Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewatuhumu viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jeshi la Polisi kwa kupanga njama ili kuwaunganisha viongozi wa juu wa Chadema kwenye kesi ya kumwagiwa tindikali, Mussa Tesha
Viongozi waliotajwa hadharani kuwa wanapanga mbinu hizo ni Naibu
Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba na Ofisa wa Jeshi la Polisi
makao makuu, Advocate Nyombi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Uenezi, John Mnyika alisema mikakati
hiyo imesababisha kukamatwa kwa Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam,
Henry Kileo wiki iliyopita na kupelekwa Igunga, mkoani Tabora
kuunganishwa kwenye kesi hiyo.
Kileo alikamatwa na kupelekwa makao makuu ya Jeshi
la Polisi ambako alihojiwa na jopo la maofisa wa polisi. Kwa mujibu wa
Mnyika baada kuhojiwa aliwekwa mahali pasipojulikana na kwamba alizuiwa
kuwekewa dhamana.
Mnyika alisema siku iliyofuata, walielezwa kwamba
Kileo alipelekwa Igunga kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka akituhumiwa
kumwagia tindikali Tesha.
“Tumepata taarifa kwamba Kileo aliteswa vibaya na
polisi ili awataje viongozi waliomtuma lakini alikuwa akibishana nao,
lakini baadaye aliandikisha mambo waliyoyataka polisi,” alisema.
Akijibu tuhuma hizo, Nchemba alisema hakuna
mikakati yoyote inayofanywa kati yake na Nyombi bali hiyo ni hofu yao
viongozi wa Chadema kwa sababu wanafahamu kwamba walitenda kitendo
hicho.
“Hatuhitaji kikao kudhihirisha hilo kwa sababu ni
jambo lililo wazi kwamba Chadema walihusika katika kitendo hicho cha
kumwagia tindikali mtu huyo,” alisema.
Kwa upande wake, Nyombi na Msemaji wa Polisi
hawakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Kamanda wa Mkoa wa Tabora,
Peter Ouma alisema jeshi hilo litawasaka wahalifu popote walipo na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria bila kujali kama ni wanachama wa
vyama fulani au la.
“Mhalifu anaweza pia kuwa mwanachama wa chama
fulani kwa hiyo tukimkamata tusihusishwe na mambo ya siasa bali ni
kufuata sheria,” alisema kuongeza kuwa Kileo bado hajafikishwa mkoani
humo.”
Chadema imeunda jopo la mawakili saba wakiongozwa
na Profesa Abdallah Safari na wengine ni Peter Kibatara na Gasper
Mwalyela wanaoondoka leo kwenda Igunga wakati Mabere Marando, Tundu
Lissu, Nyaronyo Kicheere na Method Kimomogoro watawafuata baadae.
No comments: