Ads Top

Wananchi wapata hofu Ebora kuingia nchini

WANANCHI waishio mpakani mwa Tanzania na Uganda wameingia na hofu baada ya kugundulika kuwa ugonjwa hatari wa Ebola imeingia nchini.

Watu wengi mkoani hapa kuanzia juzi walionekana kuingiwa na wasiwasi baada ya taarifa kuzagaa kuwa mgonjwa mmoja amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Karagwe ya Nyakahanga, mkoani hapa.
Wengi walisikika wakishauri serikali za Uganda na Tanzania kushirikiana kudhibiti ugonjwa huo usizidi kusambaa zaidi.
Inaelezwa kuwa mgonjwa huyo aliingia nchini akitokea nchi ya Uganda na kwamba hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya hiyo chini ya uangalizi maalumu wa madaktari.

Wananchi wazungumza
Wananchi hao walisema kuwa katika maeneo kama Mutukula ni vigumu sana kudhibiti mtu mwenye ugonjwa asiwaambukize wengine kutokana na mwingiliano mkubwa wa kibiashara uliopo.

Mkulima katika eneo hilo lililopo Wilaya ya Missenyi, Samihu Majidu alisema kuwa tangu walipotangaziwa kuchukua tahadhari, wanaishi kwa wasiwasi, wanaogopa kugusana na kushikana mikono.
Naye, Sauda Hassan, Mtanzania anayefanya biashara katika eneo la Mutukula alisema kuwa hata kama watakuwa makini kivipi, lakini bado vyombo vya usafiri ni tatizo kubwa linaloweza kueneza ugonjwa huo kwa kasi.
“Wenyewe mnaona hali ilivyo, watu wa Mbalala, Busia (Uganda) wako hapa, kama mtu ana ugonjwa utazuiwa vipi?” alihoji.

Aliongeza: “Wanakuja wamebanana kwenye magari wakati tunaambiwa msigusane, magari yanajaza sana abiria wengine wanasimama.”

Sauda alisema: “Tunafanya biashara hapa, mteja anakuja anakupa hela unashika bila kinga yoyote kama mteja ana ugonjwa ukashika hela ambayo ina majimaji utaugua, Nadhani tununue mipira ya kuvaa mikononi wakati wa kufanya biashara maana tukisema tuache biashara uchumi utashuka.”

Alisema hata kama Serikali itafunga mpaka wa nchi hizo bado tatizo litakuwepo kutokana kuwepo kwa njia nyingi za panya.

Sylvester Bundala aliziomba serikali za nchi za Tanzania na Uganda kushirikiana ili kuudhibiti.

“Tumetangaziwa katika vipaza sauti tusikae katika makundi ya watu wengi lakini hatuna jinsi hata kama mtu sio mfanyabiashara labda ni mkulima atatoka kwenda kununua mahitaji anaweza kuupata huko. Sisi tunaendelea na shughuli zetu mambo yote tumemwachia Mungu,” alisema Bundala.

Naye, mfanyabiashara wa eneo hilo, Jamada Kassim alisema kuwa ana biashara yake amepeleka Mutukula, lakini ameamua kujitenga na watu wengine na muda mwingi anasimama eneo la peke yake.

Daktari
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyakahanga, Dk Andrew Cesari alikiri kupokea mgonjwa mwenye dalili zinazowiana na za ugonjwa wa ebola.
Alisema mgonjwahuyo alipelekwa hospitalini hapo akitoka eneo la Kyerwa ambalo lipo mpakani na nchi hiyo ya Uganda.
Dk Cesari alisema kuwa mgonjwa huyo alikuwa ana homa kali, alivuja damu sehemu mbalimbali za mwili wake na kutaapika.
Daktari huyo alisema kwa mujibu wa maelezo ya ndugu zake, mgonjwa huyo alianza kupatiwa matibabu nyumbani kwao na alipoonekana kuzidiwa ikibidi wampeleke hospitalini hapo.

Alisema mgonjwa huyo alipokelewa katika chumba maalum na kupelekwa katika wodi ya magonjwa hatari ambapo ametengwa na anaendelea vizuri.
“Damu sasa imesimama kutoka, ameacha kutapika, lakini bado hatujajiridhisha kama ugonjwa alio nao ni Ebola maana yapo magonjwa mengine yanayoweza kumfanya awe na dalili hizo,” alisema.
Dalili zake
Alisema dalili za awali za mgonjwa wa Ebola ni homa, uchovu wa viungo, mafua, koo kuwasha, kutapika na kuharisha.

Aliongeza zipo pia dalili za baadaye ambazo ni  kutokwa damu, kutapika damu, ambazo zinaweza kujitokeza kuanzia siku ya tatu hadi ya nne, tangu mtu anapopata ugonjwa huo.
Alisema sio kwamba watu wote wanaougua ugonjwa huo wanakufa bali wapo wanaopona endapo watawahishwa hospitali na hatua za haraka zikachukuliwa kuzuia uvujaji wa damu.
“Mgonjwa anapofikisha siku tano hadi kumi hajafa uwezekano wa kupona unakuwepo… Lakini wengi wanakufa ndani ya siku tatu,” alisema Dk Cesari.
Kuhusu vifaa vya kujikinga, alisema kuwa tayari Serikali imeisambazia hospitali hiyo vifaa maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa aina hiyo.
Alisema serikali ilikuwa imechukua tahadhari kwa kuhakikisha wahudumu na madaktari wana taarifa za jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo baada ya watu zaidi ya 30 kuugua nchini Uganda na hadi juzi 19 walikuwa wamepoteza maisha.
Dk Cesari alisema wao kama watoa huduma za afya ambao wanapaswa kuchukua hatua za kuhakikisha wanaougua ugonjwa huo wanapatiwa huduma kuokoa maisha yao, nao wamewaka tahadhari wasiambukizwe.

Alisema Serikali tayari imewapatia vifaa maalumu vya kuvaa pale inapotokea wagonjwa wa namna hiyo.

Kwa sababu hiyo, alitoa ushauri kwa wananchi kufika hospitalini mapema wanapoona dalili za ugonjwa huo ili waweze kutibiwa na kuokoa maisha yao.

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa hofu ya ugonjwa huo, mwandishi wa habari hizi ameshuhudia mkusanyiko mkubwa watu katika eneo la Bunazi ambapo hufanyika gulio kila Jumamosi.

Gulio hilo hujumuisha watu kutoka maeneo mbalimbali wakiwepo wanaotoka nchini Uganda jambo ambalo baadhi ya watu wameeleza kuwa, ni hatari hivyo waliomba Serikali ichukue tahadhari.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.