Mabilioni ya bajeti yalivuruga Bunge Dodoma
Kitendo cha Bunge kuidhinisha matumizi ya fedha kiasi cha
Sh118bilioni katika wizara tatu licha ya kupingwa na kulalamikiwa na
wabunge wengi kwamba zingepelekwa katika maendeleo, kimepingwa na wasomi
na wanaharakati nchini ambao wamewataka wawakilishi hao wa wananchi
kuikataa bajeti ya Serikali.
Fedha hizo ni zile zilizolalamikiwa na wabunge
wakati wa uwasilishwaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na ile ya Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma.
Kutokana na kuwapo mvutano mkali bungeni, kwa
nyakati tofauti Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi,
walilazimika kutoa maelezo ya kina kuwashawishi wabunge wakubali ili
fedha hizo ziidhinishwe katika bajeti husika kwa ajili ya matumizi ya
mwaka mpya wa fedha unaoanza Juni mwaka huu.
Fedha hizo ni Sh74 bilioni zilizotengwa kwa ajili
ya mfuko wa pembejeo, Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa
kitaifa, Sh88 bilioni za Ruzuku ya Mfuko wa Pembejeo na Sh29 bilioni kwa
ajili ya kufuatilia utekelezwaji wa miradi ya Serikali.
Baadhi ya wabunge walilalamikia fedha hizo wakisema kuwa ni ulaji kwa wakubwa.
Wakizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Chuo Kikuu
Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete alisema kwa kuwa Bajeti ya Wizara ya
Fedha itapitishwa mwishoni, wabunge wanatakiwa kuikataa hadi mambo
muhimu katika bajeti zilizotangulia kusomwa, yatakapofanyiwa kazi.
“Binafsi naona hiyo ndiyo njia nzuri iliyobaki,
wabunge wanatakiwa kuamua mambo kwa masilahi ya taifa na siyo kwa
manufaa na maslahi yao binafsi,” alisema Profesa Mbwete.
Aliwataka wabunge kutumia fursa hiyo kumbana
Waziri wa Fedha ili kuhakikisha kuwa fedha zaidi zinaongezwa, au
kupunguzwa katika maeneo mengine, kwa ajili ya kupelekwa katika
maendeleo.
Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), alisema kuwa fedha zaidi zinatakiwa kuongezwa katika bajeti ya
maendeleo, badala ya matumizi ya kawaida.
“Maendeleo yatapatikana kwa haraka kama tutawekeza
zaidi ya asilimia 20 ya bajeti yetu kwenye matumizi ya maendeleo. Hii
ni tofauti na sasa, ambapo asilimia 90 ya fedha zinazotengwa zinakwenda
katika matumizi ya kawaida,” alisema.
Alisema umefikia wakati wa Serikali kuachana na matumizi yasiyokuwa na ulazima, kama ununuzi wa samani za ofisini.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper
Ngowi aliwataka wabunge kuwa makini na kukubali hoja kwa manufaa ya
taifa, siyo kishabiki.
“Wabunge wanatakiwa kutenga muda zaidi kwa ajili ya kupitia
bajeti za wizara husika kiundani zaidi, ili kujua mambo ya msingi,
baadaye kuyajengea hoja,” alisema na kuongeza:
“Hata kama watakubaliana hoja ipite, basi ipite
ikiwa tayari kila kitu kimekwenda sawa. Lakini kama wataamua tu
kupitisha mambo kwa sababu wanazozijua wao ni wazi kuwa watakuwa
hawawatendei haki Watanzania.”
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata),
Deus Kibamba alisema kwamba siyo kila fedha inayotengwa na Serikali kwa
ajili ya matumizi fulani, haistahili kuhojiwa matumizi na malengo yake.
“Zipo fedha ambazo zinapelekwa kienyeji tu katika
sekta mbalimbali, lakini haziendi kuleta jipya, kila mwaka kumekuwa na
malalamiko ya kutotekelezwa kwa miradi mbalimbali, wabunge wanatakiwa
kuwa macho na kutokubali kitu hiki kabisa,” alisema Kibamba.
Ilivyokuwa
Mvutano mkali uliozuka bungeni kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu kutenga Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi ulimlazimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi kutoa ufafanuzi.
Mvutano mkali uliozuka bungeni kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu kutenga Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi ulimlazimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi kutoa ufafanuzi.
Katika ufafanuzi wake alisema kwamba fedha hizo
zimetengwa kwa ajili ya kununua eneo la hekta 129 zilizopo eneo la
Iyumba mkoani Dodoma, ili liwe likitumika kwa mazishi ya viongozi hao
kwa mujibu wa Sheria ya Maziko ya mwaka 2006.
Ufafanuzi huo ulitolewa baada ya wabunge
kulalamikia kutenga Sh1 bilioni kwa mazishi ya viongozi wa Serikali,
wakati wananchi wanaishi hali duni ya umaskini wakisema ni ulaji kwa
baadhi ya watu.
Hata hivyo, tangu kupitishwa Sheria ya Maziko ya
Viongozi mwaka 2006, hakuna kiongozi ambaye amezikwa Dodoma huku wengi
wakizikwa mikoa wanayotoka.
Mvutano mwingine uliibuka wakati wa Bajeti ya Kilimo ambayo ilipita baada ya Waziri Mkuu kusimama na kutoa rai kwa wabunge.
Katika bajeti hiyo, Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika iliomba jumla ya Sh328 bilioni kwa maendeleo ya kawaida huku
ikiomba nyongeza ya Sh88 bilioni endapo ruzuku ya pembejeo itatolewa kwa
utaratibu wa vocha na Sh130 bilioni endapo ruzuku ya pembejeo itatolewa
kwa utaratibu wa mikopo na Sh5 bilioni kwa ushirika.
Masuala yaliyoleta sokomoko katika bajeti hiyo kubwa ni stakabadhi ghalani na mfumo wa ruzuku ya pembejeo kutumia vocha.
No comments: