Umeme wasitisha kikao Baraza la Wawakilishi

Baraza la Wawakilishi
KIKAO cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani Unguja, kimelazimika kusitishwa kwa muda kutokana na hitilafu ya umeme iliyotokea katika ukumbi wa baraza hilo la wawakilishijana asubuhi.
Akitoa tangazo kwa wajumbe wa baraza hilo, Spika
Pandu Ameir Kificho aliwaambia wajumbe kwamba kutokana na hitilafu hiyo
kikao hicho anakiahirisha hadi jioni ili kutoa fursa kwa mafundi wa
umeme kuja kufanya matengenezo katika ukumbi huo.
Spika Kificho alisema licha ya kuwashwa jenereta
na kuendelea na shughuli za baraza hilo, lakini kutokana na ukubwa na
mahitaji makubwa ya umeme katika ukumbi huo, majenereta hayo hayana
uwezo wa kumaliza shughuli nzima ya vikao vya baraza hilo na hivyo
wanalazimika kuwapisha mafundi kuendelea na kazi ya matengenezo.
“Waheshimiwa wajumbe kutokana na hitilafu ya umeme
katika ukumbi wetu huu, naomba kuahirisha kikao hiki hadi hapo jioni,
ili tutoe nafasi kwa mafundi waliofika hapa kuja kututengenezea umeme
kwa sababu jenereta lililowashwa haliwezi kutumalizia shughuli yetu hii
muhimu” alisema Spika.
Hata hivyo wajumbe wa baraza la wawakilishi
walionekana kutoka wakiwa na furaha baada ya kusikia kikao hicho
kimeahirishwa na waliendelea jioni baada ya matengenezo hayo kufanywa na
wataalamu na mafundi kutoka Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco).
Ukumbi wa baraza la wawakilishi umejengwa kwa
ufadhili wa Sheikh Ali Yussuf wa Saudi Arabia na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, lakini ukumbi huo umekuwa na hitilafu za mara kwa mara katika
mitambo yake ya umeme, vipaza sauti na hata baadhi ya sehemu ya jengo
hilo limekuwa likivuja.
Ofisa mmoja wa baraza hilo aliliambia gazeti hili
kwamba ujenzi wa jengo hilo haukuwa mzuri katika ramani yake kutokana na
kuwa mafundi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa) wameshindwa kuona njia
na paipu za kupitishia maji machafu na hivyo kuvuja kwa maji
kumeshindikana licha ya juhudi kadhaa kufanywa na wataalamu wa Zawa
kujaribu kutaka kufanya marekebisho njia hizo za maji ndani ya jengo
hilo.
“Jengo hili tokea limejengwa kuna matatizo mengi
si unakumbuka wawakilishi wakilalamikia vipaza sauti havisikiki na sasa
umeme una matatizo, pia kuna tatizo la maji hapa wamekuja mafundi na
wataalamu wengi sana, lakini wameshindwa kuona paipu hawajui zimefukiwa
au zimezamishwa wapi kwa hivyo maji yanamwagika na hayana pa kutokea na
wale waliojenga wala hawapo sasa sijui tena serikali itafanyaje,”
alisema.
No comments: