Ads Top

JE BAJETI HII ITAINUSULU CCM 2015?





























UGUMU wa maisha kwa wananchi walio wengi, kukosekana kwa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo afya, maji, umeme na miundombinu ni miongoni mwa mambo yanayochangia Chama tawala (CCM) kukosa mvuto kwa wananchi.
Hoja zinazotolewa na viongozi wa vyama vya upinzani wanapotafuta kuungwa mkono na wananchi ni umasikini uliopindukia unaokabili idadi kubwa ya wananchi huku matajiri wachache wakifaidi uchumi wa nchi hii.

Miongoni mwa mambo yanayosababisha uchumi kudorora ama kukua kwa uchumi wa nchi ni pamoja na bajeti ya serikali ambayo ndani yake hueleza mikakati yake katika kukusanya mapato ya nchi, vyanzo vya mapato na jinsi ya kutumia mapato yaliyokusanywa.

Wiki iliyopita, serikali kupitia Waziri wake wa Fedha na Uchumi Dk William Mgimwa, alisoma bajeti ya mwaka 2012-2013 ya serikali ambapo jumla ya Sh15 trilioni zimepangwa kutumika katika mwaka ujao wa fedha.

Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza katika bajeti hiyo ni ongezeko la kodi za bidhaa mbalimbali, ikiwamo, bia, soda, sigara, juisi zinazoingizwa kutoka nje huku ikifuta msamaha wa ushuru wa bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa wananufaika na msamaha huo.

Bajeti hiyo pia inaonekana kuwakumbuka wananchi wa kima cha chini ambao ndio walio wengi kwa kufuta kodi ya mshahara kwa wafanyakazi wenye kipato cha kuanzia Sh170,000 badala ya Sh135,000 ya awali.

Waziri Mgimwa aliainisha mgawanyo wa matumizi katika bajeti hiyo kuwa ni Sh10.591 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati Sh3.781 trilioni ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma katika wizara, idara na wakala za serikali; huku Sh2.745 trilioni zikielekezwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Msomi na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Kanoa Mtewa, anasema kwa mtizamo wa haraka bajeti hii ni nzuri, endapo usimamizi na utekelezaji utazingatiwa na kutekelezwa vyema.

Dk Mtewa anasema asilimia 70 iliyoelekezwa katika matumizi ya ndani ina maana ni kulipa madeni ya wakulima wa pamba, korosho, kahawa na maeneo mengine yanayoidai serikali.

“Haya matumizi ya ndani maana yake ni watu walipwe, wakulima wa korosho, pamba, kahawa, na wananchi wengine wanaoidai serikali, sasa hawa kama watalipwa wataipenda serikali yao, na hii ni wazi kuwa utekelezaji ukifanyika serikali ya CCM itarejesha matumaini kwa wananchi walio wengi,” anasema Dk Mtewa.

“Haya matumizi ya ndani maana yake ni kuwa watu walipwe, kama watalipwa wataipe muda serikali yao, wasipolipwa hapo ndipo kutakuwa na shida, maana watu watachukia serikali, na hivyo inaweza kuanguka.”

Anaongeza kuwa ili kusiwe na anguko kwa serikali na chama tawala, inatakiwa mambo yasimamiwe vizuri, viongozi wasilale, watembelee watu wasikilize matatizo ya wananchi na wayafanyie kazi.

Anaonyesha wasiwasi wa utekelezaji kwa kusema, wakati wote serikali imekuwa na mipango mizuri lakini tatizo lipo katika kuitekeleza.

Anasema si vyema watu kuitazama bajeti kwa mambo madogo kama kupanda kwa soda, bia na kadhalika, badala yake watu wanapaswa waangalie mgawanyo wa matumizi wa bajeti ulivyoelekezwa na vipaumbele vilivyowekwa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba anasema bajeti ya mwaka huu imeendelea kuwa yenye manufaa kwa viongozi wa serikali na kuwaumiza wananchi wa hali ya chini.

