Papa Benedict aahidi utii kwa ajaye
Papa Mstaafu Benedict wa kumi na sita
HUKU mchakato wa kumpata papa mpya ambaye ataongoza Kanisa Katoliki ukianza Jumatatu Machi 4, mwaka huu, Papa Mstaafu Benedict XVI ameaga akiahidi utii kwa mrithi wake.
HUKU mchakato wa kumpata papa mpya ambaye ataongoza Kanisa Katoliki ukianza Jumatatu Machi 4, mwaka huu, Papa Mstaafu Benedict XVI ameaga akiahidi utii kwa mrithi wake.
Katika salamu zake kwa makardinali jana, muda
mfupi kabla ya kung’atuka rasmi, Papa Benedict alieleza kuwa atakuwa
karibu na mrithi wake bila migongano.
Kauli hiyo imetolewa wakati kukiwa na hofu
miongoni mwa walei, watawa kwamba huenda viongozi hao wakaingia katika
mzozo wa madaraka.
Hata hivyo, wakati akitoa ahadi hiyo, mchakato huo
unaanza huku ajenda muhimu zikiwa ni jinsi ya kulisafisha kanisa hilo
ambalo limekumbwa na kashfa kadhaa.
Kashfa hizo ndizo zinazotazamiwa kutawala kikao cha makardinali kinachoanza Jumatatu.
Ingawa ni makardinali 115 kati ya 117 wenye sifa
ya kupiga kura ya kumpata papa mpya,tayari makardinali wengi akiwamo
Kardinali Polycarp Pengo kutoka Tanzania wapo Vatican kushuhudia kazi
hiyo ngumu.
Ni kazi ambayo inaweza kuchukua hadi wiki tatu
ikiongozwa zaidi na sala, mafungo huku wapigakura ambao ni makardinali
wenye umri chini ya miaka 80 wakikabiliwa na changamoto lukuki.
Kwanza, ni azma ya wengi ya kulisafisha kanisa
hilo kubwa duniani linalokabiliwa na tuhuma nyingi zikiwamo za baadhi ya
viongozi wake kuwadhalilisha watoto kijinsia, kuvuja kwa nyaraka za
siri kutoka ofisi ya Papa Benedict XVI ambaye amestaafu.
Nyingine ni ufisadi katika benki inayomilikiwa na
kanisa hilo iliyo sababisha uongozi wake kuondolewa mwaka jana na
maofisa wake kushtakiwa.
Awali, Papa Benedict Jumatano aliwaaga maelfu ya
waumini, watawa ambaye jana aliondolewa Vatican usiku wa saa 2.00 (saa
4:00 za usiku kwa Tanzania) kwa helikopta maalumu ili kuanza maisha
mapya katika makazi ya papa, majira ya kiangazi, Castel Gandolfo, kusini
mwa Rome.
Ulinzi wake kwa sasa utakuwa chini ya polisi wa
kawaida badala ya walinzi wake raia wa Uswisi ambao kibarua chao
kilimalizika rasmi jana usiku.
Lakini, nyuma yake kiongozi huyo ameacha waumini
bilioni 1.2 huku baadhi ya maeneo mengine kama Ulaya na Marekani,
watumishi hasa mapadri na watawa wakiwa wamepungua.
Sababu hiyo inalifanya Bara la Afrika kuonekana kuwa eneo
linalokua kiimani lenye waumini 177 milioni na kusababisha bara hilo
kupigiwa upatu kwamba linaweza kutoa mrithi wa Papa Benedict.
Makardinali, Peter Turkson kutoka Ghana na Francis
Arinze wa Nigeria,mwenye umri zaidi ya miaka 80, wanatajwa kuwa
miongoni mwa wanaofaa kwa kazi hiyo.
Katika hotuba yake Jumatano, Papa Benedict
alieleza kuwa maisha yake Vatican yalikuwa yenye furaha, huzuni baada
ya kupitia vipindi vigumu na wakati mwingine rahisi.
"Kuna kipindi ambako bahari ilichafuka, mawimbi na pepo zilivuma dhidi yetu ... wakati mwingine Mungu alielekea kuwa amelala."
