Dar es Salaam. Hatima ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuendelea kushiriki au kutoshiriki kwenye mchakato wa Mabadiliko ya Katiba Mpya itajulikana baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho.
Kamati
hiyo inatarajiwa kukutana katika vikao vyake vya kawaida vya kila baada
ya miezi mitatu kujadili majibu ya Serikali yaliyotolewa bungeni na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na yale ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba Mpya, Jaji Mstaafu Joseph Warioba hivi karibuni.
Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alisema jana kwamba hawawezi kukurupuka
kufanya uamuzi wa kujitoa na kuuacha mchakato huo ukatawaliwa na CCM
jambo ambalo litasababisha kupata Katiba isiyokuwa na mashiko kwa
mustakabali wa taifa.
Alisema tamko alilolitoa Mwenyekiti wa chama
hicho, Freeman Mbowe bungeni hivi karibuni ilikuwa ni uamuzi wa Kamati
Kuu hivyo na Serikali pamoja na Tume imejibu kwa kiwango chake.
“Mbowe
alitoa tamko linalotokana na maagizo ya Kamati Kuu. Hayakuwa maagizo ya
Mbowe .Chadema hata siku moja haitoi na kabla ya siku ya mwisho Warioba
alitoa jibu hakututaja lakini alikuwa anajibu hoja zetu,Waziri Mkuu
ndani ya Bunge katoa jibu,”alisema.
“Chadema haikurupuki tena,
tumeshapata aina gani ya majibu. Kinachofuata tunarudi kwenye Kamati Kuu
tunawaambia haya ndiyo majibu ya Warioba haya ndiyo majibu ya Pinda
bungeni, tuendelee au tusiendelee, tukiendelea utaratibu wa kujitoa
uweje.”
Dk Slaa alisema vikao vya Chadema vinaitishwa kikatiba,
lakini kutokana na rasimu ya Mabadiliko ya Katiba kutolewa mwezi huu
kulingana na ratiba wataweza kujadili mambo yote.
Akifafanua kuhusu
Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ambaye ni mwakilishi wa
chama hicho,Profesa Mwesiga Baregu alisema endapo Chadema kitajitoa
kisheria mjumbe huyo atakuwa amejitoa kwani atakuwa hana
anayemwakilisha.
“Tutapigania mpaka Katiba ya wananchi ipatikane,
ibara ya 8 inasema Serikali itapata mamlaka yake kutoka kwa wananchi,
lakini hivi sasa wananchi wamegeuzwa watumwa.Tunataka Katiba ambayo
wananchi wanaisimamia Serikali yao tofauti na ilivyo sasa,”alisema Dk
Slaa.
Aprili 30 mwaka huu,Jaji Warioba aliwataka wanasiasa kuacha
tabia ya kutaka kuhodhi mjadala wa Katiba Mpya na badala yake waheshimu
uhuru wa makundi yote ya wananchi kuchangia Katiba Mpya.
Alisema wao kama tume hawawezi kufanya kazi kwa shinikizo la wanasiasa bali watafuata mwongozo.
uliopo ambao utaisaidia nchi kupata Katiba ya Watanzania na si matakwa ya vikundi.
“Tusipoondokana
na suala la kujiweka vipandevipande hatutapata Katiba Mpya na wala
kufikia mwafaka, ni lazima tufanye uamuzi mgumu ili tupate Katiba
Mpya,”alisema Jaji Warioba.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa msaidizi
wa Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) Mwigulu Nchemba, Ntundu Emmanuel
amehamia Chadema na kukabidhiwa kadi na Dk Slaa.
No comments: