Nairobi. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto wametajwa katika ripoti inayowahusisha na ghasia za baada ya uchaguzi katika ripoti iliyosubiriwa kwa muda mrefu kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamau nchini humo
Ripoti hiyo hata hivyo haikutoa mapendekezo ya hatua inazotaka kuchukuliwa dhidi ya Rais Kenyatta na makamu wake, William Ruto.
Mwenyekiti wa tume hiyo, aliiambia BBC kuwa ni kwa
sababu wawili hao wanakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu
katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC.
Tume ya maridhiano na haki ilikabidhiwa jukumu la
kuchunguza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa tangu
mwaka 1963 nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake.
Iliundwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa
mwaka 2007/08 uliozua ghasia miaka mitano iliyopita kama njia ya kuleta
maridhiano miongoni mwa wakenya.
Baada ya uchaguzi huo, watu 1,500 waliuawa na
wengine zaidi ya 600,000 kulazimika kukimbia kutoka katika makazi yao.
Kenyatta na Ruto, waliokuwa mahasimu katika uchaguzi wa mwaka 2007,
walishinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Machi baada ya kuungana chini
ya Muungano wa Jubilee.
Licha ya kuwa hakuna mapendekezo yaliyotolewa na
tume hiyo dhidi ya Rais na naibu wake, inapendekeza uchunguzi zaidi
dhidi ya maofisa wakuu waliotajwa kuhusika na ghasia za baada ya
uchaguzi mwaka 2007 na hata kufunguliwa mashtaka Baadhi ya waliotajwa ni
pamoja na Waziri mpya wa Madini, Najib Balala na maseneta wawili.
Hata hivyo tume hiyo ilimtaka Rais Kenyatta
kuwaomba radhi Wakenya kwa makosa waliyotendewa chini ya Serikali
zilizopita katika kipindi cha miezi sita tangu kukabidhiwa ripoti hiyo
juzi.
Rais mstaafu Daniel arap Moi pia alitajwa katika
ripoti hiyo akihusishwa na mauaji ya waliokuwa wanasiasa mashuhuri
wakati wa utawala wake.
No comments: