Ads Top

RIPOTI YA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU MKOANI KAGERA.

Ripoti hii ni jumla ya matukio mbalimbali pamoja na vitendo vya ukiukwaji wa Haki za Binadamu ambavyo vimeshamiri katika maeneo ya Mkoa wa Kagera pamoja na haya niliyoyashuhudia kwa macho na kuyasikia kwa masikio yangu,napenda kutoa Ripoti hii ili Uongozi wa Kituo cha sheria na Haki za Binadamu pamoja na waangalizi wa Haki za Binadamu kwa pamoja,tuweze kuunda timu maalumu itakayoenda Mkoani ikiwa ni pamoja naWanasheria ili kuyapatia ufumbuzi matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi wa Tanzania waishio katika maeneo ya Mpakani mwa nchi yetu kama ifuatavyo:-
Kabla ya kuyataja mambo ambayo yanapaswa kushughulikiwa naomba kuainisha matatizo sugu niliyoyaona kuwa haya ndiyo chanzo cha ukiukwaji wa Haki za Binadamu Mipakani mwa nchi yetu hususani Mikoa ya Kigoma na Kagera:
A:  Watumishi wa Serikali kukaa muda mrefu katika vituo vyao vya kazi
B:  Rushwa kubwa wanazoshiriki kwa asilimia 100 viongozi wa Serikali.
C:  Ukabila
D:  Mawasiliano Duni katika maeneo yanapofanyika matendo ya ukiukwaji
      Wa Haki za Binadamu katika maeneo mbalimbali nchini.
E:  Kutokuwa na Viongozi wazalendo wanaosimamia dhamana Watanzania
F:  Katika mipaka ya nchi yetu ambapo kuna vitendo vingi vya uporaji
      Vinavyofanywa na watumishi wa Serikali kwa manufaa yao kupitia
      Mwamvuli wa Oporesheni ya kuwabaini wahamiaji Haramu.
G:  Uwepo wa Mtandao wa watumishi wa umma unaoshirikiana na
      Wahalifu kwa kuwapa nafasi ya kuishi katika nchi isivyo halali.
 
