Magufuli atangaza ujio barabara za juu Dar
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliwasilisha makadirio ya
matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/13 ambayo imetenga fedha kwa
ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara za juu (flyovers), kama moja
ya hatua za kupambana na msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.Kwa
ujumla wake, miradi ya kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar
es Salaam thamani yake ni Sh899.063 bilioni, lakini fedha ambazo
zimetengwa katika mwaka huu wa fedha ni Sh37.578 bilioni tu sawa na
asilimia 4.17 tu ya mahitaji hayo.
Dk Magufuli alisema
maandalizi ya ujenzi wa barabara za juu ambayo yametengewa fedha za
ndani Sh2 bilioni, unatarajiwa kuanzia katika eneo la Tazara, makutano
ya Barabara za Mandela na Nyerere na ujenzi huo utafadhiliwa Serikali ya
Japan kupitia shirika lake la misaada (JICA).
Waziri alisema upembuzi wa mradi huo chini ya JICA tayari umekamilika.
“Wizara
inaendelea na mpango wa kujenga Flyovers katika Jiji la Dar es Salaam
ili kupunguza msongamano. Usanifu katika eneo la makutano ya Barabara ya
Mandela na Nyerere umekamilika chini ya JICA na mradi utajengwa na JICA
wenyewe mwaka huu wa fedha,” alisema Dk Magufuli
Hata hivyo,
Kamati ya Miundombinu ya Bunge ilipinga ujenzi wa flyovers katika
makutano ya barabara za Mandela na Nyerere na kueleza kuwa utaongeza
tatizo badala ya kulipunguza.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo,
Makamu Mwenyekiti Anne Kilango Malecela, alisema kuwa kama Serikali
haitakuwa makini itajikuta ikiongeza tatizo badala ya kuliondoa.
Kamati
hiyo ilishauri kuwa Serikali iwe makini na ujenzi wa barabara za juu
katika maeneo mengine kwani barabara ikijengwa katika eneo moja inakuwa
ni kero kwa maeneo jirani na hivyo kufanya msongamano kuwa ni mkubwa
zaidi.
Mikakati mingine
Dk Magufuli aliitaja
miradi mingine ambayo inalenga kupunguza msongamano wa magari katika
Jiji la Dar es Salaam kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za pete (Ring
Roads) zenye urefu wa kilometa 98.15.
Alisema mpango huo
umetengewa Sh3.273 bilioni ambazo zitatumika kukamilisha kazi
zilizobakia katika barabara ya Kituo cha Mabasi Ubungo - Kigogo –
mzunguko (roundabout) ya Kawawa – bonde la Msimbazi – makutano ya Twiga
na Jangwani.
Pia katika mpango huo wa kupunguza msongamano wa
magari jijini Dar es Salaam, Barabara ya Jet Corner – Vituka hadi Devis
Corner nayo itakamilishwa.
“Kiasi cha Sh577 milioni kimetengwa
kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Ubungo Maziwa – External na Tabata
Dampo – Kigogo na Sh1 bilioni kimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa
kiwango cha lami kwa barabara ya Kimara – Kilungule – External,”
alisema Dk Magufuli na kuongeza:
“Sh2 bilioni zimetengwa kwa
ajili ya barabara ya Mbezi (Morogoro Road) –Malambamawili (pamoja na
barabara iendayo Shule ya Msingi Malambamawili – Kinyerezi – Banana,
Sh2.1 bilioni kwa ajili ya barabara ya Tegeta Kibaoni – Wazo Hill – Goba
hadi Mbezi na Sh1 bilioni kwa ajili ya barabara ya Tangi Bovu – Goba”.
Alisema
Sh577 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Kimara –
Baruti – Msewe hadi Changanyikeni, wakati ufuatiliaji na usimamizi wa
ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo kwa kasi (Bus Rapid Transit
Infrastructure) umetengewa Sh50 milioni.
Alisema wizara hiyo
kupitia Tanroads pia itazihudumia barabara ambazo ziko chini ya wakala
huyo wa barabara na kwamba kazi hiyo imetengewa Sh18 bilioni. “Wizara
pia ina mpango wa kujenga Dar es Salaam – Chalinze-Morogoro Express Way
kwa utaratibu wa Public Private Partnership (PPP),” alisema.
Alisema
daraja la Kigamboni limetengewa Sh2.788 bilioni Barabara ya Sam Nujoma
Sh 318.36 milioni ambazo zitatumika kulipa sehemu ya malipo ya mwisho ya
mkandarasi.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, Barabara ya Kilwa
imetengewa Sh8.1 bilioni kwa ajili ya kukarabati na kupanua barabara ya
lami kutoka njia mbili hadi nne kati ya Gerezani na Mbagala kwa msaada
kutoka Serikali ya Japan na Serikali ya Tanzania.
“Mradi huu
unatekelezwa kwa awamu nne ambapo awamu ya kwanza inahusisha sehemu ya
Bendera Tatu – Mtoni kwa Azizi Ally, awamu ya pili inahusisha sehemu ya
Mtoni kwa Azizi Ally – Mbagala Zakhem, awamu ya tatu inahusisha sehemu
ya Mbagala Zakhem – Mbagala Rangi Tatu na awamu ya nne inahusisha
upanuzi wa sehemu ya Bendera Tatu – Gerezani,” alisema.
Alisema
awamu ya kwanza na ya pili imejengwa kwa msaada wa fedha kutoka Serikali
ya Japan na kwamba mkataba wa awamu ya tatu ulisainiwa Oktoba 19, 2010
na umekamilika Mei, 2012.
Alisema katika mwaka wa fedha 2012/13
mradi wa Mbagala Zhakhem – Mbagala Rangi Tatu umetengewa Sh1.5 bilioni
zitakazotumika kulipia sehemu ya malipo ya kazi hizo.
“Aidha,
kiasi cha Sh6.6 bilioni kimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya upanuzi wa
sehemu ya Bendera Tatu – Gerezani (Kamata),”alisema.
Kuhusu
maegesho ya vivuko Dar es Salaam – Bagamoyo yametengewa kiasi cha Sh2
bilioni na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo – Msata
umetengewa Sh7.396 bilioni na barabara zilizokasimiwa Wizara ya Ujenzi
kupitia Tanroads zimetengewa Sh4.398 bilioni.
Mfuko wa Barabara
Kwa
mujibu wa Magufuli, katika mwaka wa fedha 2012/13 kiasi cha Sh 300.76
bilioni kutoka Mfuko wa Barabara zitatumika kwa ajili ya kufanya
matengenezo ya barabara.
“Kati ya fedha hizo, Wizara ya Ujenzi
imetengewa Sh29,775,720,000 na Tanroads Sh 267,981,436,800 huku Bodi ya
Barabara ikiwa imetengewa Sh3,007,643,200,’’ alieleza.
Katika
hatua nyingine, Waziri alisema kuwa Wizara imetenga jumla ya Sh 420
milioni kwa ajili ya kufanya maandalizi ya ujenzi wa nyumba 10,000 za
watumishi wa Serikali katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Alisema
katika kipindi cha mwaka 2012/13 wizara kupitia Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA), imepanga kujenga nyumba 2500 katika mikoa yote Tanzania
Bara ambapo jumla ya Sh180 bilioni zitatumika kukamilisha mradi huo.
Jumla
ya Sh1,023.033 trilioni ziliombwa na wizara hiyo kwa ajili ya
kukamilisha shughuli mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2012/13 ambapo fedha
hizo ni pamoja na miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo.
No comments: