Ads Top

ZOEZI LA SENSA LAZIDI KUPATA CHANGAMOTO



·       Wakazi wa kijiji cha Kituli Kata ya Tinde wameingiwa na hofu ya kutotekelezeka kwa zoezi la Sensa.
·       Waituhumu Serikali kutotekeleza mipango yake kwa Uwazi.
·       Watoa madai mazito dhidi ya Watendaji wa Serikali kuwahesabu mara kwa mara lakini hawaoni matokeo ya kuhesabiwa pindi misaada inapotolewa na Serikali.


 Zoezi la Sensa huenda likaingia Dosari kubwa katika jimbo la Solwa Mkoani Shinyanga baada ya wananchi kuishushia tuhuma nzito Serikali kuhusu zoezi la kuhesabu watu kunakofanywa mara kwa mara hasa pale wanapokuwa wakihesabiwa kwa lengo la kupewa misaada ikiwamo chakula cha njaa na matokeo yake chakula hicho kutolewa kipimo ambacho hakiendani na hesabu zoezi ambalo wamesema Sensa ni moja ya miradi inayopelekea kuwanufaisha viongozi wa Serikali badala ya malengo yaliyowekwa kwa ajili ya mipango mizuri iliyokusudiwa kwao.

Wakiongea na mwandishi wa makala hii wananchi wa kijiji cha Kituli kata ya Tinde wamesema huu siyo wakati unaofaa kwa viongozi wa Serikali kuendelea kuudanganya umma  bali ni wakati muafaka kwa kuwaweka wananchi wazi kuhusu mipango mbalimbali ya maendeleo yao na wamebainisha kuwa hali hii huenda ikawa na matatizo yatakayopelekea kutopiga hata kura katika chaguzi zijazo kwa vile wamekata tamaa ya kuchagua viongozi kwani pindi chaguzi zinapotokea hupatiwa viongozi wasio chaguo lao jambo linalowavunja mioyo ya kushiriki shughuli yoyote ya maendeleo inayopangwa na Serikali.

Wakiendelea kufunguka na kuonyesha kile walichoita maudhi yanayofanywa na viongozi,wananchi hao wanasema baadhi ya mipango inayotolewa na Serikali ni mipango ambayo haina tija kwa vile Serikali inaonyesha ubaguzi wa hali ya juu hasa katika mfumo wa Elimu kwa vile hata hizi shule za Sekondari za kata hazina manufaa kwa wananchi,wakitoa mifano wananchi hawa wamesema Serikali iache kuwadanganya wananchi kupitia mifumo ambayo ni ya kibaguzi kwa vile shule hizo huwezi kukuta Mtu hata mmoja wa viongozi akisoma pale bali shule hizo zimelenga kuwepo kwa watoto wa makabwela wasio na kipato cha aina yoyote na bado hata hivyo kabwela huyo anakandamizwa na mfumo huu kwa kunyang’anywa hata kile kidogo alicho nacho na kuwapelekea wakubwa waliobuni mpango wa Elimu hii isiyo na tija kwao.

Inasemekana shule hizo huwezi kukuta watoto wa Waheshimiwa Madiwani,Wabunge,Mawaziri na hata Mh Rais, jambo linaloendelea kuzaa matabaka katika mfumo wa Elimu katika Taifa letu.

Mambo haya yote ukiyajumlisha yanampa shida mwananchi kujitokeza katika masuala mbalimbali yanayotolewa na Serikali kwa ajili ya maendeleo hivyo wameomba Serikali iache kuwahadaa wananchi kuwa kiwango cha Elimu katika Taifa letu inaridhisha huku baadhi ya huduma zikiendelea kuwa na madaraja kwa kiwango cha kutisha, wakitolea mfano huduma za Afya wamesema mwananchi akiugua yeye matibabu yake ni hapa hapa na ni shida kupata hata hiyo huduma kwa kiwango kinachotia matumaini huku hata wale wanaotoa huduma hawapati maslahi yao inavyopaswa lakini utashangaa viongozi akiugua huangaliwa kwa mtazamo wa hali ya juu huku akiandaliwa matibabu ya nje ya nchi kwa gharama za walipa kodi jambo ambalo limezidi kuukoroga umma na kupelekea kutotaka kuhesabiwa katika zoezi la Sensa litakalofanyika mwezi huu.

Wameiomba Serikali ijirekebishe kwa kuweka mlinganyo katika mambo mbalimbali katika jamii vinginevyo chaguzi zijazo hawatakuwa tayari kupiga kura na kuchangia michango mbalimbali ya maendeleo ya jamii nchini.

Makala hii imeandikwa na Mwanaharakati na mtetezi wa Haki za Binadamu
Antony Johnson Sollo
Cell:
+255787 565 533 Email antonyjilala@yahoo.com

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.