Kufuatia sababu nilizozitaja hapo juu naomba kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo :-
A:  Watumishi wa Serikali kukaa muda mrefu katika vituo vyao vya kazi :
 Kwa kawaida mtu akifanya kazi katika kituo chake  kwa zaidi ya miaka 30 ni lazima kutatokea madhara makubwa sana kwa vile mtumishi huyo atakuwa hana tofauti na wanafamilia wa maeneo hayo na hatokuwa tayari kuwajibika ipasavyo ili kulinda maslahi ya Taifa na matokeo yake ataanza kufanya kazi kwa mazoea na kujinufaisha zaidi kupitia shida zinazowasumbua wananchi  kama ilivyo kwa watumishi wa idara mbalimbali za Serikali Mkoani Kagera.
Wanaotuhumiwa kukaa muda mrefu ni watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro ambapo hata baada ya kufanya mahojiano na Mkurugenzi wa Halmashauri alikiri kuwepo kwa tuhuma mbalimbali alizowahi kuzisikia na baada ya kuzifanyia kazi zilionekana kuwa ni za kweli ambapo tayari kulikuwa na Afisa mmoja katika Idara ya Elimu ambaye tayari amehamishwa kitengo baada ya kubainika kuwa alikuwa akiwajibu vibaya wananchi kwa ajili ya kukaa na kufanya kazi kwa mazoea.
B:  Rushwa kubwa wanazoshiriki kwa asilimia 100 viongozi wa Serikali:
Upande wa Rushwa hiki ni kikwazo kikubwa cha kupatikana kwa Haki katika maeneo mbalimbali nchini hususani Mkoani Kagera kwa kuwa nimeshuhudia kwa macho yangu Idadi kubwa ya Raia wanchi za Burundi,Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakimiliki uchumi mkubwa katika maeneo hayo na wala hakuna kiongozi anayediriki kuwaeleza lolote kwa kuwa inaelezwa kuwa viongozi mbalimbali wanahusika kuwapa hifadhi na kuwahakikishia ulinzi kwa gharama yoyote  na hali hii nimeishuhudia Nyegezi Mkoani Mwanza baada ya kutukanwa kwa Serikali ya Tanzania kuwa Serikali haipo na kama ipo imelala usingizi kwa kuwa watu hawa yaani wahamiaji haramu hupelekwa lakini hurudi baada ya kuwahonga viongozi wa serikali yetu ya Tanzania kiasi kikubwa cha fedha.
  C:  Ukabila:
Suala la ukabila limepandikizwa kandokando ya mipaka hii mpaka inafikia wananchi sasa kutambuana kwa Makabila yao ambapo kwa sasa kabila la wasukuma na baadhi ya makabira yaliyoko Mkoani Kagera wameanza kushambuliana kwa kutumia lugha za ukabila.
D:  Mawasiliano Duni katika maeneo yanapofanyika matendo ya ukiukwaji:
Inaonyesha kuwa kuhusu suala la mawasiliano ni moja ya matatizo makubwa ambayo ni kikwazo kwa ajili ya usalama wanchi yetu kwa vile hakuna hata waandishi wa habari wanaoweza kufuatilia taarifa mbalimbali na kuzitoa katika vyombo vya habari ili jamii iweze kusikia matukio hayo isipokuwa kama kuna mwandishi anayeweza kufanya hivyo si mwandishi wa kawaida bali ni mmoja wa Wanaharakati kwani upo ugumu wa utumaji wa taarifa na ripoti mbalimbali kufuatia mazingira ya maeneo hayo kuwa magumu.
E:  Kutokuwa na Viongozi wazalendo wanaosimamia dhamana Watanzania:
Kuna viongozi kweli ambao hawana uzalendo kabisa na zaidi wanafanya kazi kwa mazoea na wao kuwa watu wakisubiri kuletewa taarifa badala ya kwenda kujifunza na kuzibaini shida na matatizo yanayaikabili jamii matokeo yake inashangaza sana kusikia kiongozi akisema hana taarifa na jambo nyeti kama ukiukwaji wa Haki za raia na mali zao na kwa kweli iwapo tunataka kuwa na taifa lenye viongozi walio tayari kushughulika na kero za wananchi  hatuna budi kuishauri serikali kuwaondoa viongozi wote walioko mipakani kwa kuwa wako huko kwa ajili ya kufanya kazi kwa maslahi yao na si kwa ajili ya kuwatumikia watanzania kama yalivyokuwa malengo ya aliyewateua
F:  Katika mipaka ya nchi yetu ambapo kuna vitendo vingi vya uporaji
      Vinavyofanywa na watumishi wa Serikali kwa manufaa yao kupitia
      Mwamvuli wa Oporesheni ya kuwabaini wahamiaji Haramu.
Katika hili sasa kuna tuhuma zinawalenga viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwamo Viongozi wa Matawi,Vitongoji,Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Viongozi wa Jeshi la Polisi,Wanyama Pori,Mgambo, Mahakama na baadhi ya Wanajeshi wa JWTZ ambao wameshafanya uporaji wa mali za wananchi na ikiwemo kutoza faini ya Mamilioni ya shilingi,kuchangisha fedha kiasi cha mpaka kufikia 200,000/= 600,000/= hadi kufikia 6,000,000/=ambapo walioweza kusalimika katika zoezi hili na kuachwa salama ni makundi ya wahamiaji haramu kutoka nchi jirani kama nilivyozitaja katika kipengele kilichopo hapo juu ambapo baadhi ya Wananchi ambao ni raia wa Tanzania waliposhindwa kutimiza matakwa ya viongozi hawa kilichotokea ni kuchomewa nyumba zao na kuachwa wakiwa hawana chakula na wala hakuna mahitaji mbalimbali muhimu kwa jamii jambo ambalo hadi sasa kina mama wanajifungulia nje hususani vichakani na hawana msaada wowote.
Wapo wafugaji walioporwa mifugo yao na sasa wamefunguliwa kesi mbalimbali kuhakikisha wana 
shindwa kupeleka madai yao mbele ya sheria ili waweze kurejeshewa mali zao ,wapo pia wananchi waliopoteza familia zao akiwemo Mzee Numbu Yihorogo ambaye mpaka sasa Mke na watoto wake hawajulikani walipo na baadhi ya mifugo yake imeporwa na maafisa wa Wanyama pori na matokeo yake hadi sasa anaishi kwa wasamalia wema zipo ng’ombe zenye thamani ya mamilioni ya shilingi zimefyatuliwa risasi na kuuawa na sasa wafugaji hawa hawana pa kuanzia kudai fidia ya mali zao na sasa wanaomba msaada wa Wanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ili waweze kusaidiwa kufungua kesi ya madai dhidi ya serikali kwa kuwaachia watumishi wake kuwafanyia unyama mkubwa na kuwaita  
WAHAMIAJI HARAMU NDANI YA NCHI YAO KINYUME NA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.
  G:  Uwepo wa Mtandao wa watumishi wa umma unaoshirikiana na
      Wahalifu kwa kuwapa nafasi ya kuishi katika nchi isivyo halali.
Katika hili pia  kuna uhakika wa madai haya kwa kuwa mimi nikiwa ndani ya Basi la Kampuni ya Bunda Bus nikitoka Bukoba Jeshi la Polisi  Mkoani Geita walikamata madawa ya kulevya aina ya mirungi na kuniomba kuwa shahidi wa tukio hilo ambapo zipo taarifa zinazodai kuwa mmoja wa watuhumiwa wa kusafirisha dawa hizo ni mke wa askari mwenye cheo kikubwa ndani ya jeshi hilo Mkoani Geita na sasa imepelekea kuachiwa huru kwa mtuhumiwa huyo.
MAPENDEKEZO:
Baadhi ya mambo ambayo mimi binafsi naomba yafanyiwe marekebisho ya haraka nia kama ifuatavyo:
·        Watumishi mbalimbali  wa Serikali walioko mpakani wakiwemo Askari polisi,Wanyama Pori,Mgambo, JWTZ ,Wakuu wa Wilaya,Mikoa, na baadhi ya Wananchi wanaotuhumiwa kushirikiana na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani nilizozitaja hapo juu na viongozi wa Mamlaka ya Mapato,Uhamiaji, wachukuliwe hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi kwa kuwa wameinajisi Serikali kwa kuwanyanyasa wananchi ambao ni Raia halali na matokeo wameingiza makundi makubwa ya wahamiaji haramu huku wakiwahalalisha baada ya kupewa rushwa jambo ambalo ni kinyume na taratibu za nchi yetu.
·        Kwa kuwa uwepo wa viongozi wasio waadilifu katika mipaka ya nchi yetu upo uwezekano wa kuwa na raia wa kigeni wengi ambao watakuja kupatiwa vitambulisho vya taifa na kuondoa maana ya zoezi zima la kuratibu orodha ya watanzania ambao pia ni raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo kutumia gharama nyingi katika zoezi ambalo hakutakuwa na tija.

·        WANAHARAKATI WOTE TUUNGANE NA KUELEKEZA MACHO YETU MIPAKA YOTE ILI KUHAKIKISHA TUNAWAMULIKA VIONGOZI WASIOWAJIBIKA KATIKA NAFASI ZAO NA PIA TIMU KUTOKA LHRC NA THRD ZIKAPIGE KAMBI  KWA MUDA MKOANI KAGERA KUWEKA AMANI KWA WANANCHI WANAOTISHIWA USALAMA WAO KILA WAKATI NA LITOLEWE TAMKO RASMI KUHUSU  MATATIZO YALIYOPO MAENEO HAYO ILI KURUDISHA IMANI KWA WANANCHI WANAOHAMISHWA  KWA KUONEWA MAANA HADI SASA WAKO NJIA PANDA NA HAWAJUI HATMA YAO:
 
RIPOTI HII IMEANDALIWA NA :
ANTONY JOHNSON SOLLO
S.L.P 1288 – KISHAPU
SHINYANGA
Mob: +255 787 565533 Email antonyjilala@yahoo.com

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.