Dar na Dodoma: Serikali jana ilitangaza Bajeti yake kuu kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambayo inaashiria machungu kutokana na ongezeko la kodi na ushuru katika baadhi ya bidhaa, zikiwamo mafuta, soda, vinywaji vikali pamoja na leseni za magari
Akisoma bajeti hiyo bungeni jana, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa pia alitangaza kuanzisha kodi na ushuru katika huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia simu za mkononi, ikiwamo kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni (commission) ya usafirishaji wa fedha.
“Serikali itaanza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 14.5 kwenye huduma zote (all mobile phone services) za simu za kiganjani/mkononi badala ya muda wa maongezi tu (airtime alone),” alisema Dk Mgimwa na kuongeza: “Katika ushuru huu, asilimia 2.5 zitatumika kugharimia elimu nchini.”
Kutokana na hali hiyo, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dk Oswald Mashindano amelaumu kile alichokiita kuwa ukubwa wa kodi hasa kwa wasio na kipato kikubwa ili kufidia uendeshaji wa Serikali.
“Kama kawaida kutakuwa na ongezeko la mapato ya Serikali kutoka katika vyanzo vyake hasa ukusanyaji wa kodi. Inamaanisha kuwa kutakuwa na mzigo mkubwa kwa walipakodi hasa kundi la wenye kipato kidogo.
“Tofauti na nchi zilizoendelea ambazo wenye mitaji mikubwa ndiyo wanaobanwa kulipa kodi zaidi, nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo, kuna udhaifu mkubwa wa kukusanya kodi,” alisema Dk Mashindano.
Mafuta na magari
Waziri Mgimwa alisema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itapandisha ushuru wa mafuta ya dizeli kutoka Sh215 kwa lita hadi Sh217 kwa lita, likiwa ni ongezeko la shilingi 2.
“Tumeongeza Sh2 tu kwa kuwa tunatambua tukiongeza ushuru mkubwa kwa magari makubwa ambayo yanatoa huduma kwa jamii, tutawaumiza wananchi,” alisema Dk Mgimwa.
Kadhalika, ushuru wa mafuta ya petroli umeongezwa kwa Sh61, kutoka Sh339 kwa lita hadi Sh400. Hata hivyo, imeongeza kiwango cha ushuru wa mafuta (fuel levy) kutoka shilingi 200 kwa lita hadi shilingi 263 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 63 kwa lita na wakati huohuo mafuta hayo yakiongezewa Sh50 kwa kila lita, fedha zitakazotumika kuchangia mfuko wa kusambaza umeme vijijini.
Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), umeongezewa kiasi cha Sh186.9 bilioni ambazo awali, hazikuwa zimetengwa baada ya Serikali kukubaliana na mapendekezo ya Bunge kupitia Kamati yake ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Serikali pia imepandisha viwango vya ada ya mwaka ya leseni za magari. Magari yenye ujazo wa injini yenye ukubwa wa kati ya cc 501 na 1500 yatatozwa Sh150,000 kutoka Sh100,000 za sasa. Magari yenye ujazo wa cc 1501 hadi 2500 kiwango chake kimeongezeka kutoka Sh150,000 hadi Sh200,000 wakati magari yenye ujazo wa injini zaidi ya cc 2501 yatatozwa Sh250,000 kutoka kiwango cha sasa ambacho ni Sh200,000.
Hata hivyo, uamuzi huo hautazigusa bajaji na pikipiki (maarufu kama bodaboda) kwani Dk Mgimwa alisema vyombo ambavyo injini zake zina ujazo chini ya cc 501, ambavyo havitatozwa ada ya leseni. Ushuru pia umeongezwa kwenye magari yasiyokuwa ya uzalishaji na yenye umri wa miaka 10 kutoka asilimia 20 mpaka hadi asilimia 25. Dk Mgimwa alisema hatua hiyo imelenga kupunguza uagizaji wa magari chakavu ili kulinda mazingira na kupunguza ajali za mara kwa mara.
Pombe na Sigara
Bidhaa zisizokuwa za mafuta ambazo zimefanyiwa marekebisho na kuongezwa kodi ni mvinyo, pombe, vinywaji vikali na sigara. Vimeongezwa kodi kwa asilimia 10.
Ongezeko la kodi kwa kipimo cha lita moja ni kwa vinywaji vikali ambayo imepanda kutoka Sh2,392 hadi Sh2,631, sawa na ongezeko la Sh239, bia inayotengenezwa kwa nafaka za nchini ambayo haijaoteshwa, imepanda kutoka Sh310 hadi Sh341, sawa na ongezeko la Sh31 kwa lita wakati bia nyingine zote zimepanda kutoka Sh525 hadi Sh578 sawa na ongezeko la Sh51.
Vinywaji baridi vimepanda kutoka Sh83 kwa lita hadi Sh91 sawa na ongezeko la Sh8 kwa lita.
Sigara zenye kichungi na zinazozalishwa nchini zimepanda kwa asilimia 75, kutoka Sh19,410 hadi Sh21, 351 kwa sigara 1,000 sawa na ongezeko la Sh1.94 na senti 94 kwa sigara moja.
Mabadiliko ya Sheria
Ili kutekeleza uamuzi wa kuongeza ushuru na kodi, Dk Mgimwa amependekeza kufanya maboresho ya sheria mbalimbali za kodi ambazo ni za; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Kodi ya Mapato, Ushuru wa Bidhaa, Ushuru wa Mafuta, Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Sheria ya Usalama Barabarani. Nyingine ni Sheria za; Petroli (Petroleum Act), Uwekezaji Tanzania, Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na marekebisho mengine madogomadogo katika baadhi ya sheria za kodi.
Dk Mgimwa alisema mabadiliko ya Sheria ya Uwekezaji yanalenga kutoza asilimia 25 ya ushuru wa forodha unaopaswa kutozwa kwenye bidhaa zinazotambulika kama “Deemed Capital Goods” (yaani kutoa msamaha wa kodi wa asilimia 75 kwenye bidhaa hizo badala ya asilimia 90 za sasa) na kuondoa baadhi ya bidhaa kwenye orodha ya kupata msamaha.
“Bidhaa hizo ni zile ambazo hazina uasilia wa kuwa bidhaa za mtaji kama vile vifaa vya ofisi, samani, sukari, vinywaji (viburudisho), bidhaa za mafuta ya petroli, magari madogo (Non Utility Motor Vehicles), viyoyozi, majokofu, na vifaa vya kielektroniki, mashuka, vijiko, vikombe nk,” alisema waziri huyo. Alisema marekebisho hayo pia yanalenga kupunguza misamaha ya kodi na kubakiza misamaha yenye tija na yenye kuchochea uwekezaji mkubwa katika sekta za uchumi za kimkakati, hivyo kuongeza mapato ya Serikali.
Alisema pato la taifa linatarajiwa kukua kutoka asilimia 7.0 mwaka 2013 hadi asilimia 7.2 mwaka 2014 na wakati huohuo, bei zikitarajiwa kubaki kwenye viwango vya tarakimu moja na mfumuko wa bei kushuka hadi asilimia 6.0 Juni 2014. Kuhusu akiba ya fedha za kigeni, Dk Mgimwa alisema katika mwaka ujao wa fedha Serikali itajitahidi kuwa na akiba itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
Alisema jitihada zitafanywa ili kupunguza tofauti ya viwango vya riba vya kuweka na kukopa na kuimarisha thamani ya shilingi na kuwa na kiwango imara cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.
Mbowe, wabunge
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe alisema: “Bajeti ya mwaka huu haina jipya” kwani Serikali imeendelea kupandisha kodi katika bidhaa zilizozoeleka badala ya kusimamia kodi kwenye rasilimali za nchi.
“Bajeti hii inaonyesha Serikali ilivyokosa ubunifu wa vyanzo vya mapato, kila mwaka wanapandisha kodi kwenye bia, sigara, magari na mafuta,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisema sheria ya ununuzi ikirekebishwa kama alivyoahidi Waziri Mgimwa itasaidia kupunguza gharama ya bidhaa mbalimbali.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema kuongezwa kwa fedha za mfuko wa vijana ni ukombozi kwa kuwa miaka mingi kilio hicho hakikusikika.
“Tunaona sasa Serikali imekuwa sikivu kwa kuwa kwa muda mrefu tuliomba lakini hatukupewa,” alisema baada ya Serikali kuongeza Sh3 bilioni kwa ajili ya mfuko.
No comments: