Washington. Rais wa Marekani Barrack Obama amemteua msaidizi wake wa karibu, Mark Childress kuwa balozi wa nchi hiyo, hapa nchin
Rais wa Marekani, Barack Obama (kushoto) akizungumza na washauri wake
waandamizi akiwemo Mark Childress (kulia) ambaye amemteua kuwa balozi
mpya wa nchi hiyo hapa nchini
Obama amefanya uteuzi huo ikiwa ni wiki moja tangu
alipohitimisha ziara yake katika nchi tatu za Bara la Afrika, Tanzania
ikiwa mojawapo. Pia alizitembelea Senegal na Afrika Kusini.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ikulu ya
Marekani jana ilisema nafasi hiyo inahitaji kuidhinishwa na Bunge la
Seneti la nchi hiyo. Uteuzi wake unaweza kuwa na maana kubwa katika
kutekeleza sera za nje za Marekani.
Katika miaka ya karibuni, Tanzania imeshuhudia
ziara za viongozi wakuu wa nchi hiyo nchini ambao ni Bill Clinton,
George Bush na Obama.
Kuteuliwa kwa Childress, kunaashiria kwamba Balozi wa sasa wa Marekani nchini Alfonso Lenhardt anakaribia kumaliza muda wake.
Awali, Childress ambaye aliwahi kuwa msaidizi na
msiri wa muda mrefu wa Seneta wa zamani, Tom Daschle, alitarajiwa
kushika moja ya nyadhifa mbili katika utawala wa Rais Obama ambazo ni
Mkuu wa Utumishi katika Idara ya Huduma ya Afya ya Jamii (HHS) au Naibu
Mkurugenzi katika Ofisi ya Maboresho ya Afya katika Ikulu ya Marekani.
Hata hivyo, jina lake liliondolewa katika
mapendekezo ya uteuzi wa kuongoza ofisi hizo baada ya kuhusishwa katika
masuala ya kodi Februari 2009, hivyo kubaki pasipo na jukumu maalumu.
Pamoja na mkanganyiko uliojitokeza awali kuhusu
majukumu yake, Childress alimudu kufanya kazi kubwa katika kuwezesha
kupitishwa kisha kutekelezwa kwa mabadiliko makubwa katika sekta ya afya
ya nchi hiyo. Aliteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Utumishi wa Marekani, 2012.
Mwaka 2009, mpigania mabadiliko na maboresho ya
sekta ya afya Marekani ambaye sasa ni Seneta, Edward M. Kennedy
alimwomba Childress kujiunga na timu yake ya ushauri wa masuala ya afya,
elimu, wafanyakazi na pensheni.
Timu hiyo pia ilikuwa na kazi ya kumshauri kuhusu
masuala ya mabadiliko ya afya na Childress alikuwa miongoni mwa watu
walioshiriki kutoa rasimu ya kwanza ya muswada wa Sheria ya Mabadiliko
ya Afya 2009.
Baada ya muswada huo kupitishwa Februari 2010,
Childress aliondoka katika kamati hiyo na kujiunga na Idara ya Huduma ya
Afya ya Jamii Marekani ambako alikuwa na wajibu wa kusimamia
utekelezaji wa sheria hiyo mpya akiwa Kaimu Msimamizi Mkuu wa idara
hiyo.
Childress ni mwanasheria aliyebobea katika masuala ya kanuni za uhakika wa chakula na dawa akifanya kazi hiyo jijini Washington.
Katika miaka yake ya utumishi katika Seneti ya
Marekani (Capitol Hill) akiwa na Maseneta; Daschle na Kennedy, mara
nyingi aliteuliwa kuongoza midahalo ya usuluhishi wa migogoro ya masuala
nyeti ndani ya Seneti na kuratibu majadiliano muhimu kama vile uteuzi
wa watendaji wa Mahakama.
Mark Childress pia anatajwa kuwa mmoja wa watu wa
karibu sana na Obama, huku akielezwa kuwa mmoja wa watu wenye nguvu
kubwa ya ushawishi katika uongozi wa sasa wa Rais wa Marekani.
Tangu alipojiunga na timu ya Obama baada ya
Uchaguzi Mkuu wa 2008, Childress amekuwa na nafasi muhimu na amekuwa
akitumika katika kuweka sawa mambo magumu yanayojitokeza White House.
Anatajwa pia kuwa mmoja wa watu ambao wamekuwa
wakitumika kusahihisha makosa mengi yanayofanywa na utawala wa Obama
hasa katika Ikulu ya Marekani.
Childress (53) akitokea Carolina ya Kaskazini, pia
ameongoza katika kukabili tuhuma dhidi ya Taasisi za Ukusanyaji Kodi
Marekani ambazo zilikuwa zikiwagusa wahafidhina.
Anatajwa kwamba siyo mtu wa kupenda kujulikana na
katika mtandao wa Wikipedia, maelezo kuhusu maisha yake na kazi
alizofanya ni mistari miwili tu.
Gazeti la Washington Post linampigia debe
Childress kwamba ana sifa nyingi zinazoeleza mafanikio katika kazi zake
alizowahi kufanya na kwamba ‘anafaa kwa wadhifa aliopewa wa kuwa Balozi
nchini Tanzania’.
Naibu Meya wa Los Angeles, Jay Carson ambaye
aliwahi kuwa msemaji wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton
alinukuliwa akimwita Childress kuwa ni ‘mtu mwenye akili nyingi’, ambaye
ana uwezo wa kutanzua mizozo mipya yenye kukanganya.
Tanzanian Shilling Converter
No comments: