Ads Top

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TAREHE 31 JULAI, 2013

Ndugu wananchi;
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kwa mara nyingine tena kutekeleza utaratibu wetu huu mzuri tuliojiwekea wa Rais kuzungumza na taifa kila  mwisho wa mwezi.

Ndugu Wananchi;
Mwezi Julai, 2013 ulikuwa wa neema kubwa ya wageni kwa nchi yetu wakiwemo watu na viongozi mashuhuri duniani. Natoa shukrani nyingi kwa Watanzania wenzangu kwa jinsi tulivyowapokea wageni wetu zaidi ya 1,700. Wamefurahi kuwepo kwao nchini na wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu.  Wageni wetu wamekuwa wa manufaa makubwa kwa nchi yetu.  Wamesaidia kuitangaza Tanzania duniani na kuendeleza fursa za kukuza utalii, biashara na uwekezaji nchini na kwingineko katika Afrika.
Mkutano wa Smart Partnership
 

Ndugu wananchi;
Wageni wetu wa kwanza ni wale waliokuja kuhudhuria Mkutano waGlobal 2013 Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni hadi 1 Julai, 2013.  Mkutano huo
ulihudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka mabara yote duniani wakiwemo Watanzania.  Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na wakuu wa nchi na Serikali, viongozi wastaafu, wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika na taasisi za kimataifa, makampuni ya ndani na nje, wafanyabiashara, wasomi, asasi za kijamii na watu wa makundi mbalimbali katika jamii.  Makampuni yetu 21 nayo yaliungana na makampuni mengine 28 kutoka nje ya nchi kushiriki kwenye maonesho ya matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika sambamba na mkutano huo.
 

Ndugu Wananchi;
Agenda kuu ya majadiliano ya mwaka huu ilikuwa ni “Matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi Barani Afrika (Leveraging Technology for Africa’s Social-Economic Transformation: The Smart Partnership Way). 

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.