Ads Top

Breaking News: Mkongwe wa Muziki hapa nchini,Bi.Kidude amefariki dunia mjini Zanzibar


MWIMBAJI mkongwe wa taarab, Fatma Baraka maarufu kama Bi Kidude amefariki dunia muda huu.
Mjukuu wa marehemu, Fatuma Kidude amekaririwa na Saluti5 kutoka Zanzibar, akisema bibi yake amefariki nyumbani kwa mtoto wa kaka yake maeneo ya Bububu.
Fatma ambaye naye pia ni mwimbaji, akiimbia kundi la Gusa Gusa la Dar es Salaam ameongeza kuwa bado taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika lakini mwili wa marehemu unahamishwa muda huu kupelekwa nyumbani kwake Raha Leo.
Mara kadhaa kumewahi kutokea uzushi wa Bi Kidude kufariki, lakini Saluti5 imehakikishia kuwa habari hizi ni sahihi kwa aslimia mia moja.
Bi Kidude alianza kusumbuliwa na mapema mwaka jana, lakini baadaye akapata ahueni na kufanya mahojiano hadi na vyombo vya habari, lakini ghafla mambo yakabadilika tena na kulazwa katika hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam.
Baada ya matibabu akaambiwa asiimbe tena na tangu Machi mwaka jana hajapanda jukwani.
BIN ZUBEIRY inamtambua Bi Kidude kama gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. 
Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi Kidude aliwahi kusema enzi za uhai wake kwamba hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa alichokuwa anajua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Enzi za uhai wake, Bi Kidude alikuwa anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti Binti Saad. 
Alisema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi Kidude alikuwa hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia alikuwa ni mfanyabiashara ya 'wanja' na 'hina' ambavyo alikuwa anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni alikuwa mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na alianzisha chuo chake mwenyewe na alisema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude alikuwa ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu. 
Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Enzi za uhai wake, Bi Kidude alitembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza na kujipatia tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Quraan

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.