WARAKA WA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA TUME YA KATIBA NA WAZIRI MKUU MSTAAFU JAJI MSTAAFU NA JOSEPH WARIOBA DHIDI YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS,MAHUSIANO NA URATIBU STEPHEN WASIRA
Aliyekua Mwenyekiti wa Tume ya Katiba na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira
Waziri
Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameandika waraka kumjibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira kwa kauli yake
kuwa ndiye aliyemkimbiza CCM kwenda upinzani mwaka 1995.
Katika
waraka wa maandishi alioutuma kwa gazeti hili, Jaji Warioba alisema
maelezo ya Wasira dhidi yake katika mahojiano maalumu na gazeti hili
hayakuwa sahihi na hivyo akamtaka ajifunze kusema ukweli kwa kuwa mambo
anayosema yanaweza kumrudia baadaye.
Waraka wenyewe huu hapa:
Tarehe 22 Septemba 2014, Gazeti la Mwananchi lilitoa taarifa ya
mahojiano kati yake na Mheshimiwa Steven Wasira. Katika mahojiano hayo,
Mheshimiwa Wasira alisema mimi ndiye niliyemkimbiza CCM.
Tangu mchakato wa Katiba Mpya kuanza nilikuwa napata taarifa kwamba
Mheshimiwa Wasira alikuwa amenifanya mtaji wake katika kutetea msimamo
wake. Wakati mmoja kuna kiongozi mwenzake aliniuliza kama nina ugomvi
binafsi na Mheshimiwa Wasira kwa sababu kila akipata nafasi kwenye vikao
vyao ananishambulia. Wakati wa mabaraza ya Katiba nilipata taarifa za
aina hiyo. Nilichofanya ni kuwaarifu viongozi wake wa CCM.
Niligombea mara mbili na Mheshimiwa Wasira. Baada ya Uchaguzi wa 1990
ambao nilishinda kwa kura nyingi sana, uchaguzi huo ilitenguliwa kwa
sababu nilifanya kampeni kwa kutumia gari la Waziri Mkuu.
Uchaguzi ulirudiwa mwaka 1992. Niliunda timu ya kampeni, Mheshimiwa Wasira akiwa kiongozi.
Aliniomba
atangulie jimboni kuandaa mazingira. Alipofika huko akaanza kampeni
dhidi yangu na kutangaza kwamba anagombea. Wakati huo kura za maoni
zilikuwa zinapigwa na wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya. Wajumbe
walikuwa kama 600. Nilipata kura 400 na Mheshimiwa Wasira alipata kura
chache akiwa mtu wa tatu au nne. Baada ya matokeo akatangaza anajitoa
kwenye mchakato na jina lake lisipelekwe NEC. Alikataliwa kwa sababu
kufuatana na kanuni, muda wa mtu kujitoa ulikuwa umepita.
Mwaka 1995,
kura za maoni zilikuwa zinapigwa kwenye kata. Tulianza na Kata ya Sarama
ambayo iko upande wa mashariki, siku ya tatu tulifika Nyamuswa ambacho
ndicho kijiji ninachotoka. Nyamuswa ilikuwa kituo cha tano kati ya vituo
12.
Baada ya
hapo tulielekea magharibi ya jimbo anakotoka Mheshimiwa Wasira. Baada ya
kura kupigwa katika Kata ya Guta, Mheshimiwa Wasira alijitoa kwa sababu
aliona hawezi kunishinda hata kama angepata kura zote za kata mbili
zilizobaki. Siyo kweli kwamba Nyamuswa ilikuwa ya mwisho kupiga kura na
siyo kweli wananchi wa kata nzima walipiga kura. Kumbukumbu zote
zinaweza kupatikana wilayani na makao makuu ya CCM.
Mheshimiwa
Wasira anasema kwamba nilikuwa Jaji na kesi iliyopelekwa mahakamani ni
kama kesi ya tumbili kupelekwa kwa nyani, kwa maana kwamba majaji
walinipendelea. Kumbukumbu za kesi hiyo zipo. Wakati huo sikuwa jaji.
Isitoshe huko nyuma uchaguzi nilioshinda 1992 ulitenguliwa. Kwa nini
wakati huo sikupendelewa? Kumbukumbu za kesi zinaeleza kwa nini
Mheshimiwa Wasira alifungiwa kugombea kwa kipindi.
Mheshimiwa
Wasira ni kiongozi wa Taifa kwa kipindi kirefu. Ni mbunge wangu na
namtambua hivyo. Tunaweza kuwa na mtazamo tofauti katika baadhi ya mambo
lakini hiyo si sababu ya kusema mambo yasiyo ya kweli kwa nia ya
kujijenga kisiasa.
Yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM. Yeye ni Waziri
mwandamizi. Yeye anafikiria kugombea urais. Ni vizuri basi akajifunza
kusema kweli (ambayo ni ahadi mojawapo ya WanaCCM). Akumbuke anayosema
yanaweza kumrudia mbele ya safari.
J.S. Warioba
24-09-2014
No comments: