Baadhi ya wananchi wamekata tamaa kuhusu afya ya shujaa wao huyo na wanapofika nje ya Hospitali ya Medclinic, Pretoria alikolazwa, hushindwa kujizuia na kumwaga machozi. Baadhi yao wamekuwa wakisema ‘wako tayari kwa taarifa mbaya’ kuhusu kiongozi huyo aliyeongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi
Baadhi ya wananchi wamekata tamaa kuhusu afya ya shujaa wao huyo na wanapofika nje ya Hospitali ya Medclinic, Pretoria alikolazwa, hushindwa kujizuia na kumwaga machozi. Baadhi yao wamekuwa wakisema ‘wako tayari kwa taarifa mbaya’ kuhusu kiongozi huyo aliyeongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Mandela (94) ambaye sasa anatajwa kwa jina la Tata
yaani Baba wa Taifa la Afrika Kusini, amelazwa katika hospitali hiyo ya
magonjwa ya moyo na hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya huku taarifa
zikisema ‘anapumua kwa msaada wa mashine’.
Hali hiyo imewachanganya wananchi wa Afrika Kusini
akiwamo Rais Jacob Zuma na familia ya Mandela ambayo tayari imeingia
katika mgogoro mkubwa unaotafsiriwa na baadhi ya watu kwamba ni ‘kuwania
madaraka’ ikiwa kiongozi huyo atafariki dunia.
Usiku wa kuamkia Jumamosi, Mwenyekiti wa Taifa wa
Wanawake wa Chama tawala cha ANC, Baleka Mbete aliongoza maombi ya
kumwombea Mandela kwa wanachama na makada wake waliopo katika Majimbo ya
Cape Town na Eastern Cape huku akisisitiza: “Lazima wananchi wa Afrika
Kusini wafike mahali wamruhusu Mandela ampumzike kwa mapenzi ya Mungu.”
Ukubwa kwa kishindo cha ugonjwa wa Mandela
unaonekana hospitalini Medclinic alikolazwa, katika makazi yake Mtaa wa
Houghton, Barabara ya Laan 12, Johannesburg na makazi yake ya zamani
huko Soweto kwani maeneo hayo yamekuwa na harakati zisizokoma. Watu kwa
mamia, wamekuwa wakifika wakiwa wamebeba mabango, kadi, mishumaa na
maua, wengine katika makundi wakiimba, kusoma maneno ya Mungu na kufanya
sala.
Wapo wanaoifananisha hali iliyopo nje ya kuta za
Medclinic na Houghton na ukuta uliokuwa umezunguka jela alikokuwa
amefungwa katika Kisiwa cha Robben kwa miaka 18 kati ya 27 aliyokaa
gerezani.
“Kama watu walivyokuwa wakikaa nje ya kuta za
Gereza la Robben na kupaza sauti zao kwamba wanataka Mandela aachiwe
huru, ndivyo inavyoonekana leo. Watu wanapaza sauti, wanataka Mandela
kutoka ndani ya kuta za Medclinic,” anasema mmoja wa watu waliokuwa
kwenye lango la kuingia hospitalini hapo.
Kulia mwa lango hilo lililopo Mtaa wa Celliers,
kuna idadi kubwa ya kadi na mabango ambavyo vina ujumbe mbalimbali kwa
ajili ya Mandela, maua na mishumaa ambayo huwashwa na watu wanaofika
sehemu hiyo. Kutokana na hali hiyo, mtaa huo umefungwa pande zote mbili
kwa polisi kuweka vizuizi.
Jumamosi iliyopita, hofu juu ya afya ya Mandela
iliongezeka hasa baada ya kuwapo kwa pilika nyingi Houghton zilizodumu
kwa saa kadhaa, zikiwamo usafi usio wa kawaida uliojumuisha utengenezaji
wa bustani za maua, ufagiaji wa barabara na matengenezo ya njia za
umeme.
Mmoja wa majirani wa Mandela, Jacob Brews alisema harakati hizo si za kawaida na kwamba huenda ‘kuna jambo la ziada’.
Matukio hayo kwa jumla yake yamevivutia vyombo vya
habari vya Afrika Kusini na vya kimataifa ambavyo vimeweka kambi katika
maeneo hayo matatu yanayoonekana kuwa ni muhimu vikisubiri chochote
kitakachotokea.
Vyombo hivyo viliingia katika mgogoro na polisi wa upande mmoja
na familia ya Mandela kwa upande mwingine hasa kutokana na uwepo wake
katika lango kuu la Medclinic.
Wiki iliyopita, polisi wa Pretoria waliwaamuru
waandishi wa habari kuondoa magari na vifaa vyao nje ya hospitali hiyo
kutokana na kile walichokiita ‘sababu za kiusalama,’ amri ambayo hata
hivyo, haikutekelezwa.
Amri hiyo ya polisi ilitanguliwa na kauli ya binti
mkubwa wa Mandela, Makaziwe ambaye alivikosoa vyombo vya habari kwamba
vimeshindwa ‘kuheshimu desturi za Kiafrika pamoja na hisia za familia’
kuhusu ugonjwa wa baba yake.
Hata hivyo, kwa jinsi hali ilivyo, kauli za
viongozi na harakati katika makazi yote ya Mandela, ni vigumu kwa
wanahabari kukaa kimya katika tukio linalomgusa Mandela ambaye ni mtu
maarufu ndani na nje ya Afrika Kusini.
Mgogoro wa ‘mazishi’ ya Mandela
Utata wa afya ya Mandela unachagizwa zaidi na hali
ya sintofahamu inayoendelea ndani ya familia yake kiasi cha kuufikisha
mahakamani mgogoro unaohusishwa na ‘mazishi yake.’
Familia inavutana juu ya ni wapi kiongozi huyo
atazikwa lakini kwa sura ambayo inahusisha watoto wa Mandela ambao
walifariki siku zilizopita na kuzikwa eneo la Qunu kabla ya baadaye
mabaki ya miili yao kuhamishwa kinyemela kwenda eneo la Mvezo ambako ni
makazi ya mjukuu mkubwa wa Mandela alitwaye Mandla.
Idadi kubwa ya wanafamilia wa Mandela wakiongozwa
na binti mkubwa, Makaziwe (60), wanataka mzee wao huyo azikwe Qunu
lakini upande mwingine ukiongozwa na Mandla (38) unataka azikwe Mvezo.
Hoja kubwa na swali ambalo baadhi ya watu wamekuwa
wakiuliza ni kwamba ikiwa Mandela yuko hai ni kwa nini kuwepo mjadala
wa mahali atakapozikwa?
Mkazi mmoja wa Johannesburg, Doroth Nyati alihoji:
“Kama mtu hajafa mnawezaje kukaa kujadili mahali pa kumzika, ndiyo
maana nimekwambia ni dhahiri kwamba Mzee Madiba (Mandela) tayari
amefariki, ila wanatuficha tu.”
Jana, Mahakama Kuu ya Eastern Cape ilitoa uamuzi
kwamba mabaki ya miili ya watoto hao yarejeshwe Qunu ifikapo saa tisa ya
jana hiyohiyo ikimaanisha kwamba Mandla ambaye pia ni mbunge katika
eneo hilo alishindwa kesi.
Amri hiyo ya Jaji Lusindiso Pakade inamaanisha
kwamba marehemu hao sasa watazikwa kwa mara ya tatu; ya kwanza ni wakati
walipofariki dunia kwa nyakati tofauti, pili miili yao ilipohamishwa
kinyemela na Mandla kwenda Mvezo na tatu ni jana wakati wa utekelezaji
wa amri ya mahakama.
Makaburi hayo ya Mandela ni ya mtoto wake kwa kwanza wa kike
Makaziwe aliyefariki dunia akiwa mchanga 1948, mtoto wa pili wa Mandela,
Madiba Thembekile aliyefariki katika ajali ya gari 1969 na baba yake
Mandla aliyefariki 2005 kwa magonjwa yenye uhusiano na Ukimwi.
Mandla alihamisha makaburi hayo kwa siri mwaka
2011 ikiwa ni hatua ya kutaka babu yake; Mzee Mandela akifa naye azikwe
Mvezo ili kuwavutia watalii katika kijiji hicho ambacho yeye ni kiongozi
(chifu) wake.
Mandela aliwahi kunukuliwa akisema kwamba akifa
angependa azikwe pembezoni mwa walipozikwa ndugu zake ambako ni Qunu,
hivyo Mandla alihamisha makaburi hayo ikiwa ni hatua ya kushawishi
kwamba babu yake huyo azikwe Mvezo ambako makaburi hayo yatakuwa.
Kutokana na hali hiyo, Makaziwe aliwaongoza
wanafamilia kufungua kesi dhidi ya Mandla wakiomba Mahakama imwamuru
kurejesha mabaki ya miili aliyoihamisha ‘bila ridhaa ya wanafamilia’.
Uamuzi wa mahakama ni pigo kwa Mandla ambaye pia
anakabiliwa na hatari nyingine mbili; kwanza ni kuanza kwa mkakati wa
kumvua madaraka ya uchifu wa Mvezo, lakini pili ni kufunguliwa kwa
mashtaka ya jinai kwa kosa la kuchezea makaburi.
Ndugu wa kambo wa Mandla, Ndaba alikaririwa
akisema viongozi wa kimila wanakusudia kuchukua hatua ya kumvua madaraka
ndugu yake huyo kutokana na kukiuka miiko, mila za jadi kwa kuhamisha
mabaki ya miili ya wanafamilia waliokuwa wamezikwa Qunu na kuizika upya
Mvezo.
Wakati hayo yakiendelea, polisi wa Western Cape
wamethibitisha kuanza uchunguzi wa tuhuma kwamba Mandla alichezea
makaburi, hatua mbayo inamweka pabaya na kuzidisha mgogoro katika
familia hiyo.
Afya kuzorota
Jumapili Juni 23, mwaka huu, Rais Zuma alitangaza
kwamba afya ya Mandela ni mbaya taarifa ambayo ilizua sintofahamu, hofu
na taharuki kwa wananchi wa Afrika Kusini.
Hofu hiyo ilizidi pale Rais Zuma alipoahirisha
ziara yake ya kwenda Maputo Msumbiji, Juni 26 alikotakiwa kuhudhuria
mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) kutokana na kile alichosema kuwa ni kutokana na afya ya
Mandela.
Siku iliyofuata Juni 27, mwaka huu Zuma katika
taarifa kupiti kwa msemaji wake, Mac Maharaj kwamba hali ya Mandela ina
unafuu na kwamba bado yu mahututi lakini imara. Tangu wakati huo hadi
leo Ikulu ya Pretoria imekuwa ikitoa taarifa kwamba hali ya kiongozi
huyo haijabadilika hadi sasa.
Taarifa rasmi zinasema Mandela anasumbuliwa na
figo ambazo zimeshindwa kufanya kazi, lakini taarifa zaidi zinasema
madaktari wamekuwa wakitibu zaidi magonjwa nyemelezi yanayotokana na
ugonjwa wa msingi.
Hali halisi ya Mandela na kuwa kwake mahututi vimebaki kuwa siri
kubwa ya familia yake, hususan mke wake Graca Machel ambaye anatajwa
kuwa yuko pembeni mwa kitanda alicholazwa Mandela akimuuguza.
Kadhalika, Rais Zuma anatajwa kuwa mmoja wa watu
wenye ‘siri nzito’ kuhusu hali ya Mandela hasa kutokana na taarifa yake
ya Juni 23, mwaka huu na hatua yake ya kuahirisha safari ya Maputo.
Mandela anafikisha umri wa miaka 95 Julai 18, mwaka huu.
Rais Zuma katika taarifa yake Jumatatu wiki hii
aliwakumbusha Waafrika Kusini kwamba wajiandae kusherehekea siku ya
kuzaliwa kwa Mandela ambayo ni maarufu kama “Mandela Day.”
Zuma pia aliwahi kukaririwa akisema “Ni matamanio
ya Waafrika Kusini kusherehekea miaka 95 ya shujaa wao, Madiba kwani
maisha yake yalijaa tuzo za ubinadamu.”
Mkazi mwingine wa Johannesburg, Lebo Boya alisema
shauku waliyonayo wananchi wengi wa Afrika Kusini ni kumwona Mandela
akitimiza umri wa miaka 95, Julai 18 mwaka huu.
“Tumeambiwa anapumua kwa mashine, Serikali iziache
mashine ziendelee kufanya kazi hadi mwezi ujao, tunatamani afikishe
miaka 95 ili tusherehekee siku ya Mandela pamoja naye, baada ya hapo
basi wazitoe maana ni kweli kwamba umri wake ni mkubwa sasa,” alisema
Boya.
Kiongozi kundi la polisi wa Pretoria ambao
walifika Medclinic kumtakia heri Mandela, Mosses Sithebe anasema:
“Anayeweza kuhesabu siku za Madiba ni Mungu pekee na wala siyo mwanadamu
na sasa muda wa Mungu bado haujafika.”
Tofauti na awali, matumaini ya Mandela kufikisha
miaka 95 yanaongezeka hasa kutokana na kupungua kwa kauli za Ikulu
zilizokuwa zikionyesha kwamba yu mahututi kiasi cha kukatisha tamaa.
Ujio wa Obama
Ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama Afrika
Kusini, nayo iliibua hisia mpya kuhusu hatima ya afya Mandela hasa pale
kiongozi huyo wa Marekani alipotangaza kwamba hatamtembelea hospitali
kutokana na matakwa ya familia.
Obama alikuwa amepanga kumwona Mandela lakini Jumamosi asubuhi ilitolewa taarifa kwamba hatafanya hivyo.
Badala yake, alikutana na familia ya Mandela
kufanya kile kilichoelezwa na wasaidizi wake kuwa ni ‘kuwapa ushauri na
kuungana nao katika kumwombea’.
Hata hivyo, katika kikao hicho, Graca hakuweza kuhudhuria na badala yake aliwasiliana na Obama kwa simu.
Hatua hiyo pia ilizua maswali mengi na baadhi ya watu walianza kutilia shaka taarifa kwamba hali ya Madiba ilikuwa ikiimarika.
Maneno yanayotumiwa na Ikulu ya Afrika Kusini
kwamba Mandela yu mahututi lakini imara pia yalizua mjalada na kuwaumiza
vichwa baadhi ya watu wakiwamo wasomi.
Profesa Guy Richards wa Chuo Kikuu, Johannesburg
alionukuliwa na Gazeti la The Citizen la hapa akiikosoa: “Kusema kwamba
Mandela yu mahututi lakini imara, kwa kawaida si kauli ya kitabibu na
nina uhakika hakuna daktari hata mmoja ulimwenguni ambaye aliwahi kutoa
kauli ya aina hii.”
Rais Obama baada ya kukutana na Rais Zuma,
Pretoria alimtakia Mandela heri na kuimarika kwa afya yake... “Tupo naye
kimawazo pamoja na familia yake na wananchi wa Afrika Kusini.”
Wasemavyo wananchi
Mkazi wa Durban, Nomnikelo Ndelu (80) analalamikia
kifungo cha miaka 27 jela alichofungwa Mandela kwamba kina mchango
mkubwa katika kudhoofisha afya yake.
“Hebu ifikirie miaka 27 jela mtu akiwa mbali na
familia yake, watoto, ndugu, jamaa na marafiri zake, ni dhahiri kwamba
hali hii ilimwathiri kiafya na kisaikolojia,” alisema mwanamke huyo na
kuongeza:
“Nasema hivyo kwa sababu hapa kwetu wapo watu wana
umri zaidi ya miaka 100, kama Mama Mbeki (mama yake Rais wa pili
mzalendo, Thabo Mbeki), lakini wako imara kabisa, kwa hiyo adhabu ya
jela ilimwathiri sana, tunamwombea Mungu amjalie apone.”
Rafiki wa Madiba, Mzee Pathekile Holomisa (72)
alisema: “Kweli tunapita katika kipindi kigumu, muda umefika kwa Madiba
kuwa katika hali aliyonayo. Kwa bahati mbaya sisi hatuna tunachoweza
kufanya.”
“Tunaambiwa kwamba anasaidiwa kupumua na mashine,
katika hatua hii Mungu pekee ndiye anayeweza kutuvusha, pengine Zuma ana
siri ya afya yake,” alisema Holomisa huku akilengwa na machozi.
Mbali na wananchi wa Afrika Kusini pia wageni
kutoka nchi mbalimbali wameungana na wenyeji kumtakia heri Madiba. Raia
wa Cameroon aliyejitambulisha kwa jina la Sule Zachari alisema:
“Hatuwezi kuizungumzia Afrika bila kumtaja Mandela na hiyo ndiyo sababu
iliyonisukuma mimi na wenzangu kuona umuhimu wa kufika hapa.”
Mkazi mwingine wa Johannesburg, Faith Sanyani alisema: “Kwetu
sisi Mandela haelezeki. Tunaweza kusema ni baba, mzazi, shujaa… na
mengine mengi …tunampenda, tunamwombea kila siku ili Mola ampe afya
njema.”
Mwanamke huyo alisema viongozi wa sasa wanapaswa
kuzingatia maono ya Mandela hasa katika suala la elimu kwa kuhakikisha
kwamba kila mtoto wa Afrika Kusini anapata elimu bora kwa maisha yake ya
baadaye.
Mwingine, Myst Smith alisema Mandela alijenga
taifa imara lenye umoja na mshikamano; “Nimefika mimi na mke wangu
kuwapa nguvu wanafamilia kwa kumtakia heri Mzee Mandela, tunafahamu umri
wake ni mkubwa lakini bado tunampenda.”
Mkazi wa Pretoria, Lisa Wright alisema
wasingependa kumpoteza Mandela lakini kwa jinsi hali inavyoendelea ni
dhahiri kwamba maradhi yanamzidi nguvu hasa kutokana na umri mkubwa.
“Tutamkumbuka sana Mzee Mandela, amechangia sana
kufuta uhasama baina ya watu weupe na weusi hasa kutokana na moyo wake
wa kusamehe baada ya kutoka gerezani. Suala la siasa za ubaguzi
litageuka historia hasa baada ya kizazi hiki kupita,” alisema Lisa.

Tanzanian Shilling Converter
No comments: