Ads Top

MGODI WA WILIAMSON NA MAUAJI YA KINYAMA SERIKALI KIMYAAA!!



kaburi la marehemu Dotto James huko Mwanzuki Mwadui Luhumbo Wilayani Kishapu


Na Antony Sollo Shinyanga.
Katika hali isiyo ya kawaida yametokea matukio mawili yaliyosababisha majonzi mazito kwa wakazi wa kijiji cha Maganzo pamoja na Mwadui Luhumbo na vitongoji vyake hususani tarafa ya Mondo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.
Hii ni baada ya mnyama anaye tambulika kama fisi kudaiwa kumla binadamu na hatimaye kummaliza kabisa jambo ambalo limezua maswali mengi miongoni mwa wakazi wa kata ya songwa Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.
Baada ya mwandishi wa habari hizi kufika eneo la tukio alijionea hali halisi ya tukio na baada ya kufanya uchunguzi kujua kulikoni alikutana na kiongozi mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema ana mashaka sana na maelezo yaliyotolewa kwa mtindo wa funika kombe mwanaharamu apite.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi kiongozi huyo alisema kuna kitu kilichofichwa kuhusiana na tukio hili kwa vile ni vigumu mno kwa mtu kuliwa na fisi hadi mwili wake kuisha kabisa isipokuwa inaonekana marehemu aliuawa na baadaye kutupwa na hatimaye maiti yake kuliwa nafisi hadi kumalizwa na mnyama huyo na kuwataka polisi kuwa makini katika ufuatiliaji wa matukio ya aina hiyo,badala ya kutoa majibu rahisi katika masuala mazito kama hayo.

Katika tukio lingine lililotokea katika kijiji cha Mwadui Luhumbo kitongoji cha Mwanzugi Wilayani Kishapu,kijana aliyejulikana kwa jina la Dotto James Ngong’ho ameuawa katika mazingira ya kutatanisha baada ya kutekwa na Askari wa mgodi wa Wiliamson Diamond Limited huko Mwadui Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.
Akisimulia mkasa mzima kijana mmoja aliyekuwa na marehemu siku ya tukio amesema siku ya jumamosi ya tarehe 15 mwezi wa tisa walikwenda katika shughuli zake za kutafuta madini aina ya Almasi katika maeneo ya mgodi wa Mwadui  ambapo walipofika katika eneo hilo,walikuta kulikuwa na ulinzi mkali uliokuwa umeandaliwa kukabiliana na wachimbaji hao ambao idadi yao walikuwa ni kundi la vijana 12,baada ya  kundi hilo kuingia katika pampu ya kutolea makapi eneo la Delfa askari wa mgodi huo walianza kuwamiminia risasi zinazotumia gololi maarufu kama blankoo na ndipo wachimbaji hao maarufu kwa jina la WABESHI walianza kukimbia na ndipo marehemu alitekwa na walinzi na kupelekwa kusikojulikana na hatimaye kuonekana akiwa hoi na baada ya muda mfupi alifariki dunia.
Akizungumzia kwa undani zaidi suala la kifo hicho Diwani wa kata ya Mwadui Luhumbo bwana Paul Magembe amesema kuwa amesikitishwa sana na tukio hilo ambalo linaashiria ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu maana si tukio la mara ya kwanza kutokea Wilayani humo na hususani maeneo ya Mwadui Luhumbo na vijiji mbalimbali vinavyozunguka mgodi wa Wiliamson
 Diwani huyo ameiomba Serikali kuhakikisha kuwa inachunguza kifo hiki kwa umakini mkubwa ili walinzi wa mgodi waliokuwa zamu siku ya tukio watakapobainika kuhusika moja kwa moja na tukio hilo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
“ndugu yangu matukio haya sasa yamezidi na huu si wakati muafaka kwa wananchi kuendelea kuuawa na Serikali kuyafumbia macho masuala mazito kama haya,nitatumia uwezo wangu wote na nguvu zangu zote kuhakikisha suala hili linawafikia viongozi ngazi za juu ili haki iweze kutendeka dhidi ya waliohusika na mauaji haya kwa kijana huyu aliyekuwa tegemeo la familia hii”.
Naye Kamanda wa polisi Wilayani Kishapu alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa kifo hiki kimetokana na wachimbaji hao kupigana wenyewe kwa wenyewe jambo ambalo limepingwa vikali na wananchi pamoja na familia yote kwa ujumla.
Mwandishi alimtafuta kamanda wa Polisi Mkoa wa shinyanga kuuliza kuwa ni hatua zipi zinafuata baada ya familia kutaka ufanyike uchunguzi dhidi ya tukio hilo ambapo Kamanda huyo alisema kuwa ni vyema wanafamilia hao wakaiandikia barua Mahakama kuomba kufanyika uchunguzi huo jambo ambalo ndiyo utaratibu unaopaswa kufanyika iwapo kuna matukio ya aina hii.
Baada ya majibu ya kamanda wa Polisi mwandishi alipiga kambi kwenye familia kujua iwapo familia iko tayari kutekeleza ushauri wa kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga,familia kwa pamoja walikuwa na kauli ya pamoja tu iliyotaka kutekelezeka kwa suala hilo lakini familia ikaenda mbali zaidi kwa kutoa mapendekezo yafuatayo:
1.    Wameiomba Serikali iunde tume maalumuitakayokuwa na wataalamu mbalimbali kushughulikia taarifa hii kuhakikisha  taarifa haina mashaka kuondoa utata katika jambo hili.
2.    Askari wa mgodi waliokuwa zamu siku hiyo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili haki itendeke.
3.    Wanamuomba Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake kufika katika maeneo yao kujua matatizo yanayowasibu wananchi hao kwa vile si muda mrefu walichomewa nyumba zao na hakuna aliyewasikiliza hali iliyozaa sintofahamu!
4.    Kwa vile eneo hilo la mgodi kuna ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu,ukatili wa kijinsia na ubakaji wanaomba kufutiwa leseni kwa kampuni ya ulinzi ya ZENITH SECURITY hii inatokana na wafanyakazi hao kukithiri kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za Binadamu kwa kiwango kikubwa kuliko maeneo mengine nchini.
Maombi haya yametokana na kile kinachoonekana kama kuna jambo lisilo la kawaida katika mauaji haya kwa vile polisi hawajawakamata walinzi wanaotuhumiwa kumuua marehemu Dotto James huku mazingira yote yakiwa wazi kwamba wahusika ni wao.

5.    Wanaiomba Serikali iunde tume kuchunguza mauaji hayo kwa maana polisi inatoa majibu rahisi utadhani amekufa ng’ombe na hata ng’ombe hufuatiliwa sana

Mwisho.

1 comment:

  1. Wananchi wamekuwa wakipotoshwa sana. Hapa hatuwezi kuwasingizia moja kwa moja wana siasa, bali Watu wenye uwezo wamekuwa wakiwatumia watanzania wasiokuwa na Elimu na vipato vizuri kuwadanganya kuvamia maeneo ya wawekezaji. Kwanza ijulikane kuwa Tanzania ni nnchi yetu sote, Na wawekezaji wa hapa nchini wanasaidia ajira watanzania wengi japo sio wote lazima waajiriwe ila mwekezaji ataajiri watu kulingana na mahitaji ya shughuri zake. Mwekezaji ni sawa na Mpangaji mwenye mkataba harali na mwenye nyumba. Je unafikiri ni rahisi kumwambia leo sisi watoto wa mwenye nyumba tunataka kuja kulala chumbani kwako? Hii ni kitu amabacho hakikubaliki mahala popote duniani. Hawa Watanzania wenzetu wamekuwa wakihadaiwa na matajiri wenye roho mbaya na kuwadanganya wananchi wasiokuwa na Elimu juu ya haki za wawekezaji ili wavamie eneo la mwekezaji. Inatakiwa tuwaonee huruma hawa watu, kwanza wamekuwa wakipatiwa malipo kidogo sana hata pale wanapopata almasi hulazimishwa kuwauzia matajiri hao kwa sababu tuu huwa wanawahudumia chakula nyakati zote wanapokuwa katika kazi zao za uchimbaji. Ni sawa mwekezaji ilifikia sehemu akatenga eneo kwa ajiri ya wachimbaji wadogowadogo maarufu kama walengwa. Wamepewa eneo katika Mgodi huo wa Mwadui ili wafanye shughuri zao. Bado wananchi hawa hataki kuridhika, na wanaendelea kuvamia eneo analochimba mwekezaji na kuiba mchanga. Na wakati mwingine huwa wanatumia siraha ili kushambulia askari wa Mgodi na Polisi. Hapo Mwadui kuna uharibifu mkubwa sana umefanywa na hawa wavamizi wajulikanao kama WABESHI. Magari ya mgodi kushambuliwa kwa mawe, Uvunjaji wa majengo ya ofisi za mgodi na mambo mengine mbalimbali yamekuwan yakitokea hapo Mwadui

    ReplyDelete

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.