Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimempongeza Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu kwa uamuzi wake wa kugoma kujitoa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuadi kuwa kwa kitendo hicho ameonyesha uzalendo mkubwa kwa taifa lake
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari
ambapo alisema, Profesa Baregu ameweka maslahi ya taifa mbele badala ya
vyama.
Kauli hiyo ya CCM imekuja muda mfupi baada ya
vyombo vya habari kuandika habari zinazohusu Profesa Baregu kukataa
kujitoa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba hiyo licha ya Chadema kutaka
afanye hivyo kwa kile kinachodaiwa kuwa, CCM imeteka mchakato wa Katiba
kwa kuingiza makada na viongozi wake wengi katika mabaraza ya Katiba.
Baregu alikaririwa akisema hakuna tatizo katika
tume hiyo na kwamba chama chake kinahitaji kujishauri upya kuhusu
kusudio lake la kutaka kususia mchakato huo.
Baregu alifika mbali zaidi aliposema kama angeambiwa achague nchi yake na chama basi angechagua nchi kwanza.
Jana Nape alisema,“CCM inampongeza kwa dhati
Profesa Baregu kwa uzalendo na ukomavu wa kisiasa aliouonyesha kwa
kuwakatalia kujitoa kwenye tume na kuweka mbele maslahi ya taifa lake,
huyu ni mfano wa kuigwa ameweka pembeni uchadema wake kwa kuthamini
utaifa.”
Alisema kitendo cha Baregu kukataa kujitoa kwenye
tume inapaswa kuwa fundisho kwa chama hicho kuondokana na tabia za
kitoto za kususa.
Alisema Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa
Katiba na Sheria, Tundu Lissu alitoa malalamiko bungeni kwamba CCM
imeteka mchakato wa Katiba Mpya kwa kujaza makada wengi katika mabaraza
hayo.
“Wajifunze kutoka kwetu, wakati CCM inahamasisha
wananchi washiriki kwenye mchakato wa Katiba, wao Chadema wanahamasisha
watu wavuruge mchakato huo kwa maslahi wanayofahamu wenyewe,” alisema.
“Tunapongeza msimamo wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kwa kupuuza hoja ya kufuta mabaraza ya Katiba, kama wanasusa sisi
tutaendelea na mchakato,” alisema Nape.
Alisema nchi nyingi hasa za kiafrika, zimekuwa
zikikumbwa na machafuko yanayosababishwa na upatikanaji wa Katiba na
kwamba wananchi wanatakiwa kuwa makini na malengo ya chama hicho.
“ Chadema wanaona Watanzania wanaendelea na
mchakato bila machafuko wanakosa majibu kwa mabeberu wanaowafadhili
kuchafua nchi yetu, ndiyo maana kila kukicha wanakuja na visa na vituko
kusumbua mchakato wa Katiba,” alisema Nape.
Aidha, chama hicho kimewalaumu baadhi ya wabunge wa Chadema
kutumia Bunge kama jukwaa la kuwashambulia watu ambao hawana fursa ya
kuingia bungeni kujibu mashambulizi hayo.
“Utamaduni huo ni wa hovyo na unakiuka haki za
msingi za binadamu ambazo zinataka mtu anayetuhumiwa kupewa fursa ya
kusikilizwa,” alisema Nape.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu
wa Chadema, Wilbroad Slaa na Msemaji wa Chadema, John Mnyika
walipopigiwa simu hawakupatikana jana
No comments: