Ads Top

MH MNYIKA ATIMULIWA BUNGENI KWA KUSEMA KUWA RAIS KIKWETE NI DHAIFU

































Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika akiingizwa na askari wa bunge kwenye gari baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru atolewe nje ya viwanja vya bunge baada yambunge huyo kugoma kufuta kauli yake kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

 BUNGE jana lilichafuka tena baada ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kusema kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, kauli ambayo ilisababisha Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru atolewe bungeni.Mnyika alitoa kauli hiyo wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13, ambapo alieleza kuwa analazimika kusema Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, wabunge ni wazembe na nchi imefika hapa ilipo kutokana na upuuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

"Mimi nasikitishwa na jambo moja, tumefika hapa kutokana udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa bunge na wabunge na tumefika hapa kutokana na upuuzi wa CCM, nasema hivi nina ushahidi.”

Lukuvi/ Ndugai
Kauli hiyo ya Mnyika ndio ilichafua hali ya hewa  bungeni, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na Uratibu, William Lukuvi ndipo alisimama na kuomba mwongozo wa Spika.
“Nataka kumbukusha Mnyika, kutokana na kauli zake, kwa kutumia kanuni ya 64 (d) ambayo inaeleza mbunge yeyote hatatumia jina la Rais kwa dhihaka katika mjadala au kulishawishi bunge kwa jambo lolote,” alisema Lukivi.

Aliendelea kufafanua kuwa, “Lugha kwamba Rais Kikwete ni dhaifu, CCM ni wapuuzi nilikuwa naomba, Mheshimiwa Mnyika, miongoni mwa watu ninaowaheshimu sana, nadhani katika hili, amepotoka naomba afute kauli yake.”
Baada ya kauli hiyo ya Lukuvi, Ndugai alifafanua zaidi kuhusu jambo hilo akisema ni kweli kanuni inajieleza vizuri sio tu katika maneno yake pia amelisema vibaya Bunge hilo na kumtaka afute kauli hiyo.

Mnyika alisimama na kuomba apewe nafasi ya kufafanua kauli yake ya kwanini Kikwete ni Rais dhaifu, lakini Naibu Spika, alimuomba afute kauli yake, kitu ambacho mbunge huyo aligoma kufanya, badala yake akasisitiza bunge limpe nafasi ya kufafanua.
Kutokana na uamuzi wa kumtimua Mnyika bungeni.

Ndugai alisema mbunge anapotoa lugha ya matusi au maudhi na akatakiwa na kiti cha Spika afute kauli yake na bado akagoma, ni mamlaka kwa kiti hicho kumtoa nje ya bunge katika muda uliosalia au hata kumsimamisha asihudhurie vikao vitano vya bunge.
Ndugai aliamuru walinzi wamtoe Mnyika nje mara moja na kumzuia asishiriki shughuli yoyote ya bunge hadi kesho saa 3:00 asubuhi.

“Ndugu wabunge tunaongozwa kwa utaratibu, nikitoa uamuzi wangu kwa Kanuni ya 73 (2), ambayo inaeleza kuwa, mbunge au waziri atakayetoa lugha ya maudhi atatatakiwa na Spika ajirekebishe na akikataa atakaa nje kwa muda wote ulisalia katika kikao cha siku hiyo. Nikiwa Naibu Spika ninayejiamini, uamuzi ambao nauchukua sasa, Askari mliopo hapa naagiza mumtoe nje mheshemiwa Mnyika mara moja,” aliagiza Ndugai.

Kabda ya tukio hilo, Mnyika alichangia bajeti hiyo kwa maneno makali dhidi ya wabunge wa CCM wanavyopigania bajeti ya Serikali isiyotekelezeka, huku akiwafananisha na mtu asiye na akili timamu (chizi), kwamba yeye akiendelea kupambana nao ndio ataonekana chizi zaidi.
 “Mtu ukiwa unamkimbiza chizi wewe ndio utaonekana chizi zaidi, hivyo siungi mkono na waache machizi waendelee na uchizi wao,” alisema.

Kauli hiyo ya Mnyika inaonekana kutaka kujibu mapigo ya kikao cha juzi ambapo mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba wakati akichangia bajeti, alisema kuwa wapinzani ni wanafiki, waongo, wana mapepo na wanapaswa kuombewa na kupimwa akili.

Alisema bajeti hiyo haiendani na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano, ambao ulisainiwa na Rais  Kikwete na pia haiendani na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo akashangaa kauli za wabunge wa chama tawala kuishambulia Bajeti ya Upinzani kwa maneno ambayo aliyasema anaweza kuyafananisha na uchizi.

“Wanasema mipango, unafikia kusema maneno mengine ni ya uchizi uchizi, hivi kutokana na maeneno yaliyotekelezwa, kama ya upinzani haitekelezeki, lakini tumezungumza pensheni ya wazee katika bajeti iliyopita, kwa bahati mbaya wabunge hawa wa CCM sijui hamuwasikilizi hata viongozi wenu?" alihoji Mnyika.

Alifafanua kuwa ,"Suala la malipo ya pensheni kwa wazee, hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kulizungumza mjini Morogoro katika sherehe za wazee, na aliahidi Serikali itakwenda kutoa pensheni ya wazee.  Sasa hapa unaposema haitekelezeki ndio maana unafikia kusema kuna kauli nyingine kama ni za uchizi uchizi hivi."

Alisema pia katika suala la ongezeko la mishahara hadi kufikia 315,000, wamerudia katika bajeti ya upinzani kwani linawezekana, sitaki kutaja hapa takwimu za wafanyakazi wote wa Serikali na malipo yao.

“Lakini, bunge lililopita tulitoa takwimu hapa jinsi ambavyo inawezekana mshahara kima cha chini ufikie 315,000 na ndio sababu leo tumerudia tena, kwani Serikali haijatekeleza, lakini kuna wapofu wa kumbukumbu ambao hawasomi kumbukumbu za bunge," alisema Mnyika.

Nje ya Bunge
Baada ya agizo hilo la Ndugai, askari wa bunge walimwondoa Mnyika na kumsindikiza hadi nje ya uzio wa bunge, ambako alizungumza na wanahabari na kufafanua kuwa, alisema Rais Kikwete ni dhaifu kutokana na sababu ambazo alikuwa nazo, ila hakupata nafasi ya kuzitaja.

Alisema sababu hizo zilitokana na bajeti ya Serikali ambayo ilisomwa bungeni, ambayo haitekelezeki na inakinzana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano.

“Bajeti hii ni matokeo ya udhaifu wa Rais Kikwete, narudia tena kwani yeye ndiye aliyesaini Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano kama Kiongozi Mkuu wa nchi tena kwa wino mwekundu, mpango ambao sasa unapingana na bajeti hii,” alisema.

Alisema pia Rais Kikwete ni dhaifu kwani ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na bajeti ilipita katika baraza hilo, lakini imedhihirika kwamba haikuzingatia kuzingatia mpango wa maendeleo, pia kushindwa kutekelezwa kwa bajeti iliyopita ni matokeo pia ya udhaifu.

"Mnyika alisema pia kwa mujibu wa Katiba, Rais ndiye anapeleka bajeti bungeni, Waziri mwenye dhamana anapeleka tu kwa niaba. Hivyo Rais amepewa mamlaka makubwa juu ya bajeti, hivyo Rais Kikwete anapaswa kuagiza Waziri wa Fedha bajeti iondolewe irudi kwenye Baraza la Mawaziri ikafanyiwe marekebisho kama atataka," alisema.

Hata hivyo, alisema kutokana na ubovu wa Katiba, michango ambayo inaendelea sasa bungeni, haitaweza kupinga bajeti kwani inatakiwa ipitishwe kwa kupiga kura kwa kila mbunge, na kama wabunge wengi wakipinga ina maana Rais atalivunja bunge na hivyo kufanyika uchaguzi mwingine, kitu ambacho wabunge wa CCM hawatakubali.

Nassari alia na wabunge wa CCM

Katika hatua nyingine, kutokana na uamuzi huo wa kutolewa nje Mnyika, wabunge kadhaa wa Chadema pia walitoka kwa hiari yao, akiwapo Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari ambaye alisema wakati anagombea ubunge hakudhani kuwa bunge kama chombo kikubwa cha uamuzi, chenye umuhimu mkubwa kwa Watanzania hasa kipindi hiki cha kupitisha bajeti, linaweza kutumiwa kama mkutano wa chama na kutupiana mipasho.

“Nimesikitika sana nimeona ni bora nitoke, bunge limekuwa la mlengo wa kisiasa na kupeana mipasho, nasikitika Mnyika kutolewa nje.

Alisema Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alitoa kauli za kuudhi wapinzani, lakini spika alimwambia arejee maneno yake mara ya pili,” alisema Nassari.

Kabla ya Mnyika kutolewa nje, Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa, pia alionywa na Ndugai kutokana na kutoa kauli za kumpinga pale alipomtaka Mnyika afute kauli yake.

“Naomba wananchi wa Iringa mjini, kupitia Mchungaji Msigwa ni vizuri kuwa na nidhamu kwa bunge hili. Hiki ni kikao kikubwa, anayezungumza ni Mnyika nimemkataza kuita mtu chizi…, muache hii habari ya kuropoka kama una jambo simama, kiti ndio kina uamuzi wa mwisho,” alisema Ndugai.

Pia Ndugai, alikataa mwongozo wa Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje ambaye alitaka mwongozo, kuhusiana na kauli za kuudhi ambazo zilitolewa juzi na Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi.

Nchemba atuzwa Sh210,000
wa Uchumi na Fedha wa CCM, juzi alituzwa Sh210,000 baada ya kuiponda bajeti ya upinzani na kuiita ni ya kipuuzi na haitekelezeki, wapinzani wamejaa uigizaji na kumrushia kombora Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa anawahadaa Watanzania kwa kukataa gari kuukuu, na baada ya ya kupewa jipya alikubali kimya kimya.

Nchemba akizungumza na waandishi nje ya bunge, alisema jumla ya fedha alizopewa na wabunge na mawaziri kadhaa zilifikia Sh210,000.
                      
Mchango wa Lusinde

Mbunge wa Mtera-CCM, Livinstone Lusinde alisema bajeti ya upinzai ya uongo na haitekelezeki.

Lisinde huku akieleza kumuunga mkono, Nchemba alisema yaliyoandikwa hayana uhusiano na ilani ya uchaguzi wa Chadema, kwani waliwahi kusema watatoa elimu bure lakini suala hilo halimo kwenye bajeti.

Kauli hiyo ya Lusinde ilimfanya Naibu Spika kumtaka airejee tena, naye akarudia maneno yake kuwa hutuba
hiyo ya bajeti kivuli ya upinzani inatofautiana na Ilani ya Uchaguzi ya Chadema kwani suala la elimu bure halipo.

Lusinde pia alimrushia alisema Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, anajidai kukataa posho ya Sh80,000 lakini, anakubali malipo ya Sh2 milioni kwa mwezi huku akitembelea gari la kifahari la Serikali.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.