Ads Top

Tume yaongeza siku za kuchagua mabaraza

 
 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeongeza siku mbili za kupiga kura ya kuchagua wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, zoezi ambalo awali lilipangwa mara ya kwanza kufanyika kati ya Machi 30 mpaka Aprili 3, mwaka huu.
Mabadiliko hayo ya ratiba yamekuja baada ya baadhi ya makanisa kutumia ibada ya juzi Jumapili pamoja na mambo mengine kuonya juu ya ratiba hiyo ya Tume kuwanyima haki wafuasi wa dini ya Kikristo kutokana na siku zilizokuwa zimepangwa kuangukia kwenye Sikukuu ya Pasaka.

Katibu wa Tume hiyo, Assaa Ahmad Rashid aliieleza Mwananchi jana kuwa muda umesogezwa mpaka Aprili 5 mwaka huu badala ya Aprili 3 kama ilivyokuwa imetangazwa awali.

“Kwa mujibu wa mabadiliko mapya, vikao hivyo sasa vitafanyika kati ya Machi 30 hadi Aprili 5, kwa msingi huu kila kijiji au mtaa kitachagua tarehe ambayo wananchi watapiga kura kuwachagua wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya,” alisema.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine Niwemugizi, alisema tarehe hizo zinajumuisha siku za Sikukuu ya Pasaka ambayo Wakristo wote duniani huadhimisha kufufuka kwa Yesu Kristo na kuonya baadhi ya watu wanaweza kupanga shughuli hiyo ya uchaguzi kuangukia kwenye sikukuu hiyo.

Niwemugizi ambaye ni Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara, alisema kuwa endapo tarehe hiyo ya kuchagua wajumbe hao itaangukia Machi 31 ama Aprili Mosi, wao watahesabu kuwa huo ni uchokozi na mbinu za kuwanyima haki ya kushiriki kuchagua watu watakaoenda kupitia rasimu hiyo kwa ngazi ya wilaya.

“Tunaangalia Machi 31 kuwa ni Jumapili ya Pasaka na Aprili Mosi ni Jumatatu ya Pasaka, kwa nini iwe kwenye tarehe hizo,” alihoji na kuongeza.

Alisema kuwa, endapo siku za kupiga kura hiyo zitaangukia kwenye Pasaka, wao wataona kuwa ni mpango wa shetani na hivyo wataamua kuitoa sadaka sikukuu hiyo na kwenda kupiga kura kisha kufanya misa jioni.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo, Assaa, alisema kuwa ingawa muda waliotoa ndani yake unajumuisha Sikukuu ya Pasaka, hawatarajii kuona watu watapanga siku za mikutano hiyo ziangukie kwenye siku hizo.

Alisema kuwa vikao hivyo vitakuwa vikifanyika kwa siku moja na wametoa muda mrefu bila kutaja siku rasmi ili visiweze kukwazwa na shughuli za watu.
Alisema kutokana na uzoefu walioupata wakati wa ukusanyaji wa maoni, baadhi ya maeneo huwa na magulio hivyo kupanga siku moja ya kufanya shughuli hiyo kutawakosesha haki baadhi ya watu.

Taarifa ya Tume hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilifafanua kuwa kutokana na mabadiliko hayo ya tarehe, muda wa vikao maalumu vya Kamati za Maendeleo za Kata vya kuwachagua wajumbe wanne waliochaguliwa na vijiji na mitaa navyo vimesogezwa mbele na sasa vitafanyika kati ya Aprili 7 mpaka 10 mwaka huu.

Awali, vikao hivi vilipangwa kufanyika kati ya Aprili 5 mpaka Aprili 9 mwaka huu.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Mhashamu Baba Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa alitoa maagizo kwa maparoko na wenyeviti wa parokia za jijini Dar es Salaam kuhamasisha waumini wao kushiriki katika mchakato huo.

kwa habari zaidi bofya hapa....>>>>> 

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.