Kuhusu sifa ambayo makardinali hao wangependa awe
nayo mrithi wa Papa Benedict XVI, wapo wanaodhani kuwa hakutakuwa na
mabadiliko makubwa kwani viongozi wa kanisa hilo ni watu wasiopenda
mabadiliko.
Kwa maana hiyo, makardinali wachache watapenda kuona mabadiliko ndani ya kanisa hilo.
Kwa mtazamo wa wengi, mfumo utawazuia wengi
kukimbilia mabadiliko na kitu ambacho watakitafuta makardinali ni kupata
mtandao mkuu miongoni mwao.
Pia, wapo wengine ambao wanafikiri kuwa
makardinali wangependa kumpata mtu ambaye ni mzungumzaji mzuri. Lakini,
hawalazimiki kumteua mtu anayezungumza lugha nane kama za Papa Benedict
na mtangulizi wake, Mwenyeheri Yohani Paul II, ila kiongozi anayefaa
kuingia madarakani na kutambulika kuwapo kwake duniani.
Sifa nyingine ambayo inatazamiwa kuangaliwa ni ya
kiongozi ambaye atakuwa mtu wa watu, tofauti na Papa Benedict XVI
ambaye alishindwa kufuata nyayo za Mwenyeheri Yohane Paul II.Kwa
wengine ndani ya kanisa, Papa Benedict XVI anaonekana kuwa alishindwa
kuwafikia wengi, yakiwamo makundi ya watu ambao walikuwa tayari
kumsikiliza.
Wakosoaji wa mfumo wa kumpata papa mpya wanaeleza
kuwa suala la makardinali kutozungumza wakati wote wa mchakato unazuia
mijadala kuhusu hali ya baadaye na ustawi wa kanisa, hasa kwa kuzingatia
ukweli kwamba kanisa hilo linaonekana kuwa limefungwa.
Kuondoka kwa papa madarakani baada ya miaka 600
iliyopita kunaelekea kuwa kumeacha ombwe, mtazamo ambao unaungwa mkono
na mwanahabari mwandamizi wa Vatican, John Thavis.
Thavis anaeleza kuwa watu wengi waliopo Vatican
hawana mpangilio wa kazi zao, wamechanganyikiwa kutokana na kung'atuka
ghafla kwa papa.
Kwa
mtazamo wa wengi, uamuzi wa papa kung'atuka ulikuwa wa dharura mno,
kiasi kwamba hakuwahusisha wengine, jambo ambalo linalifanya ofisi yake
iliyoko Vatican pamoja na wasaidizi wake kuwa na wakati mgumu kusaka
majibu.
"Kila mmoja anataka kuandika historia, lakini hakuna anayejua lipi litatokea baadaye.
"Kuna tatizo la kutoa maamuzi Vatican, utaratibu umebakia zaidi wa kimila. Ni uamuzi ambao unategemea zaidi watu binafsi, bila kuangalia mtazamo wa jamii," anaeleza Thavis.
"Kuna tatizo la kutoa maamuzi Vatican, utaratibu umebakia zaidi wa kimila. Ni uamuzi ambao unategemea zaidi watu binafsi, bila kuangalia mtazamo wa jamii," anaeleza Thavis.
Mwandishi huyo ambaye ameishi na kufanya kazi
katika Shirika la Habari la Catholic News Services kwa miaka 30 anaamini
kuwa kumekuwa na wakati ambao papa alikatishwa tamaa na alitambua hilo.
Pia, alifikia mahali pa kuona amesalitiwa,
anaeleza mwandishi huyo katika kitabu chake, Vatican Diaries na kuongeza
kuwa hilo lilimuumiza binafsi papa, ambaye hata hivyo aliumia kila
alipokosolewa.
Jambo lingine ambalo limeachwa na papa huyo
aliyestaafu ni kukosekana kwa uwazi katika baadhi ya mambo yakiwamo ya
utoaji zabuni, mambo ambayo yanaweza kuitwa kuwa ni rushwa ndogo
zilizotendeka Vatican.
No comments: