hakukuwepo taarifa na elimu juu ya hifadhi ya barabara tangu mwanzo hivyo kuonekana kuwa jambo hili sasa ni jipya.

Tanzania Daima lilifika Ofisi za wakala wa barabara kujua hatma ya mchakato huo na kukutana na Mhandisi wa Barabara kuu Mkoa wa Mwanza Pius Joseph ambaye alikanusha madai hayo na kusema kuwa lengo lililowapeleka huko ni kutoa elimu juu ya sheria mpya ya hifadhi ya barabara na 13 ya mwaka 2007 (Road Act No 13 of 2007).

Pius alisema kuwa, kwa mujibu wa kanuni ya 29 (1)A na B ya mwaka 2009 ya sheria hii eneo la hifadhi ya barabara limeongezeka na kuwa mita 60 (sitini) yaani mita 30 kuanzia katikati ya barabara kila upande kwa barabara zote kuu na Mkoa.

Mhandisi Joseph aliendelea kufafanua kuwa hapo awali eneo la barabara lilikuwa ni mita 45 yaani mita 22.5 kila upande wa barabara na kusema kuwa kuanzia sasa wananchi wafahamu kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria kujenga nyumba,kufyatua matofali,kulima au kufanya shughuli yoyote ndani ya mita 60 (sitini) yaani mita 30 kila upande wa barabara.

Tanzania Daima linayo nakala ya maelekezo ya Meneja wa wakala wa barabara Mkoa yenye kumb Na TNRD/RM/MZA/B.1570/VI/40 ikifafanua juu ya kwenda kwa wataalamu hao wilayani misungwi kwa lengo la kutoa elimu na si kwenda kutoa taarifa ya kuvunjwa kwa nyumba za wananchi wilayani humo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Nathan Mshana alipotafutwa kuzungumzia suala hilo simu yake iliita bila kupokelewa na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Mwisho.

Madaktari nchini India wametumia saa 7 kufanikisha upasuaji wa kinywa cha kijana Ashik Gavai mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa akipata maumivu ndani ya kinywani

Dr Sunanda Dhiware, mkuu wa Kitengo cha tiba ya meno katika hospitali ya JJ mjini Mumbai ameiambia BBC kuwa wamefanikiwa kuyang’oa meno 232 kinywani mwa Ashik aliyeletwa hospitalini hapo akiwa amevimba taya huku akilalamika kwa maumivu makali. 
 
Madaktari wamesema wamelazimika kutumia nyundo na tindo kuyatoa meno hayo na wakadai kwamba hilo ni tukio la ajabu na linaingia katika rekodi ya dunia.Hata hivyo Upasuaji huo umehusisha jopo la madaktari wanne.
Dr Dhiware anasema katika uzoefu wake wa miaka 30 ya udaktari wa kinywa na meno hajawahi kukutana na tukio la namna hiyo. Ameongeza pia kuwa kulingana na vitabu vilivyopo vinasema hali kama hiyo inaweza kujitokeza katika taya la juu na meno yaliyowahi kung'olewa katika hali hiyo yalikuwa 37 lakini cha kushangaza ni kuwa tukio la Ashik Gavai limetokea katika taya ya chini na ameng'olewa meno 232 idadi ambayo ni kubwa huku akisalia na 28 kwa matumizi yake ya kawaida wakati kitaalamu mtu mzima anapaswa kuwa na meno 32.
Baba mzazi wa kijana Ashik ,Suresh Gavai amenukuliwa akisema mtoto wake alikuwa akilalamika kwa miezi kadhaa juu ya maumivu na kwamba walidhani inaweza kuwa ni matatizo ya saratani na ndipo wakamleta Mumbai.

Habari na BBCswahili.com

Dk Kamani apata mwarobaini wa mauaji ya walemevu wa ngozi albino


Na Antony Sollo  Busega
July 22.2014

MAUAJI ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) huenda yakabaki historia wilayani Busega,hii ni kufuatia juhudi zinazofanywana Mbunge wa jimbo hilo, Dk. Titus Kamani, kuanzisha ujenzi wa kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa Ngozi ikiwa ni pamoja na shule yao.

Hayo yamejiri kufuatia ziara ya Mbunge wa Jimbo la Busega Dk. Titus Kamani iliyoanza mapema mwezi huu ambapo aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari ujenzi wa kituo hicho umeshaanza katika Kijiji cha Lukungu, Kata ya Lamadi, jimboni hapa.

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Lamadi, Dk. Kamani alisema  kwamba,kituo hicho kitagharimu Sh bilioni 1.5, na kwamba kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuhudumia watoto zaidi ya 100 kwa wakati mmoja.

Dk. Kamani ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi alimshukuru Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kumuunga mkono Katika ujenzi huo kwa kuchangia Sh milioni tano.

Dk Kamani Alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni miongoni mwa mambo ambayo amedhamiria kuyatekeleza katika Jimbo la Busega kwa manufaa ya jamii nzima kwani jamii imezungukwa na makundi mbalimbali wakiwamo walemavu wa ngozi,wasioona nk huku kila kundi likihitaji huduma na kwamba ameguswa kusaidia makundi hayo kwa moyo wa dhati.

“Albino ni kundi maalum la watu ambao wamekuwa wakisahaulika katika jamii, ninamshukuru Waziri Mkuu ambaye pia ni mlezi wa walemavu hao kuguswa na jitihada zangu na kuniunga mkono kwa kunichangia kiasi hicho cha fedha,” alisema Dk. Kamani.

Aliomba taasisi mbalimbali na watu wenye uwezo kumuunga mkono kwa hali na mali Katika kulinda na kuokoa maisha ya walemavu hao.

Mratibu wa Kituo hicho, Moody Gimonge, alisema kitakapokamilika kitaanza kuchukua walemavu wa wilayani Busega wanaolelewa katika vituo vya Shule ya Msingi Mwisenge mkoani Mara, Buhangija mkoani Shinyanga na sehemu nyingineza wilayani.

“Tuna walemavu wa ngozi 22 wanaolelewa Mwisenge na wengine zaidi ya hao wako Buhangija, pindi kituo hiki kitakapokamilika tutaanza kwa kuwachukua kwanza hao walioko katika vituo hivyo ili vipate fursa ya kusaidia watoto wengine,” alisema.

Alieleza kusikitishwa kwake na watu wanaoanzisha vituo vya aina hiyo kwa
ajili ya maslahi kujipatia yao binafsi badala ya kuwa na dhamira ya dhati
ya kuwasaidia walemavu hao kama ambavyo Dk. Kamani ameonesha dhamira ya kweli kwa vitendo.

Mwisho

APIGWA SHOKA LA KICHWA BAADA YA KUFUMANIWA NA MKE WA MTU

Baada ya madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kupambana kuokoa maisha ya jamaa huyu mkazi wa Mwanza, aliye fumaniwa na kupigwa Shoka ya Kichwa akiwa na mke wa mtu, hatimaye wamefanikiwa kuchomoa shoka hilo kichwani lakini hali yake bado mbaya akiwa katika chumba cha ICU kwa uangalizi zaidi. ''Mke wa mtu sumu'

KICHANGA CHATELEKEZWA USAGARA

Na Antony Sollo Mwanza
July 22, 2014.
KITOTO kichanga chenye umri wa miezi miwili kimetelekezwa katika maeneo ya Usagara Wilaya ya Misungwi Mkoani mwanza   barabara ya Kigongoferry kuelekea Sengerema na Geita.

Akizungumza na Tanzania daima Afisa mtendaji wa Kijiji cha usagara Raymond Mahumbi alisema kuwa tukio hilo lilitokea julai 21  majira ya saa 2:00 asubuhi huko Usagara ambapo alipewa taarifa za kutelekezwa kwa kichanga hicho ndipo alipokwenda katika eneo la tukio na kukuta kichanga hicho kikiwa kimetelekezwa katika nyumba ya Mapambano Wilson.

 Imedaiwa kuwa julai 21  majira ya saa 2:00 asubuhi  mama wa kichanga hicho alifika nyumbani kwa Mapambano na kuomba maji ya kunywa mara baada ya kunywa maji hayo, mtu aliyemhudumia alirudisha kikombe ndani na aliporudi hakuweza kumkuta mama wa kichanga hicho kwani alikuwa ametokomea kusikojulikana na kukiacha kichanga chake hicho sebuleni hapo.

“Mama wa kichanga hiki alifika hapa nyumbani akaniomba nimsaidie maji ya kunywa,nilimpatia na nilirudisha kikombe ndani nilikikuta kichanga hiki kikiwa peke yake kinalia na nilipojaribu kuchungulia huku na huku sikuweza kumuona mama huyo ndipo nilitoa taarifa kwa Afisa Mtendaji wa kijiji”alisema Mapambano .  

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema mama wa huyo amefanya kitendo kisichokubalika katika jamii hivyo wanannchi hao wamekilaani kitendo hicho kwa nguvu zote na kuomba kutoa ushirikiano kwa mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za mama huyo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Valentino Mlowola  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa,Jeshi la Polisi linamsaka mama huyo ili akipatikana aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria kufuatia kitendo cha kikatili alichokifanya kwakuwa ni kitendo kisichokubalika katika jamii.
Mwisho
 
UHURUTZ © 2010 | DESIGNED BY ZEPHANIA RICHARD KAYAGA