Kibamba anasema bejeti ya wananchi, ingetakiwa iguse sekta mbalimbali zitakazowanufaisha wananchi moja kwa moja, lakini akasema bajeti iliyosomwa mwishoni mwa wiki iliyopita haijaonekana kuwagusa wananchi zaidi ya kuwaumiza.

“Ukiangalia bajeti ya 2012-2013 , sehemu yenye mapato na matumizi, utagundua maeneo ya mapato yana matatizo makubwa na yale ya matumizi yana matata makubwa…. Bajeti inatakiwa iguse maisha ya wananchi, lakini hii inalenga katika kuneemesha miradi mikubwa ambayo haiwanufaishi wananchi moja kwa moja,” anasema Kibamba.

Anasema kwa mtazamo wake, serikali ya CCM imekuwa na tatizo la kuongeza bajeti kila mwaka ambapo anasema tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, bajeti imekuwa ikoongezeka kutoka Sh 4 trilioni mpaka Sh15 trilioni, huku vyanzo vya mapato vikiwa vile vile vinavyomuumiza mwananchi.

“Leo nikiambiwa nieleze bajeti ya mwaka 2015 nitaeleza tu, maana hakuna jipya…, nitakwambia vyanzo vya mapato ni katika soda, bia, konyagi, sigara na mishahara ya wafanyakazi, ndio kitu ambacho wataalamu wa uchumi wa nchi hii wanachokijua, ukiwaambia vyanzo vya mapato ni katika migodi ya madini, gesi na dhahabu, wanajifanya hawaelewi…, hii ni hatari na inaonyesha udhaifu mkubwa kwa watendaji wa serikali,” anasema.

Anasema vyanzo vya uhakika vya mapato visivyomuumiza mwananchi ni kuvunja mikataba mibovu kwa makampuni ya uchimbaji wa madini, ambapo anasema gharama za kuvunja mikataba hiyo endapo makampuni hayo yataishtaki nchi ni ndogo kuliko mapato yatakayopatikana kupitia marekebisho ya mikataba hiyo.

“Nimekuwa nikiishauri serikali, badala ya kumnyonya mwananchi kwa kumbebesha mzigo wa kodi usio wa lazima, itoze kodi zaidi kwenye madini, wanaogopa kwenye mikataba ya kimataifa Ni heri kulipa Sh100 bilioni kama gharama za kuvunja mkataba, kisha uvune Sh 1trilioni kutokana na kutoza kodi inavyostahili,” anasema Kibamba.

Kibamba anasema kutokana na mchanganuo huo, haoni serikali ya CCM kunusurika na hasira za wananchi walio wengi ambao bajeti imeonekana kuwazidishia makali ya maisha.

“Kwa bajeti hii, CCM iko kwenye ukingo, inatakiwa iendelee kuomba maana upepo ukivuma tu itaanguka, maana moto wa wananchi kwa CCM umeshuka, na unaendelea kushuka na hii kutokana na kukosekana kwa ubunifu kwa wataalamu wa uchumi wa serikali.

Profesa Humphrey Moshi, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema bajeti ya 2012-2013 ni mchanganyiko ambayo haielezi wazi madhumuni ya serikali.
Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja katika kituo cha utangazaji cha TBC, Profesa Moshi anasema bajeti hiyo imekuja na mambo mengi, huku ikiyachanganya na yale ya zamani na kusababisha kukosa uelekeo wa madhumini ya Serikali.
‘Haiko wazi, imeshindwa kufafanua kwa uwazi endapo kiasi fulani cha fedha kitafanya kazi hii na hiki kitatumika kufanya kazi ile…, hapa ilipaswa kufafanua vipaumbele vyake na kasma zake kwa uwazi.”
Anatoa mfano kuwa bajeti hiyo imezungumzia reli ya kati pekee, badala ya kuzungumzia na reli ile ya Arusha, na kusisitiza kama ni miradi ya reli ingetakiwa kutengewa fedha na kujengwa kwa pamoja ili kuepuka marudio ya ujenzi wa aina hiyo.
Anaongeza kuwa bajeti hiyo haijafafanua endapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya maeneo kama katika sekta ya kilimo zitakavyotumika na hivyo kuacha maswali badala ya kutoa majibu.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.