Ads Top

Katiba Mpya itoe ulinzi kwa haki za binadamu

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wapiwapakiza vijana waliowamatwa katika eneo la Darajani mjini Unguja Zanzibar baada ya kutokea vurugu kati ya Polisi na kikundi cha Uamsho wiki iliyopita

Maudhui ya haki hizi ni kulinda utu na heshima ya binadamu, hivyo hakuna mtu yeyote wala kikundi chenye mamlaka ya kuchukua haki hizi, hata iwe ni Serikali.

Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mapungufu yake inatambua haki hizi, japokuwa zina mapungufu. Pia inatoa fursa kwa mtu atakayepokonywa haki zake kuzidai mahakamani kupitia Ibara ya 30(5).

Wakati wa kuandika Katiba mpya, ni muda muafaka wa kutazama upya na kutafakari tena haki za binadamu .
Jambo la msingi zaidi ni kuhakikisha zinakuwamo na kutambuliwa, pia kuziboresha kwa kuondoa udhaifu uliopo na kuongeza haki za binadamu ambazo hazimo katika katiba ya sasa.

Katiba ya Uhuru (ya Tanganyika) ya mwaka 1961 haikuwa na haki za binadamu. Hata kwenye hii ya sasa ya mwaka 1977 haki hizo ziliingizwa kupitia mabadiliko ya tano mwaka 1984 kwa sheria No 15 ya mwaka 1984.

Kupitia ibara yake ya 64(5) Katiba inapata nguvu ya kisheria kama sheria mama ya nchi, na kutamka bayana kuwa sheria yoyote itayoenda kinyume na Katiba itakuwa batili.

Kwa kuwa haki za binadamu zipo ndani ya Katiba basi zinapata ulinzi huo wa kikatiba.

Pia Mahakama Kuu imepewa mamalaka ya kutengua sheria yeyote ile inayoenda kinyume na ibara za Katiba, hivyo haki za binadamu zinapata ulinzi huo.
  
Haki za binadamu kupitia Katiba ya sasa, zimeanzia Ibara 12 mpaka ya 24. Ibara 25 na 29 zinaonyesha wajibu.

Haki za binadamu ndani ya Katiba

Tunapotafakri kuhusu haki za binadamu kwa ujumla wake, kwanza tuone Katiba ya Tanzania imekidhi kwa kiasi gani haki hizo ukilinganisha haki hizo na haki za binadamu za kimataifa ambazo zimegawanyika katika makundi makuu matatu; haki za kisiasa na kiraia, haki za kiuchumi, kijami na kitamaduni na tatu haki za jumla.

Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 imeonyesha haki za kisiasa na kiraia kwa upana kuliko haki za kiuchumi, kijamii, na haki za ujumla.

Haki ya usawa wa binadamu ipo katika ibara 12, na  Ibara ya 13 inaonyesha usawa mbele ya sheria. Kupitia ibara hizo za Katiba inaonyesha kuwapo usawa wa  binadamu kwenye sheria za nchi, usawa wa kijinsia na kupinga ubaguzi.

Pia ibara ya 14 inaonyesha haki ya kuishi ya binadamu na haki hiyo ya kuishi ndio msingi wa haki zote za binadamu.

Haki zingine za binadamu zilizopo katika Katiba, ni haki ya uhuru wa mtu binafsi katika ibara ya 15, haki ya faragha, na ibara 16 usalama wa mtu na uhuru wa mtu kwenda atakako unapatikana katika ibara ya 17.

Katiba inaendelea kuelezea uhuru wa maoni katika ibara 18, uhuru wa mtu kuamini dini atakayo ibara 19, uhuru wa kushirikiana na wengine (ibara 20), uhuru wa kushiriki shughuli za umma (ibara 21), haki ya kufanya kazi ibara 22, haki ya kupata ujirai ya  23 na haki ya kumiliki mali ibara ya 24.

Changamoto za haki za binadamu

Pamoja na haki za msingi kuwapo kwenye Katiba bado hazijajitosheleza na hivyo kuhitajika Katiba Mpya ili kuziba mashimo yaliyopo.

Msingi wa kuangaliwa upya wa haki za binadamu unatokana na mapungufu kadhaa ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho katika Katiba ya sasa, ambayo ipo katika awamu ya kwanza ya hatua ya kukusanya maoni.

Ulinzi wa haki za binadamu

Masharti ya ibara ya 98(1)(a) ya Katiba,  inatoa fursa kwa Bunge kufanya mabadiliko ya ibara zilizomo katika Katiba, ikiwamo kubadilisha haki hizo za kibinadmu kwa namna yoyote linavyoona.

Ili kulinda haki hizo za binadamu basi, Katiba Mpya iweke ibara itakayoeleza kuwa  bunge halitaweza kubadlisha haki za binadamu mpaka kuwe na kura za maamuzi kwa wananchi wote, hilo litaongeza ulinzi  wa haki hizo za msingi za binadamu.

Pamoja na mapungufu yake, mfano mzuri wa ulinzi wa haki hizo unapatikana katika Ibara ya 80A (1), ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inaeleza Baraza la Wawakilishi halitaweza kufanya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.

Miongoni mwa mambo yaliyoainishwa katika Ibara 80A(2) ya Katiba hiyo ni haki za binadamu, kwamba hayawezi kubadilishwa na baraza hilo mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kura ya maoni.

Pia Katiba ya Kenya ya mwaka 2010 , katika ibara  255 pamoja na mambo mengine inaeleza kuwa mabadiliko yoyote yaliyoko katika ibara ya 255(2),  zikiwamo haki za binadamu, lazima yakubaliwe na wananchi kwa kura ya maoni.

Mifano hiyo inaonyesha si tu uhai wa haki za binadamu, bali pia ulinzi wake kutoka kwa wananchi wenyewe wanaotoa mamlaka kwa Serikali.

Katika mchjakato wa Katiba Mpya Tanzania inapaswa kujifunza kutoka Zanzibar na Kenya jinsi ya kutoa ulinzi wa haki za binadamu kwa masalahi ya umma.

Bunge la Tanzania linyang’anywe meno ya kuvunja  vifungu vya Katiba kuhusu haki za binadamu isipokuwa kama mabadiliko hayo yamekubaliwa na wanachi kwa kura ya maoni.

Mbali na upungufu huo, pia Katiba ya sasa haijaweka haki za kiuchumi na haki za jumla. Haki za elimu na efya ziko kwenye katiba katika Ibara 11 ya Katiba,ila ziko katika mtindo ambao mtu hawezi kwenda mahakamani kuzidai.

Katiba hii ya sasa inatoa fursa kwa Bunge kutunga sheria pingamizi dhidi ya haki za binadamu.

Tunapotaka kuandika Katiba Mpya ni wakati wa kutunga sheria itakayoliwekea Bunge mipaka lisitunge sheria yoyote ambayo inakinzana na  haki za binadamu zilizomo katika Katiba.

Kuwapo kwa ukizani wa Ibara na vifungu, mathalan Ibara ya 14 ya Katiba inayozungumzia haki ya kuishi, lakini kifungu cha Sheria ya Makosa ya Jinai sura ya 16 kifungu cha 197 inatoa adhabu ya kifo kwa mtuhumiwa atakayepatikana na kosa la kuua.

Kutokana ukizani huo wa sheria, adhabu hiyo ya kifo itaendelea kutolewa kwa kuwa masharti ya Katiba ya imetoa mwanya huo. Hata pale inapoonekana wazi kuwa ni uvunjaji wa haki ya kuishi.

Makundi maalumu yanayokandamizwa na mifumo kandamizi kama wanawake, walemavu, wazee na watoto na hata suala la kijinsia na uhusiano baina ya wanawake na wanaume katika nyanja za maisha, wamekosa ulinzi kwa maana kwamba Katiba ya sasa haiwatambui .

Tanzania kama nchi inayojitanabaisha kuwa inafuata mfumo wa  kidemokrasi na utawala bora na kuongozwa na utawala wa sheria, inatakiwa kuwa na Katiba Mpya itakayolinda haki za msingi za binadamu na kutoruhusu mtu  kuzichezea kwa njia yoyote, iwe Serikali yenyewe au hata mtu mmoja mmoja.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.