Ads Top

Wanachama Yanga kuchangia Sh250 U/Kaunda

 
Mashabiki ya timu ya Yanga.  

WANACHAMA wa Yanga kila mmoja anatakiwa kuchangia Sh250 kila wiki sawa na Sh200 milioni kwa mwaka ili kufanikisha ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa Kaunda, jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay Dar es Salaam, uongozi wa Yanga  uliwahakikishia wanachama wa klabu hiyo kuwa ujenzi wa Uwanja wa Kaunda unaanza mwezi Juni kama ulivyopangwa na sasa kinachotakiwa ni kupatikana kwa Sh32 bilioni.
Kwa mujibu wa uongozi wa Yanga, tayari wameshafanya mazungumzo na Kampuni ya Unit Trust of Tanzania ambao ni wataalamu wa kiuchumi wenye uwezo wa kufanya mipango ya upatikanaji wa fedha kupitia benki na taasisi za kifedha na kwamba hadi mwezi Mei fedha hizo zitakuwa zimeshapatikana.
Uongozi huo pia uliwataka wanachama wa Yanga kila mmoja kuchangia Sh250 kila wiki kwa lengo la kupata Sh8 bilioni kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwamo makusanyo ya ada za uanachama, michango mbalimbali, harambee, Kalenda na mauzo ya jezi na bidhaa zenye nembo ya Yanga ili kuwezesha kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo.
Katika hatua nyingine Makamu mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alitangaza kuwavua rasmi uanachama aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa na msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu  pamoja na mwanasheria Godwin anayemiliki Kampuni ya Auda & Company Advocates kwa kile alichoeleza kuwa wamekiuka katiba ya Yanga kwa kuishtaki klabu hiyo wakati wao ni wanachama.
Mwesigwa ameishtaki Yanga kwa kuwa anaidai Sh183.4 milioni, wakati Sendeu anadai Sh79.9 milioni huku mwanasheria Godwin anadai Sh4.5 milioni baada ya kupewa jukumu la kushughulikia kesi ya Steven Marashi na Wisdom Ndlovu.
Mbali na hilo pia Sanga alisema kamati yake ya utendaji imeamua kufuta posho zote zilizokuwa zikitolewa kwa wajumbe wa Kamati ya utendaji ya Yanga.
KATIBA YAGOMA
Wanachama wa Yanga jana waligomea kufanya marekebisho ya katiba ya kupitisha kipengele cha kumchagua mwenyekiti na makamu, iwapo wanamaliza muda wao basi wachague viongozi wengine wawapendao kuwarithi.
Hoja hiyo ilipingwa vikali kwa madai kuwa hawataki kuburuzwa katika hilo na badala yake waachiwe uhuru wao wa kuchagua kiongozi wanayemtaka kama ilivyo sasa.
Kipengele hicho cha tano kilichowasilishwa na uongozi wa Yanga cha marekebisho ya katiba katika uchaguzi wa viongozi wa Yanga kilisema kutakuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambao watakuwa na tiketi moja na pamoja waunde kamati ya utendaji yenye nguvu ya kuajiri na kufukuza pale inapohitajika.
Pia kipengele hicho kilisema mwenyekiti na makamu wachague Kamati ya utendaji wanayoitaka wao kwa sababu Kamati ya utendaji iliyopo hivi sasa iliyochaguliwa na wanachama, baadhi ya wajumbe wanaonekana siyo waaminifu, ambapo wanachama waliridhia uamuzi huo.
“Naombeni ridhaa yenu ya kuchagua kamati ya utendaji ninayoitaka, hii niliyonayo naona wengine siyo waaminifu na wamekuwa wakiutukana uongozi,” alisema kiongozi mmoja wa Yanga. bofya hapa kwa habari zaidi..>>>>

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.