Ads Top

MBUNGE MUKASA APONGEZWA KWA KUSAIDIA SHULE YA SEKONDARI

Na Antony Sollo Biharamulo.

MBUNGE wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Oscar Mukasa amepongezwa na Bodi ya Shule ya Sekondari ya Kagango iliyopo Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera baada ya kufanikisha kuitafutia ufadhili wa Shule hiyo ili kukamilisha ujenzi wa Bweni la Wavulana kidato cha Sita.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa niaba ya Bodi ya Shule hiyo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kagango Tumaini France alisema Bodi hiyo imefurahishwa na namna Mbunge huyo alivyoshiriki kikamilifu kuitafutia msaada Shule hiyo ili iweze kufanikisha ujenzi wa bweni la wanafunzi hao.

“Kwa niaba ya Bodi ya Shule hii napenda kumpongeza kwa dhati Mbunge
wetu kwa kuona umuhimu wa Elimu na kupigania kwa hali na mali upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa bweni hili,tumeuona mchango wake tunauthamini na tutaendelea kuuenzi”alisema Mwalimu France.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo ujenzi wa bweni hilo umekamilika kwa gharama ya Shilingi Mil 10,000,000 fedha ambazo zilitolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) baada ya Mbunge huyo kutafuta ufadhili kutoka katika Mfuko wa Mamlaka ya Elimu (TEA) na kuongeza kuwa tayari Bweni hilo limekamilika na limeshaanza kutumika.

Changamoto zingine zinazoikabili Shule hiyo ni viwanja vya michezo,vyumba vya madarasa,mabweni matatu,ukumbi wa mikutano kwa ajili ya watoto pamoja na Samani zake,(Usafiri )Basi la Shule kwa ajili ya Safari za Mafunzo .

France amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza na kuisaidia Shule hiyo
kutokana na changamoto nyingi zinazoikabili. 

“Tunawaomba wadau mbalimbali wa Elimu Wilayani pamoja na Mkoa mzima wa Kagera kujitokeza ili kuisaidia Shule hii kwani inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na upungufu wa matundu ya vyoo,Zahanati ya Shule,kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi”alisema France.

Hata hivyo kutokana na umri wa Shule hiyo unahitajika ukarabati mkubwa pamoja na kuongeza majengo na Maktaba pamoja na vitabu mbalimbali kwa ajili ya kuwaongezea uelewa wanafunzi katika Shule hiyo.

Jiwe la Msingi la Shule ya Kagango liliwekwa Feb15 1990 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya pili ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Ally Hassan Mwinyi ambaye kwa sasa ni Rais Mstaafu takribani miaka 29 iliyopita.

Katika kutafuta kujua Mbunge Mukasa atakabiliana vipi na changamoto zilizopo katika Shule hiyo Tanzania Daima lilimtafuta ili kuzungumza ambapo alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia ahadi kwa kuwa anahitaji kuja kukaa na uongozi ili kujaili kwa kina na kuona namna ya kutafuta wafadhili watakaotoa fedha kwa ajili ya kuboresha mapungufu hayo. 

“Siwezi kuzungumzia juu ya nini nitafanya kwa sasa hadi nitakapokaa na uongozi ili kujadili kwa kina na kuona namna ya kutafuta wafadhili wengine watakaotoa fedha kwa ajili ya kuboresha mapungufu hayo” alisema Mukassa.

MWISHO.





No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.