Imetimia miaka 50 tangu Martin Luther King alipotoa hotuba yake ya kihistoria. King aliyekuwa mwanaharakati wa kupigania haki za watu weusi Marekani, alizungumzia ndoto yake ya kuwa na nchi yenye usawa kwa wote
"Nina ndoto kwamba siku moja watoto wangu wanne wataishi kwenye nchi
ambapo hawatatathminiwa kulingana na rangi ya ngozi yao bali kulingana
na tabia yao." Ilikuwa tarehe 28 Agosti mwaka 1963, pale ambapo Martin
Luther King na maelfu ya Wamarekani weusi waliandamana mjini Washington
kudai uhuru na haki sawa ya kupata ajira kwa watu weusi. King alikuwa
miongoni mwa waandalizi wa maandamano hayo na mmoja wa watu waliotoa
hutoba siku hiyo. Hotuba yake ya I have a dream - yaani nina ndoto -
inaelezea mustakabali anaoutamani kwa nchi yake. Alitaka Marekani iwe na
umoja na watu wasibaguliwe kwa sababu ya rangi ya ngozi yao.
"Hatuwezi kuridhika iwapo mtu mweusi kutoka Mississippi hana haki ya
kupiga kura na mtu mweusi anayeishi New York haoni sababu ya kupiga
kura," alisema King katika hotuba yake. Miaka hamsini baadaye, sehemu
fulani ya ndoto ya Martin Luther King imetimia. Kwa mara ya kwanza
Marekani inaongozwa na rais mweusi.
Ubaguzi bado tatizo sugu
Barack Obama ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani
Barack Obama leo ataongoza maadhimisho ya miaka 50 ya hotuba ya
King. Atatoa hotuba kwenye jengo la kumbukumbu ya Lincoln mjini
Washington - mahali pale pale ambapo King alielezea ndoto yake miaka 50
iliyopita.
Obama ameeleza kuwa mafanikio yake kama mwanasiasa mwenye mamlaka
makubwa zaidi Marekani, yamejengwa juu ya misingi ya juhudi za Martin
Luther King na wenzake. Anaamini kwamba asingekuwa rais wa Marekani leo,
kama wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wasingekuwa tayari
kuvumilia vitisho, mateso na hata kufungwa jela.
Hata hivyo, ubaguzi wa rangi bado ni tatizo sugu kwenye baadhi ya maeneo
ya Marekani. Kisa cha kijana Trayvon Martin aliyepigwa risasi na
Mmarekani mwenye ngozi nyeupe aliyehisi kuwa Treyvon ni kibaka kiliweka
wazi kwamba bado yapo maoni potofu juu ya watu weusi. Suala lililozusha
mjadala mkubwa zaidi ni kwamba aliyempiga risasi kijana huyo hakupewa
hukumu yoyote mahakamani.
Sherehe za leo za mjini Washington zitahudhuriwa pia na marais wa zamani
wa Marekani. Bill Clinton na Jimmy Carter ni miongoni mwa wale
watakaotoa hotuba
Kwa habari zaidi bofya hapa..>>>>>
Kwa habari zaidi bofya hapa..>>>>>
No comments: