Ads Top

Arusha. Kitendo cha Chadema kutetea viti vyake vinne vya udiwani kwenye uchaguzi mdogo wa juzi, kimetafsiriwa kwamba ni kumfanya Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kukalia kuti kavu

 
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (katikati) akizungumza kwenye Ofisi za Halmashauri ya Arusha akiwa na madiwani wapya wa Chadema waliochaguliwa juzi. Kutoka kushoto mstari wa mbele ni Jeremiah Mpinga (Elerai), Edmund  Kinabo (Themi), Kessy Lewi (Kaloleni) na Rayson Ngowi (Kimandolu).  

Kwa ushindi wake huo, Chadema kimefikisha viti 15 kwenye Baraza la Madiwani la Arusha wakati CCM kimebakiwa kuwa na viti 12 wakati TLP ina viti sita.
Pia Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti zaidi kwani ina nafasi moja ya viti maalum iliyokuwa ikishikiliwa na Rehema Mohamed aliyetimuliwa mwaka 2011.
Mwenyekiti wa madiwani wa Chadema, Isaya Doita alisema jana kwamba ushindi wa juzi ni chachu katika msimamo wa chama chao kutaka uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha urudiwe akiamini kuwa alichaguliwa kimizengwe.
Doita ambaye ni Diwani wa Ngarenaro, alisema wana imani muda si mrefu Jiji la Arusha sasa litapata Meya ambaye amechaguliwa kwa misingi ya sheria.
Chadema ilitetea viti vya Kata za Themi, Kimandolu, Kaloleni na Elerai ilivyovipoteza baada ya kuwafukuza waliokuwa madiwani wake kwa kosa la kukiuka maagizo ya Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu mwafaka wa umeya.
Ushindi huo unakihakikishia wingi wa wajumbe katika baraza hilo la madiwani hivyo kuwa na fursa kumwondoa madarakani Meya Lyimo. Doita aliahidi kuwa chama hicho kitakaa leo kutoa msimamo kuhusu suala hilo la umeya wa Arusha.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alisema Chadema kisahau suala la kuchagua meya mpya kwani uchaguzi wake ulishapita.
Chatanda, ambaye pia anaingia katika vikao vya Baraza la Madiwani la Arusha kutokana na kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, alisema Chadema kinapaswa kufanya kazi na meya wa sasa.
“Unajua vikao hivi vinaongozwa kwa kanuni, kwa hiyo wingi wao si hoja ya kumvua meya au kulazimisha kupitisha mambo yao,” alisema

Mamia wafurika Manispaa
Wabunge wanne wa Chadema jana waliongoza mamia ya wafuasi wa chama hicho katika shamrashamra ya kuwasindikiza madiwani wanne kwenda kujitambulisha kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.
Hata hivyo, furaha yao ilizimwa na polisi baada ya kumuomba Mbunge Arusha Mjini, Godbless Lema kuwatawanya.
Wabunge wengine walikuwa Mchungaji Israel Natse (Karatu), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) na Grace Mukya (Viti Maalumu) ambao walitokea ofisi za Chadema Mkoa wakiwa na wafuasi wa Chadema wakiwamo vijana wa bodaboda, magari na watembea kwa miguu.
Wakati wabunge hao, wakiwa katika magari yao, Madiwani wanne wa Chadema, walioshinda, Mchungaji Rayson Ngowi (Kimandolu) Edmund Kinabo(Themi), Mhandisi Jeremiah Mpinga (Elerai) na Kessy Lewi (Kaloleni), walikuwa katika gari la wazi.
Hata hivyo, walipofika katika eneo la Halmashauri waliwakuta polisi wakiwa wametanda katika eneo hilo na kuwaruhusu wabunge, madiwani na viongozi pekee kuingia. Agizo la Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Gillis Mrotto kuwataka wafuasi hao kutawanyika halikufanikiwa hadi alipomuomba Lema kuwatawanya wafuasi hao.
Akizungumza na madiwani hao, Mkurugenzi Jiji, Sipora Liana aliwaahidi ushirikiano: “Nawapongeza na naomba tushirikiane katika kazi. Mimi kwa kawaida sipendi ubadhirifu.”

Mbowe ajisalimisha Polisi
Jeshi la Polisi Makao Makuu limemhoji Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa madai kuwa kauli zake alizozitoa baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho ni za uchochezi.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi  ya Upinzani Bungeni alihojiwa kutokana na madai kwamba alisema polisi ndiyo waliohusika na ulipuaji wa bomu Arusha, waliisaidia CCM kwenye uchaguzi na kumtuhumu Rais Jakaya Kikwete kuhusika na mauaji ya Arusha kutokana na kukaa kwake kimya.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.