Mtwara. Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji jana aliachiwa baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na mahakama
Mtwara. Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji
jana aliachiwa baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na mahakama na
kumwezesha kuwa huru kwa dhamana.
Mbunge huyo alirudishwa rumande juzi kutokana na
kushindwa kutimiza masharti. Sharti hilo lilikuwa ni kuwa na hati ya
kusafiria ambayo aliiacha Dar es Salaam.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mtwara, Dynes Lyimo
alimwachia mbunge huyo kwa dhamana na hivyo kumtaka mtuhumiwa na
mdhamini wake kusaini hati za kumtolea dhamana.
Baada ya maelezo yote, hakimu Lyimo aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 4,mwaka huu mahakamani hapo.
Mbunge huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi mkoani hapa mwishoni mwa wiki akituhumiwa kwa kosa la uchochezi
anaodaiwa kuufanya Januari 19, mwaka huu eneo la Ligula mkoani hapa.
Hata hivyo viongozi wengine wa vyama vya siasa vya
upinzani wanaohusishwa na vurugu za gesi wanatarajiwa kufikishwa
mahakamani kwa mara nyingine kesho kusikiliza kesi inayowakabili yenye
makosa matatu.
Viongozi hao ni Katani Ahmed Katani (33) na Said
Kulaga (45) wa CUF, Hassan Uledi (35) wa NCCR Mageuzi na Hamza Licheta
(51) wa TLP, wote wakazi wa Mtwara.
Mbunge huyo pamoja na wenzake hao wanashtakiwa kwa
makosa ya uchochezi yaliyopelekea kufanyika kwa vurugu na kusababisha
uvunjivu wa amani na mali za watu pamoja na miundombinu kuharibiwa
vibaya.
No comments: