Ads Top

Tanga. Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amesema ni wajibu na haki kwa waandishi wa habari nchini “kudai kwa sauti kubwa” wale walioshiriki katika kuwadhuru wenzao watiwe nguvuni na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

  Chikawe alisema Serikali inasikitishwa na madhara mbalimbali ambayo waandishi wa habari wamekuwa wakikumbana nayo katika utekelezaji wa majukumu na kazi zao kiasi cha wengine kupoteza maisha.
Akifungua Mkutano wa Pili wa mashauriano baina ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Chikawe alisema Serikali inatambua mazingira magumu na hatarishi ambayo yanawakabili waandishi wa habari pamoja na changamoto ambazo zinawakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kauli ya waziri huyo ni ya kwanza kuzungumzia suala la mateso kwa waandishi wa habari kwa undani, kwani kabla viongozi wakuu wa Serikali wamekuwa wakikwepa kuzungumzia suala hilo.
Hivi karibuni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara hakuzungumzia suala la usalama wa waandishi wa habari wakati akiwasilisha hotuba ya matumizi ya wizara yake na wabunge waliojaribu kuzungumzia mateso yanayowapata waandishi wa habari hawakupata ruhusa ya kutoa wanayoyafahamu.
Lakini jana Waziri Chikawe ni kama alibadili mwelekeo huo pale aliposema: “Mnayo haki na kwa hakika ni wajibu wenu kudai kwa sauti kubwa wale walioshiriki katika kuwadhuru wanahabari watiwe nguvuni na kufikishwa katika vyombo vya sheria”.
Waziri Chikawe aliongeza: “Kwa kushirikiana na ninyi, Serikali itaendelea kuhakikisha mazingira ya kazi ya waandishi yanaboreshwa na pale ambapo maisha ya waandishi yanakuwa hatarini, Serikali haitasita kuchunguza na kuchukua hatua stahiki.’’.
Alitoa salamu za pole kwa wanahabari na ndugu wa waandishi wa habari waliopata madhara.
mbalimbali na kwamba Serikali iko pamoja nao na inatambua mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo ya nchi.
Waziri Chikawe pia alizungumzia kazi za MCT na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kusema kwamba vyombo hivyo ni muhimu kwani vinafanya kazi kubwa ya kusimamia tasnia ya habari nchini.
“Kwangu Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri ni vyombo muhimu katika tasnia hii. Hivi ndivyo vyombo pekee ambavyo vina uwezo wa kuifanya tasnia ya habari ijisimamie yenyewe. Vyombo hivi vinaijua tasnia ya habari ilikotoka, iliko na inakokwenda, naamini tukivitumia vizuri tuna uwezo wa kujisimamia wenyewe na kuboresha utendaji kazi wetu,”alisema Chikawe.
Alisema MCT na TEF vinapaswa kuendelea kutekeleza wajibu wake wa kuwakemea baadhi ya waandishi wa habari wanaochafua au kudhalilisha taaluma ya habari na kwamba vinapaswa kufanya hivyo kwa dhati ili kulinda maadili ya taaluma hiyo.
“Lakini mtambue katika tasnia ya habari Mhariri asipokuwa imara na makini chombo chake cha habari kinaweza kisitoe matokeo yanayo tarajiwa na wanachi wetu. Mwisho wa siku walaji watakataa bidhaa dhaifu wanazoletewa,”alisema Chikawe.
Pia Chikawe alizungumzia mpango wa kuendesha shughuli za Serikali kwa uwazi (OGP ) unaolenga kukuza uadilifu na kuimarisha uwazi kwa umma, kuimarisha usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na kupambana na rushwa.
Alisema kupitia mpango huo ndio maana Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa Sheria ya Haki ya Kupata Habari (Right to Information) inatungwa kwa kuwashirikisha wadau wote ili kuwapa wananchi haki ya kutafuta habari na kuzitumia kwa maendeleo yao.
Akizungumza wakati akimkaribisha Waziri kufungua mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mkajanga alisema ingawa vyombo vingine vya habari vinamilikiwa na watu binafsi, lakini MCT imebeba dhima ya kuvisimamia.
Hata hivyo, alisema wahariri wa vyombo hivyo wanawajibika kutoa mrejesho kwa MCT ikiwa ni pamoja na kukosoa maamuzi yasiyo sahihi.
Huu ni mkutano wa pili wa mwaka unaoandaliwa na MCT kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini kujadili masuala mbalimbali yakiwemo usalama wa waandishi wa habari na bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana,    

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.