Ads Top

NEC Misungwi yaitaka TANROADS kutoa Elimu

Na Antony Sollo Mwanza.
July 22, 2014

MJUMBE wa mkutano Mkuu wa chama cha Mapinduzi Wilayani Misungwi Jackob Dalali Shibiliti amewataka wakala wa Barabara Nchini TANROADS Mkoa wa Mwanza kufika katika kijiji cha Misasi Wilayani Misungwi kuzungumza na wananchi kuhusu operesheni ya bomoabomoa ya nyumba zilizo ndani ya hifadhi ya barabara.

Akizungumza na Tanzania Daima Shibiliti alisema kuwa juni 6 mwaka huu  wakala wa barabara Mkoa wa Mwanza,walipita wakitangaza juu ya Operesheni hiyo ambayo itafanyika kupisha ujenzi wa barabara ya Mwanangwa Salawi lakini akishangazwa na uamzi usio shirikishi kwa wananchi kwa kuwa,hakuna mkutano wowote uliowakutanisha wadau na kujadili faida za ujenzi wa barabara hiyo.

Katika ufuatiliaji wake Mjumbe huyo wa NEC alikutana na watendaji wa TANROADS Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo ya kina huku akiwaomba wafike katika vijiji vinavyopitiwa na mradi huo kwa ajili ya kutoa Elimu kwa wananchi hao.

Shibiliti amevitaja vijiji vitakavyopitiwa na mradi huo kuwa ni Mwawile, Misasi, Kijima Busongo, kabala, Mwagiligili na Inonelwa na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupatiwa elimu hiyo ili kuweza kujua faida na hasara ya mradi huo.

Wakitoa maoni yao baadhi ya wazee wa maeneo ya Misasi akiwemo Msafiri Mchenya wameishauri Tanroads kuangalia uwezekano wa kuipitishia barabara pembeni mwa mji kwa ajili ya kuondoa usumbufu kwa wananchi na pia kuepuka matumizi mabaya ya fedha za umma kwa, kuwa hakukuwepo taarifa na elimu juu ya hifadhi ya barabara tangu mwanzo hivyo kuonekana kuwa jambo hili sasa ni jipya.

Tanzania Daima lilifika Ofisi za wakala wa barabara kujua hatma ya mchakato huo na kukutana na Mhandisi wa Barabara kuu Mkoa wa Mwanza Pius Joseph ambaye alikanusha madai hayo na kusema kuwa lengo lililowapeleka huko ni kutoa elimu juu ya sheria mpya ya hifadhi ya barabara na 13 ya mwaka 2007 (Road Act No 13 of 2007).

Pius alisema kuwa, kwa mujibu wa kanuni ya 29 (1)A na B ya mwaka 2009 ya sheria hii eneo la hifadhi ya barabara limeongezeka na kuwa mita 60 (sitini) yaani mita 30 kuanzia katikati ya barabara kila upande kwa barabara zote kuu na Mkoa.

Mhandisi Joseph aliendelea kufafanua kuwa hapo awali eneo la barabara lilikuwa ni mita 45 yaani mita 22.5 kila upande wa barabara na kusema kuwa kuanzia sasa wananchi wafahamu kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria kujenga nyumba,kufyatua matofali,kulima au kufanya shughuli yoyote ndani ya mita 60 (sitini) yaani mita 30 kila upande wa barabara.

Tanzania Daima linayo nakala ya maelekezo ya Meneja wa wakala wa barabara Mkoa yenye kumb Na TNRD/RM/MZA/B.1570/VI/40 ikifafanua juu ya kwenda kwa wataalamu hao wilayani misungwi kwa lengo la kutoa elimu na si kwenda kutoa taarifa ya kuvunjwa kwa nyumba za wananchi wilayani humo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Nathan Mshana alipotafutwa kuzungumzia suala hilo simu yake iliita bila kupokelewa na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Mwisho.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.