Ads Top

DODOMA. Serikali imeainisha maeneo yenye vipaumbele katika Bajeti ya mwaka 2013/2014, iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa na kueleza kuwa fedha zitakazotolewa ni zile zitakazokusanywa


Wananchi wakiwa katika foleni ya kuchota maji.Serikali imesema katika bajeti ya mwaka 2013/14 kipaumbele kitakuwa katika kutatua kero ya maj
Dk Mgimwa alisema Bajeti ya mwaka 2013/2014  itazingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14 na mfumo mpya wa utekelezaji wa vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wizara hiyo mjini Dodoma kabla ya kuwasilisha hotuba yake, Dk Mgimwa alisema kwa kuzingatia sera za uchumi,  misingi na shabaha ya bajeti, Serikali inatarajia kukusanya jumla ya Sh18,249 bilioni kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato vya ndani na nje.
Shabaha na Malengo ya bajeti.
Waziri Mgimwa alisema  bajeti ya 2013/2014 imeelekezwa katika kufikia shabaha na malengo manane, likiwamo la kukua kwa Pato la Taifa kutoka asilimia 7 ya mwaka huu hadi kufikia asilimia 7.2 mwaka ujao.
Mengine ni kudhibiti kupanda kwa bei kutoka asilimia 8.3 hadi kufikia asilimia 6 ifikapo mwakani na kuongeza mapato ya ndani yatakayofikia uwiano wa Pato la Taifa wa asilimia 20.2 katika mwaka wa fedha wa 2013/14 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 17.7 ya mwaka 2013.
Dk Mgimwa alitaja lengo lingine kuwa na nakisi ya bajeti isiyozidi asilimia 5.0 ya Pato la Taifa, kudhibiti ongezeko la ujazo wa fedha katika wigo wa asilimia 15 ifikapo Juni mwakani.
Hali kadhalika, ongezeko hilo kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayokidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne ya  mwaka 2013/14.
Waziri huyo  aliyataja malengo mengine kuwa ni kupunguza tofauti ya viwango vya riba vya benki na kuimarisha thamani ya Shilingi na  kuwa na kiwango imara cha ubadilishanaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.
Misingi ya bajeti ya Serikali 2013/14
Dk Mgimwa alisema ili kufikia shabaha na malengo hayo,  misingi inayokusudiwa na Serikali ni pamoja na kuendelea kuimarisha na kudumisha amani, usalama, utulivu na utengamano na kwamba kuna fedha zilizotengwa  kwa ajili ya kutuliza ghasia. Mingine ni kuzingatia vipaumbele vilivyopo katika mpango wa kwanza wa maendeleo ya miaka mitano, kuboresha mfumo wa utekelezaji wake,  kuimarisha sera za fedha ili ziendane na sera za bajeti  zitakazosaidia kupunguza mfumko wa bei.
Dk Mgimwa alisema msingi mwingine ni kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi.
Mgawanyo wa rasilimali.
Dk Mgimwa alisema Serikali imeweka kipaumbele katika kutatua kero ya maji kwa wananchi,   ambapo kiasi cha Sh747.6 bilioni  zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini. Alisema Serikali pia imetenga Sh2.169 trilioni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ikiwamo barabara, reli, madaraja, bandari na viwanja vya ndege, ikilinganishwa na Sh1.940 trilioni kwa bajeti iliyopita.
Alisema Sh196.8 bilioni katika fedha hizo  zitatumika kuimarisha miundombinu ya reli, zikiwa ni ongezeko la asilimia 46.6 ikilinganishwa na Sh134.2  bilioni katika bajeti iliyopita. “Kwa upande wa nishati na madini, juhudi zitaelekezwa katika kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ambapo Shilingi trilioni 1.426, ikilinganishwa na Shilingi bilioni 731.8 kwa bajeti iliyopita,” alisema.
Sera za matumizi. Waziri Mgimwa alisema Serikali itaendelea kudhibiti matumizi yake katika maeneo mbalimbali.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.