Ads Top

VURUGU ZAIBUKA DAR KUFUATIA KUKOJOLEWA KWA QUR'AN

Baadhi ya wafanya furugu wakipambana na polisi
Mojawapo ya makanisa yanayosemekana kuharibiwa likiungua moto
Baadhi ya watuhumiwa wakipandishwa kwenye gari la polisi  
 
Na mwandishi wetu Stephano Simon
ENEO la Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam jana liligeuka uwanja wa mapambano kati ya makundi ya watu wanaosadikiwa kuwa ni Waislamu na polisi baada ya watu hao kuvamia Kituo cha Polisi Kidogo cha Maturubai kilichopo eneo hilo.
Watu hao walivamia kituo hicho wakitaka wakabidhiwe mtoto anayedaiwa kukojolea kitabu kitakatifu cha Quran ili wamwadhibu.
Vurugu hizo zilizoanza tangu saa nne asubuhi, zilisababisha makanisa matano kuchomwa moto, magari kadhaa kuvunjwa vioo na watu hao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema watu kadhaa wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo... “Siwezi kutaja idadi ya waliokamatwa, lakini kuna watu tunawashikilia kutokana na kufanya fujo, kwa sasa niko katika operesheni, nitazungumza kwa kirefu baadaye.”
Hata hivyo, Misime alisema hakuna kifo kilichotokea wala majeruhi.
“Pamoja na kwamba bado tupo katika eneo la tukio bado hatujashuhudia vifo wala majeruhi na tunaomba Mungu mambo hayo yasitokee.
Aliyataja makanisa hayo kuwa ni la TAG Kizuiani, Wasabato Kizuiani, TAG la Shimo la Mchanga na KKKT Mbagala Zakheim.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema uchomaji wa makanisa hayo ni kosa la jinai na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu hao.
Alisema katika vurugu hizo gari la Mkuu wa Polisi Wilaya ya Temeke (OCD) limevunjwa vioo.
Kamanda Kova alisema Jeshi hilo litaimarisha ulinzi katika makanisa hayo ili kuhakikisha kunakuwa na usalama.
Miongoni mwa magari hayo matano yaliyoharibiwa katika vurugu hizo ambazo zilisababisha Barabara ya Kilwa kufungwa kwa muda ni gari la Kituo cha Televisheni cha Clouds ambalo lilivunjwa vyoo.
Akizungumzia suala hilo, mkazi wa Mbagala Mission, Nassor Mohamed alisema vurugu hizo zilitokea baada ya mtoto mmoja kukojolea Quran.
Alisema mtoto huyo alifikia hatua hiyo baada ya kuwapo na ubishi na mtoto mwenzake ambaye wanasoma wote katika Shule ya Sekondari Chamazi.
Mohamed alisema mtoto huyo mwenye miaka 14, alikuwa akibishana na mwenzake mwenye umri kama huo kwamba mtu akikojolea kitabu hicho hugeuka kuwa nyoka.
Alisema kuwa mtoto huyo aliamua kufanya kitendo hicho ili kuona kama atageuka nyoka na wakati akifanya kitendo hicho mzee mmoja alimuona na kumhoji kisha kumpeleka kwa mama yake na kumshtaki.
“Yule mama aliwajibu kuwa kama ni hilo tu, basi awape hela wakanunue kingine. Aliposema hivyo wale watu wakakasirika wakamwambia, sisi tulikuja kukuambia kwa uzuri ili umwadhibu mwanao, lakini kutokana na majibu yako hatukuachii tena huyu mtoto,” alisema.
Alisema baada hapo, watu hao walimpeleka mtoto huyo katika Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Chamazi ambako waliandikiwa barua na kumpeleka kituo kidogo cha polisi kilichopo katika eneo hilo.
Jumatano jioni, watu hao walifika katika kituo hicho wakitaka wapewe tena mtoto huyo na ndipo walipoambiwa kuwa amehamishiwa katika Kituo cha Maturubai.
Alisema baada ya kumkosa mtoto huyo walihamasishana na kukubaliana kuwa baada ya kutoka msikitini kesho yake (jana), wakavamie kituo hicho na kumtoa mtoto huyo.
Wakati ghasia hizo zikiendelea, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Wilaya ya Temeke, Farid Salehe aliwasihi waumini wa dini hiyo kuwa watulivu.
Katibu wa Vijana wa Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam, Abdulkarim Kulao aliwataka Waislamu waliokuwa wamekusanyika katika eneo la kituo hicho cha polisi kurejea majumbani kwao kwani mtuhumiwa huyo alikuwa ameshahamishwa.
Baadaye Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanyisha baadhi ya watu waliokuwa wamekiendelea kubaki katika eneo hilo.
Askari waliokuwa na mabomu ya machozi walitawala eneo hilo kuweka ulinzi na hatimaye kufanikiwa kuwatawanya watu hao.
Baada ya kutimuliwa katika mkusanyiko huo, kundi moja la watu hao lilifika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Mbagala na kulichoma moto.
Mzee wa Kanisa hilo, Siaga Kiboko alisema mali kadhaa zimeharibika na kwamba walishatoa taarifa polisi.
Nyongeza na Raymond Kaminyonge

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.