Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amewatumia salamu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela akiwataka wasithubutu kuvuruga uchaguzi wa kata nne utakaofanyika mwezi ujao.
Uchaguzi mdogo wa kata nne za wilaya za Arusha umepangwa kufanyika Juni 16, mwaka huu.
Akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Ngarenaro, Arusha Lema alisema yeye na wafuasi hawatakubali kuona wakipokonywa haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka kwenye uchaguzi huo.
Amemtunishia misuli Mkuu wa Mkoa ikiwa siku chache baada ya kuachiwa kwa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za uchochezi.
Mbunge huyo anatuhumiwa kuwahamasisha wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kumzomea Mulongo wakati alipokwenda kuwatuliza walipotishia kuandamana baada ya kifo cha mwanafunzi mwenzao, Henry Kago, wiki iliyopita. “Ninawatahadharisha viongozi hawa wasithubutu kutumia vyombo vya dola kwa nia ya kukipa ushindi Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye kata hizo. Waache uchaguzi ufanyike kwa amani.
“Tutahakikisha tunapiga kampeni usiku na mchana na pia tutalinda kura zetu siku ya uchaguzi ili tusipokonywe,” alisema.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya walipotafutwa kuzungumzia madai hayo ya Lema hawakupatikana na walipopigiwa simu, ziliita bila ya kupokewa na hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) hawakujibu.
Lema alisema ataripoti bungeni Jumatatu ijayo lakini atarejea Arusha kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo mdogo zilizopangwa kuanza Mei 15 na kumalizika Juni 15, mwaka huu.
“Niko tayari kuachia posho za bungeni katika muda huo ili nishiriki kwenye kampeni za uchaguzi huu,” alisema Lema.
Joto la uchaguzi huo limeanza kupanda katika Jiji la Arusha katika Kata nne za Themi, Kaloleni, Elerai na Kimandolu na watu wapatao 60 wamechukua fomu ili kuwania kupitishwa na Chadema kugombea nafasi hizo.
Hata hivyo, amelalamikia kutoitishwa kwa uchaguzi mdogo wa Kata ya Sombetini ambayo pia haina diwani baada ya Mawazo Alphonce kupitia CCM kujitoa na kujiunga na Chadema na ameapa kupigania kuitishwa kwa uchaguzi wa Sombetini pia katika kipindi hicho.
No comments: