Rais wa Venezuela Hugo Chavez afariki
Wafuasi wa Hugo Chavez wamekuwa wakimuombea aweze kuugua pole
Katika taarifa kwa taifa,
makamu wa rais wa Venezuela Nicholas Marduro ametangaza kufariki dunia
kwa rais Hugo Chavez, 58, kufuatia kuugua muda mrefu maradhi ya
Saratani. Rais Chavez ametoweka katika hadhira ya nchi hiyo kwa muda
mrefu ambapo alikuwa anapokea matibabu nchi jirani ya Cuba.
Alirejea , mjini Caracas mnamo Februari 18 kwa
mara ya kwanza tangu maradhi yake yamzidie ambapo alipelekwa hospitali
ya kijeshi kuendelea kupokea matibau. Hata hivyo maelezo zaidi
hayakutolewa juu ya afya yake. Waandamanaji waliandamana katika mji mkuu
Caracas mwishoni mwa juma wakidai kuwa watu wa Venezuela wanapaswa
kupewa habari zaidi kuhusu afya ya rais wao
Bwana Chavez amekua uongozini nchini
Venezuela kwa miaka 14 na anatazamiwa kuleta mageuzi makubwa
yaliyolenga zaidi kuimarisha maisha ya raia wa pato la chini.
Ujumbe wa Jeshi
Taarifa kutoka kwa jeshi imesema kuwa
wataendelea kuilinda hadhi ya nchi na kuimarisha usalama. Pia jeshi
limeahidi kuendelea kuwa waaminifu kwa makamu wa rais Nicholas Marduro
na wakatoa wito kwa raia kuwa watulivu.
Chavez - wasifu
Hugo Chavez alijitosa katika siasa za
Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa luteni katika jeshi. Aliongoza
mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos Andres Perez.
Lakini
kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo
wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na
aliwekwa korokoroni.
Aliingia uongozini baada ya ushindi mkubwa
ulioviondosha vyama vya kisiasa wakati huo. Katika kuapishwa kwake mnamo
February 1999, Hugo Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya
mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi sio kampeni tu. Alitimiza ahadi yake
na kuiongoza nchi hiyo katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa
katika muda wa miongo kadhaa. Alibadili muundo wa bunge na kulifanya
kuwa la kikatiba, ambalo liliiunda katiba mpya baada ya kura ya maoni
iliyoidhinishwa na 88% ya wapiga kura.
Rais Chavez alitaifisha rasilmali ukiwemo
utajiri wake mkubwa wa mafuta. Sera kama hizi zilimfanya azozane na
kampuni za kimataifa za mafuta, lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa
watu maskini
No comments: