NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE
Kila mwanamke aliye na hekima huijenga nyumba yake: Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe’. Tafsiri
ya neno nyumba ni familia, naam na familia inajumuisha baba, mama na
watoto endapo mmejaliwa. Hata hivyo katika hali ya kawaida watoto
watalelewa katika msingi mzuri endapo ndoa husika imetengamaa. Ifahamike
kwamba hili andiko si la wanandoa peke yao, bali hata wanawake wasio
wanandoa wenye familia kama wajane, walezi nk linawahusu. Kwa kuwa hapa
tunazungumzia habari za wanandoa nitalifafanua zaidi kutoka kwenye kona
hiyo. Pia neno nyumba limetumika ili kutupatia urahisi wa kuelewa namna
nyumba za kawaida zinavyojengwa ili tueguze dhana hiyo kiroho pia. Kwa
lugha rahisi ndoa yako ni nyumba, hivyo ubora, uzuri na mvuto wa ndoa
yako unategemea namna unavyoijenga daima kwa hekima.
Ni vizuri ukafahamu kwamba suala la
ujenzi/maboresho ya ndoa yako ni jukumu la kila siku ya kuishi kwa ndoa
yenu mpaka kifo kiwatenganishe. Kila mmoja katika ndoa ni lazima
ahakikishe anasimama kwenye nafasi yake na kufanya yale yampasayo ili
kuifanya ndoa yake kuwa bora zaidi. Endapo hakutakuwa na jitihada za
wanandoa katika kuimarisha ndoa yao, Shetani atatumia fursa hiyo
kuivuruga ndoa husika. Kujenga kunakozungumziwa hapa ni kule
kuhakikisha ndani ya ndoa kuna mahusiano na mawasiliano mazuri baina
yenu ambayo yatafanikisha kutekelezwa kwa kusudi la Mungu.
Ukweli wa ajabu na wa pekee
Ni ajabu sana kuona kwamba jukumu la
ujenzi wa ndoa/nyumba amepewa mwanamke. Hii haina maana mwanaume
hahusiki, hapana, bali ki-nafasi jukumu la ujenzi wa nyumba/ndoa ni la
kwako mama. Kumbuka nilikueleza kwamba nafasi hizi tano za Mwanamke
katika ndoa zinafanya kazi kwa pamoja na kwa kutegemeana. Katika nafasi
hii ya ujenzi unapaswa kuhakikisha unajenga ndoa yako ili kuzuia kila ufa/fursa ambayo Shetani anaweza kutumia kuvuruga ndoa yako.
Kumbuka katika hali ya kawaida kujenga ni kuimarisha/kuweka mazingira
bora juu ya kile unachokithamini ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea.
Naam nafasi hii inalenga kukusaidia uwe makini sana na kila kinachoweza
kubomoa ndoa yake.
Suala la ujenzi wa ndoa ni endelevu kwa sababu siku zote adui anatafuta kubomoa ndoa yako. Ni lazima uwe makini kujua
wapi ni mahali palipobomoka ambapo Shetani anapatumia sasa kuharibu
ndoa yako au anaweza kutumia baadaye kuharibu ndoa yako, naam ukishajua
kwa kutumia hekima, jenga ukuta imara ambao adui hawezi penya. Kama
ndoa yako ina nyufa basi ni rahisi adui kupita kwenye hizo nyufa.
Kumbuka hata kama umemaliza kujenga kila kitu kwenye nyumba yako, bado
kuna matengenezo ya mara kwa mara yanahitajika ili kuifanya nyumba yako
kudumu katika hadhi inayostahili.
Maeneo ya msingi katika kujenga ndoa yako
- Utiifu kwa mumeo
Maandiko yanasisitiza sana wanawake
kuwatii waume zao (Waefeso 5:22-24, 1 Petro 3:1). Mitume
walindika maandiko haya ili kuwaonya wanawake kutokana na mienendo yao
mbele za waume zao kitabia na hasa katika suala zima la utiifu. Bahati
mbaya baadhi ya akina mama sio watiifu kwa waume zao na tena wengine
wana dharau kubwa sana. Naam fahamu kwamba Mke si Mke bila Mume, na Mume
si Mume bila Mke. Hata siku moja ndoa yako haiwezi kujengwa kwa kiburi
au dharau kwa mumeo bali utakuwa unaumba jambo baya sana ndani ya mume
wako.
Najua unaweza ukasema tabia za mume wangu ndiyo zinazifanya kumdharau, kumsema vibaya nk. Suala
sio tabia zake, bali ni wewe kutumia hekima katika kukabiliana na tabia
zisifofaa za mumeo kwa kuwa kumdharau ni kuendelea kubomoa na si
kujenga, naam ni kuendelea kuleta tatizo na sio kutatua tatizo.
Umeshawahi kuwaza juu ya jambo hili kwamba, Mke anaagizwa kumtii mume
wake kama vile kumtii Bwana. Imeandikwa katika Waefeso 5:22 ‘Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu’. Je ni kweli ndivyo unavyomtii Mumeo? Naam haijalishi mume wako yukoje usionyeshe dharau, mtiii tu, ni mume wako.
Mtume Petro anawaonya wanawake akisema ‘kadhalika
ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno,
wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno’ (1Petro 3:1).
Sijui kama wewe Msomaji unaona uzito uliopo kwenye mistari hii. Kwa
lugha nyepesi utiifu wa mke kwa Mume utawafanya wengine kumwamini Yesu
mnayemtumaini. Naam na upande wa pili, kukosa utiifu kwa mumeo
kutawazuia wengine kumwamini Yesu, je unajua gharama ya kuwazuia wengine
kumjua Kristo kwa sababu ya kukosa utiifu kwa mumeo (asomaye na afahamu
siri hizi).
Wanaume kadhaa walioko kwenye ndoa
wamekuwa wakiniambia kwenye suala la tabia hawajaona tofauti kati ya
wanawake wasiokoka na waliokoka. Na kikubwa wanachosema ni kudharauliwa
na wake zao. Hata kama katika hali ya kawaida mumeo anafanya mambo
yanayopelekea wengine kumdharau wewe usifanye hivyo yeye ni kichwa chako
Fahamu kwamba daharau ni sumu mbaya
kwenye ndoa yako yako mama, jizuie kabisa. Naam utiifu ni kila kitu kwa
Mwanume, binafsi nimegundua wanachotafuta wanaume kwa wake zao bila
kujali elimu zao, uchumi wao nk ni utiifu, naam kumdharau mumeo ni
kubomoa nyumba yako ni kumruhusu Shetani kuharibu ndoa yako, ni
kumuingiza mume wako fikra za wanawake wengine tofauti na wewe.
- Kutunza siri za mume wako
Katika kuijenga nyumba yako ni lazima
ujifunze kutunza, kuhifadhi na kuficha mapungufu ya mumeo kwa wengine.
Naam hiyo ndiyo hekima. Baadhi ya akina mama bila hata kujali
wanaongea na nani, wamekuwa wakieleza mambo ya ndoa yao na siri za waume
bila hata kujua athari yake. Naam kufanya hivyoni kubomoa na si
kujenga. Unawajibika kmtii na kumtunzia mumeo siri zake licha ya
mapungufu aliyo nayo na uzidi kumwomba Mungu kwamba aiponye ndoa yako.
Naam na hata kama ni muhimu uwaeleze kwa
lengo la kujenga basi ni muhimu kuwe na mipaka ya nani unazungumza naye
na nini unawaweleza maana si kila kitu wanapaswa kujua cha wewe na
mumeo. Katika kulisistiza jambo hili Paulo anawagiza Tito akimweleza
kwamba awatumie Wazee wa kike wenye mwenendo wa utakatifu ‘Ili
wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto
wao, na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa
wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe’ (Tito 2:3-4).
- Matumizi ya kinywa chako
Mara kadhaa nimewasikia wanawake
walioolewa wakisema maneno yasiyofaa kwa waume zao. Najua wengine ni
kutokana na hasira na wengine kutokana na mfululizo wa matukio yasiyofaa
ya mumewe. Nimesikiia wanawake wakiwaaita waume zao wajinga, wapumbavu,
na mengine ambayo nisinependa kuandika hapa. Ninachotaka ukijue ni
hiki, imeandikwa Mtu atashiba kwa matunda ya kinywa chake.
Tambua kwamba mume wako naye ana nafasi
zake kama mwanandoa kwako, na nafasi moja wapo ni kuwa kichwa cha
mwanamke. Sasa kila baya unalotamka kwake maana yake unaliumba kwenye
kichwa chako mwenyewe na hivyo tarajia mabaya na uharibifu kwenye ndoa
yako. Najua utaniambia Patrick kuna mambo yanaudhi sana na hayavumiliki,
na mimi nitakujibu ni kweli lakini namna ya kushughulika nayo ni wewe
kutumia hekima kama mjenzi na kuiponya ndoa yako na si kumesema vibaya.
Fahamu pia kwamba katika ulimwengu wa
roho kuna pepo ambao kazi yao ni kufuatilia maneno/mawazo mabaya ambayo
mtu anayanena ili kuyaumba yatimie. Mfano ukiwa na wazo kwamba kwamba
Mume wangu si mzuri uwe una uhakika kuna pepo watakuja juu yako na
kuhakikisha siku zote wana kufanya umuone mume wako mbaya.
Je hujasoma Zaburi 36: 4 inasemaje ‘Huwaza maovu kitandani pake, hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii”.
Naam tafsiri yake ni kwamba hali ya sasa ya mtu huyo ni matokeo ya
mawazo yake, naam mwanandoa huyu amewaza na kunena mabaya juu ya mume
wake, na kwa sababu hiyo ameiingiza ndoa yake kwenye mabaya. Naam ni
lazima ujifunze kunena mananeo yenye kuijenga ndoa yako na si kubomoa,
ndivyo na nafsi yako, fikra zako zitakapokiri hivyo, naam ndivyo na
BWANA Mungu naye atahakikisha hayo yanakujia.
- Msamaha (kusameheana)
Ndoa nyingi leo zinashida kwa sababu ya
wanandoa kushindwa kusameheana. Ni kweli kwenye ndoa kuna mambo mengi
ambayo katika hali ya kibinadamu yanaweza kukufanya ushindwe kusamehe,
nami kama Mwalimu sina budi kukufundisha kile ambacho neno la Mungu
limeelekeza. Kumbuka imeandikwa tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote…
(Waebrania 12:14). Naam watu wote wa kwanza akiwa na mumeo, hatutegemei
uwe na mahusainao mazuri na watu wa nje, wakati mume wako hutaki
kumsamehe, utakuwa unajidanganya nafsi yako.
Hivyo bila kujali Mumeo amefanya kosa
ganii hakuna namna ni lazima ujifunze kusamehe na kusahau. Hii ni kwa
sababu kutokusamehe ni kumpa Ibilisi nafasi ya kuendelea kuwavuruga. Si
hivyo bali usitegemee kwamba hata maombi yenu nyote wawili yatakuwa
yanasikilizwa. Maana kwa kushindwa kwako kusamehe una haribu mahusiano
na Mungu (Mathayo 6:14) na kwa mwanaume kwa kushindwa kwake kukaa kwa
akili na wewe kama mke, maandiko yanasema maombi yake hayatasikilizwa.
Je unategemea nini kitatokea kama hautakuwa tayari kumsamehe.
- Kujali mahitaji ya mwenzako (tendo la ndoa)
Paulo Mtume aliwaandikia hivi wanandoa wa Korinto ‘Lakini
kwa sababu ya zinaa kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe, na kila
mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na
vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili
wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali
mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa
kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi
kwenu’ (1Wakorinto 7:1-5).
Kimsingi andiko hili linalenga wanandoa
wote wawili, bali kwa kuwa ujumbe huu ni maalum kwa wanawake nitaandika
zaidi upande wa mwanamke. Biblia iko wazi kwamba kwa sababu ya zinaa
(tendo la ndoa) kila mume awe na mke wake mwenyewe. Moja ya sababu
muhimu za wewe kuolewa ni ili kumtosheleza mumeo kwa habari ya tendo la
ndoa kama ilivyo na kwako pia.
Kwa wanandoa wengi haja ya tendo la ndoa
inatofautina, hata hivyo mara nyingi uhitaji wa tendo la ndoa kwa
Mwanaume uko juu kuliko ilivyo kwa mwanamke. Hata hivyo kila mmoja ana –
muhitaji mwenzake ili kutoshelezwa katika hitaji hili muhimu. Baadhi ya
wanawake kwa kujua ukweli huu na tofauti hii ya uhitaji wa tendo la
ndoa, kwa kutokufikiri athari zake kwa wenzi wao, kwao binafsi na
‘future’ yao huwanyima waume zao haki yao ya tendo la ndoa hasa pale
wanapokuwa wametofautiana juu ya jambo fulani. Mbaya zaidi wapo akina
mama ambao wakikasirika huwanyima waume zao haki hii ya msingi kwa muda
mrefu kwa mfano mwezi mmoja, minne, hata zaidi ya mwaka na wanaishi
nyumba moja na wengine wanalala kitanda kimoja.
Mume wako akijua kwamba unatumia
ugomvi/tofauti zenu au hata kwa makusudi kumnyima haki yake ya tendo la
ndoa, na jambo hilo likawa endelevu uwe na uhakika taratibu unaanza
kuharibu ndoa yako. Maana, Shetani ni mzuri sana wa kutumia nafasi
ambazo wana wa Mungu wanampa. Ndani ya mume wako yataingia mawazo mabaya
(Ezekieli 38:10) na kumweleza ‘je mbona kuna wanawake wengi, ni suala
la kwenda kumaliza haja yako kwa mwanamke yoyote mwingine’. Wazo jingine
pia litamwambia kwa nini huyu mwanamke akutese kiasi hiki, kwa nini
usiwe na nyumba ndogo nk. Uwe na uhakika endapo mumeo ameokoka, hofu ya
Mungu ndani yake ndiyo itakayomzuia kufanya mambo haya lakini ukimuuliza
taratibu atakuambia mawazo haya hunijia mara kwa mara unaponinyima haki
yangu ya tendo la ndoa.
Naam, hata kama hatafanya hayo, uwe
na uhakika kwamba tayari kwenye ufahamu wake umeshapanda mbegu mbaya na
itaendelea kukua endapo utaendelea na tabia yako ya kumnyima haki yake. Ndiyo,
usishangae siku moja kukuta mumeo ametoka nje ya ndoa, usikimbilie
kumlaumu Shetani, maana wewe ndiye ulifungua mlango na kumkaribisha.
Nakumbuka mwanandoa mmoja (Mwanaume) alisema hizi ndoa za Kikristo
zinatutesa sana wanaume, na zinawafanya hawa wanawake wajisahau sana,
kwa kuwa wanajua Biblia imetuzia kuoa mke zaidi ya mmoja. Naam ilibidi
nitumie muda mwingi kurejesha ufahamu wa huyu ndugu kwenye msingi wa
ki-Mungu kwa kuwa nilijua tayari kuna wazo lilishaingia moyoni mwake na
nilijua wapi linampeleka.
Nimeandika jambo hili kwa kirefu kwa
sababu mara nyingi sehemu kubwa ya kesi za wanandoa inapofika kwenye
suala la unyumba, wanawake ndio wanao – wanyima waume zao. Naam nakiri
hata wanaume wapo lakini ni mara chache sio kama ilivyo kwa wanawake.
Mwanamke sikia, kitendo cha Mungu kukupa huyo mume ni heshima ya pekee
sana kwamba ni wa kwako pekee yako. Ukitaka kujua gharama yake waulize
wanawake ambao wana ‘share’ mume namna inavyowagharimu kihisia, kifikra
na kimaisha. Naam ni lazima ujifunze kujali na kutimiza mahitaji ya
mwenzi wako vinginevyo unafungua mlango kwenye ufahamu wa mumeo na
kumwambia angalia kule nje kuna wanawake wengine (Asomaye na afahamu).
Ukweli ni kwamba kuna sababu mbalimbali
ambazo hupelekea wanawake kwenye ndoa kufanya hivyo, ila ushauri wangu
ni kwamba, uamuzi wa namna hii (kumnyima tendo la ndoa mumeo) ni wa
kuharibu na si kujenga. Hivyo haijalishi huyo baba kakukosea nini (labda
ziwe issue za kiafya), suala la tendo la ndoa kwake ni muhimu sana na
ni haki yake, kutokumpa haki yake ni kukaribisha Shetani kwenye ndoa
yako. Naam ni vizuri mka-hakikisha kwamba tofauti zenu zote mna –
zimaliza kabla hamjaingia kulala, itawasaidia sana.
Kuna maeneo ambayo ningeweza kuandika
pia, lakini hayo matano hapo juu ni msingi wa mengine mengi. Kutokana na
urefu wa nafasi hii ya Mwanamke kama Mjenzi nimelazimika kuigawanya
mara mbili kwa hiyo katika sehemu ya tano nitamalizia kipande
kilichobaki ambacho ndani yake nitaonyesha mwanamke anawezaje kupata hekima ya kumsaidia kuafanya haya na nitaweka baadhi ya mifano yenye kusaidia.
No comments: