Kauli aliyotoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni hivi karibuni haiwezi kupita bila kujadiliwa
Kwa upande wangu, naamini kwamba haikuwa kauli ya bahati mbaya
bali ni ya makusudi na ndiyo maana hatuoni Pinda akiomba radhi au hata
Rais akimkosoa au hata chama tawala CCM kiikemea.
Pinda huyu huyu aliyeingia katika nafasi hiyo
akiwa mnyenyekevu na kujiita mtoto wa mkulima, sasa anaonyesha sura yake
ya pili ya ukatili.
Siyo mara ya kwanza kutoa kauli tata kama hizo,
kwani mwaka jana wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaraktari,
Dk Steven Ulimboka akitekwa, Pinda alionyesha kukata tamaa pale
aliposema, “liwalo na liwe”.
Huo bila shaka ndiyo msimamo wa chama na Serikali,
kwamba mtu akitaka kukunyang’anya kitumbua chako yaani madaraka hata
kwa sanduku la kura, huyo ni mhalifu. Tena siyo wa kupeleka mahakamani
bali kupiga na ikiwezekana kuua kabisa.
Wakati watu wengine wakiitafsiri amani kuwa ni
hali ya watu kutosheka kiuchumi na kijamii, wengine wanaona amani ni
kundi la watu wachache kufaidi utamu wa nchi bila bugdha. Amani kwa
tabaka la viongozi na matajiri ni utamu wao kutoguswa na kundi la
wasionacho.
Kundi hilo la wachache limejijengea ngome za
kijeshi, yoyote anayetoa mawazo mbadala ni adui, hata kama nchi yetu
inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Bahati mbaya majeshi yetu yamejengwa katika
misingi ya utii, yaani kutii kila mari inayotoka kwa mkubwa. Sasa mkubwa
kashawaambia pigeni, tunatarajia nini, ni kipigo kipigo, kipigo.
Ndiyo maana mwanafalsafa wa zamani wa Ujerumani,
Karl Marx aliwahi kusema kuwa, katika kila jamii kuna makundi mawili ya
walionacho, na wasionacho (ambao ni wengi); ili wasionacho wafanikiwe ni
lazima kundi hilo lifanye mapinduzi kwa kundi la walionacho.
Hapa sizungumzii mapinduzi ya kijeshi, ila nchi
yetu inahitaji mapinduzi ya kifikra kutoka kwa wasionacho. Ni lazima
tabaka la viongozi likubali kukosolewa iwe ni kwa vyombo vya habari,
maandamano, mikutano na njia nyinginezo.
Huo ndiyo uhuru unaoweza pia kutumika kuwasifia viongozi hao kama watafanya vizuri.
Kama alivyosema Pinda, nchi yetu inafuata utawala
wa sheria, hivyo tufuate utaratibu wa sharia kwa vitendo kwa kuwakamata
watuhumiwa wote – wanaotii amri na wakaidi na kuwafikisha mahakamani. Lakini kwa tangazo la Waziri Mkuu Pinda kinachofuata ni kipigo tu, na kipigo si lelemama matokeo yake ni majeruhi na hata vifo.
No comments: