Ads Top

MTUMISHI WA TAKUKURU KISHAPU ABURUZWA KORTINI KWA KOSA LA KUTISHIA KUUA

Na Antony Sollo Kishapu. 
Katika hali isiyo ya kawaida mtumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Wilayani kishapu bwana Kesy Sultan Mitiko umri wa miaka 28 amefunguliwa kesi ya kosa la jinai kesi namba CC145/2012 katika Mahakama ya Mwanzo wilayani Kishapu akituhumiwa kwa kosa la kutishia kumuua kwa maneno bwana Mlamuzi Pius Kuhanda ambaye ni Afisa wa TAKUKURU Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga. Imedaiwa mahakamani hapo kuwa,mnamo tarehe 22 mwezi wanne mwaka huu majira ya saa moja na nusu katika ofisi za Taasisi hiyo, mshitakiwa alitoa vitisho hivyo baada ya watumishi wa Taasisi hiyo akiwemo aliyekuwa akikaimu nafasi ya Kamanda wa Takukuru Wilayani humo Bi Lupakisyo Peter Mwakyolile kwenda katika ofisi hizo majira ya saa moja na nusu jioni kwa lengo la kurudisha Pikipiki ya Ofisi. Akisimulia mkasa huo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Kishapu Bwana Kuhanda amesema walipowasili katika ofisi hizo walishangazwa na jinsi hali waliyomkuta nayo mshitakiwa ambapo ilibidi wapande ukuta ili kufungua geti la uzio wa ofisi hizo kufuatia mshitakiwa kulala fofofo na pia kutojitambua kabisa,jambo lililowapa hofu kuwa huenda mshitakiwa alikuwa amekufa. Watumishi hao walipoingia ndani walimuita mshitakiwa bila mafanikio na baada ya muda mshitakiwa alishituka na akiwa hajui hata ilikuwa ni saa ngapi Bwana kesy alimuuliza mlalamikaji kuwa bwana Kuhanda una nguvu gani ya kuweza kuingia humu saa hizi saa nane usiku? Mlalamikaji alimjibu mshitakiwa kuwa hivi unatutambua kuwa sisi ni watumishi wenzio? Kwa nini hutaki kuuliza na kujua kwa nini tumeingia ndani? Na ni kwanini umechukua jukumu la kutaka kutuua kwa kutupiga risasi?kwani hutujui?baada ya mahojiano hayo mshitakiwa alishikilia msimamo wake akimwambia kwa kurudia rudia kwamba bwana Kuhanda ni lazima nikuue kwa kukupiga risasi. Kwa vile tayari mshitakiwa alikuwa amenyanyuka na kwamba alikuwa na silaha aina ya Short gun bwana Kuhanda na mwenzake waliamua kuondoka ofisini hapo kwa vile walikuwa wameona kuwa mshitakiwa alikuwa na nia ya kuwafyatulia risasi na kuwaua,hivyo waliondoka na Pikipiki hiyo hadi nyumbani kwa Kaimu Kamanda wa Takukuru Bi Lupakisyo Peter Mwakyolile. Baada ya muda mshitakiwa alimfuatilia mlalamikaji hadi nyumbani kwake lakini hakumkuta kwa vile alikuwa bado hajafika kwani alibaki kwa muda nyumbani kwa kaimu kamanda wa huyo,baada ya kumkosa mlalamikaji,mshitakiwa alirudi ofisini ambapo tarehe 23 mwezi wanne mshitakiwa alifika ofisini na kusisitiza kuwa alichokuwa akikisema jana ni kweli na ni lazima atimize ahadi yake ya kumuua kwa risasi mlalamikaji. mlalamikaji aliripoti tukio hili ofisini kwao na kuomba kuwa alifikishe Polisi kwa Hatua zaidi lakini alishauriwa na watumishi wenzake kuwa asitishe uamuzi wake ili suala hili lipatiwe suluhu ya Ofisi ya Taasisi hiyo bila mafanikio. Baada ya kumtolea maneno hayo bwana Kesy aliondoka ofisini na kwa kujua kuwa alikuwa ametenda kosa,na kwamba mlalamikaji angekuwa amelifikisha Polisi,mshitakiwa alitoroka na kwenda kusikojulikana na kukaa huko kwa muda wa siku 3 bila taarifa zozote kwa mwajiri wala kwa wafanyakazi wenzake,ambapo siku ya nne alionekana akiwa na cheti cha wagonjwa akieleza kuwa alikuwa anaumwa jambo ambalo si utaratibu wa Ofisi kwa watumishi wa Umma. Akizungumza kwa huzuni bwana Kuhanda amesikitishwa na Ofisi za Taasisi hiyo kushindwa kutatua tatizo hilo kwa kushindwa kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi huyo na kueleza kuwa anafika mahala anashindwa kufanya kazi kwa amani kwa vile mshitakiwa huyo anakaa na silaha muda mwingi hivyo kuhofia kuwa huenda atatimiza ahadi yake wakati wowote. Si hivyo tu, amesikitishwa pia na Viongozi wa Taasisi hiyo ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa kulifumbia macho suala hili kwani walimzuia kulipeleka katika vyombo vya usalama yaani Jeshi la Polisi akiamini lingepatiwa ufumbuzi lakini imekuwa ni kinyume baada ya baba wa mshitakiwa kusikika akitamba kuwa ataweka mawakili na kuhakikisha kuwa mwanae anabaki kazini na kwamba kuna taarifa kwamba kutochukuliwa kwa hatua dhidi ya mshitakiwa kunatokana na kwamba baba yake ni mmoja wa watu wanaofanya kazi kwa karibu na Mh Rais Jakaya Kikwete hivyo hakuna aliye na uwezo wa kulikemea wala kulishughulikia suala hili. Mshitakiwa amekana mashitaka na yuko nje kwa dhamana ya shilingi Laki tano ( 500,000/=)ambapo kesi hiyo itatajwa tena Novemba 7 mwaka huu. Mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Kishapu Bwana Kundya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa suala hilo limepelekwa mahakamani huko ili haki itendeke, ambapo kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga Evarist Mangala hakupatikana ili kulizungumzia suala hili kwani simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa. Mwisho.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.