Ads Top

Viongozi waapa mashambulizi mabaya ya bomu la kwenye gari hayatazuia maendeleo Somalia

Viongozi wa Somalia wameapa kusimama madhubuti dhidi ya al-Shabaab baada ya gari lililokuwa likiendeshwa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga karibu na Jengo la Maonyesho la Somalia mjini Mogadishu kuua watu 10 na kuwajeruhi kiasi cha wengine 14 siku ya Jumatatu (tarehe 18 Machi).  
Mwanamke wa Kisomali akilia baada ya mashambulizi ya gari lenye mabomu ya kujitoa muhanga katikati ya Mogadishu siku ya Jumatatu (tarehe 18 Machi). [Mohamed Abdiwahab/AFP]
Magari yakiungua baada ya gari lenye mabomu la al-Shabaab kulipuka. [Ali Adam/Sabahi] 
Magari yakiungua baada ya gari lenye mabomu la al-Shabaab kulipuka. [Ali Adam/Sabahi]
Raia wakitafuta manusura kwenye vifusi. Raia waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali za Madina na Daaru Shifa. [Ali Adam/Sabahi] 
Raia wakitafuta manusura kwenye vifusi. Raia waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali za Madina na Daaru Shifa. [Ali Adam/Sabahi]
Polisi wakiubeba mwili wa mtu aliyeuawa katika mashambulizi mabaya kabisa ya bomu la kwenye gari siku ya Jumatatu. [Mohamed Abdiwahab/AFP] 
Polisi wakiubeba mwili wa mtu aliyeuawa katika mashambulizi mabaya kabisa ya bomu la kwenye gari siku ya Jumatatu. [Mohamed Abdiwahab/AFP]

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia aliyaita mashambulizi hayo ya "kinyama" akitoa salamu zake za rambirambi kwa wahanga na familia zao kwa niaba ya serikali ya shirikisho.
"Tunaweza tu kukisia kwamba katika kiwango hiki mashambulizi haya ya kijoga ni kazi ya al-Shabaab," alisema Mohamud katika taarifa iliyotolewa muda mfupi baada ya mlipuko huo. "Wamedhoofishwa sana na sasa wamegeukia ugaidi na mauaji dhidi ya raia wa Somalia wasio na hatia. Lazima tuendelee kuungana dhidi yao."
"Vikosi vya al-Shabaab/al-Qaeda havina nafasi kwenye ulimwengu huu na hatutawaruhusu kuwa na nafasi ndani ya Somalia," alisema. "Tutawashinda tu."
Moshi mweusi ulilifunika anga la eneo lilikofanyika mashambulizi hayo huku mabaki ya gari lililokuwa na mabomu na basi dogo jeupe likiungua. Baada ya moshi kusafika na polisi wa Somalia kuliweka eneo hilo chini ya ulinzi, ndipo vikosi vya usalama na wapita njia walipoanza kuiondoa miili ya waliouawa na majeruhi.
Wengi kati ya wahanga hao walikuwa na abiria wa basi hilo dogo lililokuwa likipita karibu na eneo ulipotokea mlipuko. Waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali za Madina na Daaru Shifa.
"Tulipokea watu wanane waliojeruhiwa na wanne waliofariki," alisema Dokta Mohamed Yusuf, mkurugenzi wa Hospitali ya Madina. "Mmoja wa majeruhi alikufa wakati wa upasuaji. Kwa sasa kuna watu majeruhi saba waliolazwa hapa hospitalini, baadhi yao wakiwa na hali mbaya sana."
Majeruhi watano na waliofariki watatu walipelekwa kwenye hospitali binafsi ya Daaru Shifa, Yasmin Omar, mfanyakazi wa idara ya dharura, aliiambia Sabahi.
Mohamed Mohamud, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 28 anayeishi Mogadishu, alikuwa eneo la karibu wakati mlipuko ulipotokea.
"Nimehuzunishwa sana na mlipuko huu uliotokea Mogadishu leo," aliiambia Sabahi. "Kwa siku za karibuni tulikuwa tumeanza kuona matumaini mapya ya maendeleo na mabadiliko. Ningelipenda kuwaambia wafanyaji wa tendo hilo, waache kutufanyia haya."

Al-Shabaab wadai kuhusika

Al-Shabaab walidai kuhusika na shambulio la kujitoa muhanga, wakisema lilikuwa likilenga msafara wa magari na pikipiki wa kamanda wa Shirika la Usalama la Taifa Kanali Khalif Ahmed Ereg wa Benadir.
"Mujahidina hao walihusika na shambulio dhidi ya kafiri Khalif Ereg," msemaji wa al-Shabaab Shekhe Ali Mohamud Rage aliiambia AFP. "Mashambulio dhidi ya watu kama hao yataendelea hadi waondolewe kabisa katika ardhi yote takatifu ya Somalia."
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya mlipuko, Ereg alisema shambulio hilo lilishindwa katika jaribio lake na lilidhuru raia wasio na hatia katika mchakato huo. Alisema alipata majeruhi kidogo wakati mlipuko huo ulipovunja madirisha ya gari ambalo alikuwa akilisafiria.
"Kuna kitendo cha uhalifu kilichofanywa na vikundi vinavyopinga amani katika jaribio la kudhoofisha amani na maendeleo ambayo Somalia imeifurahia hivi karibuni," Ereg alisema. "Hawatapewa nafasi ya kuiharibu."

Waandishi wa habari wauawa, kujeruhiwa

Mwandishi mmoja wa habari aliuawa na wengine watatu walijeruhiwa katika shambulio la Jumatatu.
Mwandishi wa habari wa Redio Mustaqbal Mohamed Ali Nuhurkey, mwenye umri wa miaka 28, alikuwa mmojawapo kati ya watu kadhaa waliokuwa wamekaa katika mgahawa karibu na Ukumbi wa Maonyesho wa Taiifa wakati wa mlipuko, kwa mujibu wa Redio RBC ya Somalia. Alifariki akiwa hospitalini kutokana na majeraha.
Mpiga picha wa kujitegemea Ilyaas Sheikh Ahmed, mwandishi wa habari wa Redio Mustaqbal Abdirashid Nur Ibrahim na Munasar Nur, ambaye alikuwa wakifanya kazi kwa Redio Goobjoog, kituo huru cha redio huko Mogadishu, walijeruhiwa na kulazwa hospitali ya Madina.
"Kwa niaba ya waandishi wa habari wa Somalia, ninatoa pole na salamu za rambirambi kwa familia hizo, marafiki na wafanyakazi wenzake wa marehemu Mohamed Ali Nuhurkey," alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Kitaifa wa Waandishi wa Habari wa Somalia Mohamed Ibrahim. "Waandishi wa habari wa Somalia wanapaswa kuwa na tahadhari na kuchukua hatua za usalama kuhakikisha usalama wao binafsi na kubaki watulivu kufuatia shambulio hili la kutisha."
Nuhurkey alikuwa mwandishi wa habari wa pili kuuawa nchini Somalia mwaka huu, kwa mujibu wa Horseed Media ya Somalia. Tarehe18 Januari, watu wenye silaha walimuua mtangazaji wa redio Abdihared Osman Adan wa mtandao wa Shabelle Media Network katika wilaya ya Wadajir.

Shambulio halitasimamisha maendeleo

Ufufuaji wa Somalia bado utakuwa mbali kuendelea kwa nchi hii kuondolewa kwenye shambulio hili la "kipuuzi", Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon alisema.
"Ukweli ni kwamba maisha yatakuwa na amani zaidi na Mogadishu ina usalama zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 20 iliyopita," alisema. "Majaribio haya yasiyo na mwelekeo wa kutuondoa tulipo hayatakuwa na athari. Tumeishafanya maendeleo mengi sana kuondoa siku mbaya zilizopita. Amani, utulivu na biashara ni kanuni ya siku hizi."
"Huo ulikuwa ni uvamizi wa kikatili kwa raia wa Somalia wasio na hatia," alisema Mwakilishi Maalumu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia Balozi Mahamat Saleh Annadif.
Alisema Mogadishu imekuwa katika kipindi kirefu cha amani katika miongo miwili, ambayo imewapa Wasomali fursa ya kuanza kujenga upya maisha yao.
"[Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia] imeahidi kuisaidia Somalia kulinda usalama wa raia wake na tutaendelea kusaidia jitihada za kujenga uwezo wa Vikosi vya Ulinzi vya Taifa na kuviondoa vitisho vya al-Shabaab nchini," alisema.
Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Augustine Mahiga alisema shambulizi lilikuwa "halikubaliki kabisa".
"Somalia imeendelea vizuri katika njia ya maendeleo na kuimarika na uvamizi huo wa uoga wa kigaidi utachochea tu azma ya wananchi wa Somalia ya kustahimili," alisema. 

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.