Ads Top

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewaagiza Watanzania kuwa na uzalendo wa kuwaenzi na kuwakumbuka wenzao ambao wamefanya kazi muda mrefu kwa kuthamini mchango wao

 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
 
Pinda alitoa kauli hiyo juzi katika viwanja vya Bunge, aliposhiriki hafla ya kuwaaga wafanyakazi waliostaafu utumishi na wale waliohamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuanzia 2010.
Hata hivyo, Pinda alisema  yeye ndiye aliyemwagiza Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia kuandaa hafla hiyo ili kuwatunuku zawadi na kula nao chakula pamoja na watumishi hao, ambao idadi yao ilikuwa 59 kutoka sehemu mbalimbali nchini. Hata hivyo walihudhuria 35.
Juzi ilikuwa ni siku ya pili mfululizo kwa Pinda kushirikia warsha katika viwanja hivyo, siku iliyotangulia alikuwa ameshiriki  sherehe kubwa iliyoandaliwa na Bunge kumwaga Spika Mstaafu ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye alitumikia nafasi ya Uspika kwa miaka mitano 2005/10.
 Sherehe ya juzi ambayo iliandaliwa kwa agizo la Pinda, inapingana na kauli na maagizo yake ambayo amekuwa akitoa kwa nyakati tofauti kwamba, makongamano na warsha zisizo na tija ni ufujaji fedha za umma.
“Mimi ndiye niliyeamua kufanya hivi na huu ni ubinadamu tu nikaona nimtume mama Ghasia afanye maandalizi hayo, lengo kuu la hapa ni kukaa pamoja na wenzetu na kuwaambia kuwa tunashukuru kwa kazi yenu nzuri na pia tunathamini michango yenu,” alisema Pinda.
Alisema huo ulikuwa ni mwanzo, lakini Tamisemi itakuwa ikifanya hivyo kila mwaka  kuwaaga watu wanaostaafu na wanaohamia wizara zingine.
Kuhusu wastaafu hao, alisema Serikali inapaswa kuwathamini na kutambua michango yao wakati wote kuliko kuwatelekeza kama ilivyo sasa.
Alisema kustaafu kwa mtu sio kwamba anakuwa amepungukiwa hekima na maarifa, bali ni utaratibu ukifika wakati fulani anatakiwa kupumzika.
Licha ya hilo,  aliwaagiza viongozi wa Tamisemi kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watu wanaojiandaa kustaafu ili wajenge nyumba za kufikia na familia zao, kwani wengine humaliza muda  na kushindwa  kujenga. 
Tangu kuingia ateuliwe, Pinda amekuwa akipiga vita sherehe na ununuzi wa magari ya kifahari kwa madai kuwa, ni ubadhirifu wa fedha za umma.
Hatua hiyo inaonyesha ameanza kubariki fedha hizo kufanya sherehe.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.