Ads Top

DC MULEBA AHUSISHWA NA UTAPELI WA ARDHI YA WANANCHI

CHADEMA YANASA SIRI NZITO
 DC Muleba adaiwa kushiriki utapeli.
Kigogo CCM ajichukulia heka 8000.
Na  Antony Sollo  Muleba.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA)  Wilayani Muleba Mkoani Kagera,kimemtuhumu Mkuu wa Wilaya hiyo,Limbres Kipuyo na baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani humo, kujihusisha na utapeli wa ardhi ya wananchi.

Tuhuma hizo dhidi ya DC wa Muleba, zilitolewa na Diwani wa Kata ya Kasharunga, Khalid  Hussein, kuwa anajihusisha na genge linalodaiwa kufanya utapeli katika ofisi mbalimbali kwa ajili ya kujinufaisha katika eneo linalodaiwa kumilikiwa na kada wa CCM katika kijiji cha Kiteme . 

Akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliondaliwa na Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Conchesta Rwamulaza ambaye pia ni Katibu wa chama hicho Mkoa wa Kagera,diwani huyo aliwaeleza wananchi kuwa chama hicho kina dhamira ya dhati ya kuwatumikia  wananchi na kuwaondolea kero na matatizo yao bila kujali itikadi za vyama na dini zao.

Hussein alisema kuwa mgogoro wa ardhi unaofukuta katika kitongoji cha Byantanzi katika kijiji cha Kiteme umesababishwa na baadhi ya makada wa CCM ambao wamejitwalia ardhi ya wananchi ekari 8000 bila kufuata taratibu. 

Diwani huyo alisema baada ya kufuatilia alibaini utapeli huo unaofanywa na  viongozi waandamizi wa Serikali na wa CCM wilayani Muleba, baada ya kunasa barua aliyoandikiwa DC huyo kuhusiana na utapeli huo.

Katika hali ambayo alidai kuwa inathibitisha kuhusika kwa Mkuu huyo wa Wilaya kushiriki kwenye sakata hilo ni kutokana na tamko linaloashiria utekelezaji wa mpango wa utapeli huo kwa kuwaamuru wananchi kuondoka katika maeneo hayo ifikapo tarehe 15 februari 2014,  huku wakiwa wamelima mazao yao ya aina mbalimbali yanayotarajiwa kukomaa siku zijazo.

Alidai kuwa marehemu Edward Barongo akiwa Mkuu wa mkoa wa Kagera wakati huo, alijipatia ardhi yenye ukubwa wa ekari 8000 zaidi ya alizoomba,lakini viongozi wa serikali na chama wakamkingia kifua,akajipatia ardhi hiyo kinyume cha taratibu. 

Wakati DC huyo watuhumiwa,wengine ni viongozi wa CCM na serikali Wilayani Muleba wanatuhumiwa kujihusisha kumkingia kifua kada wa CCM Edward Barongo ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera katika sakata hilo la kujipatia ardhi yenye ukubwa wa ekari 8000 zaidi ya hekari alizoziomba ilidaiwa kwenye mkutano huo na Diwani huyo kuwa, marehemu Barongo aliomba kupatiwa ekari 2000, uombaji ambao hukufuata kanuni na taratibu, hata ushirikishwaji wa wananchi haukuzingatiwa,hivyo kuzua mgogoro mkubwa kati ya familia ya marehemu Edward Barongo na wanakijiji wa Kiteme.


 Naye Mbunge wa Viti  Maalum wa CHADEMA Conchesta Rwamlaza, akizungumza alisema kuwa kufuatia kushamiri kwa migogoro ya ardhi nchini,serikali iwe makini na kuchukua hatua za haraka kutatua migogoro hiyo  na akailaumu CCM na serikali yake.

“Serikali  ya CCM imeshindwa kuwajali wananchi kaya zaidi ya 400 watakaoathirika na zoezi la kuondolewa  katika maeneo yao.

Haya ndiyo matokeo yakushamiri kwa migogoro hii ya ardhi kwa wakubwa kupora ardhi ya wanyonge bila aibu,”alisema Mbunge huyo .

Alisema kuwa  watendaji wa serikari,DC na makada wa CCM pia ni viongozi wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yao ya kazi, hivyo wanapojiingiza katika masuala ya aina hii umma wa Watanzania utakosa haki kwa kuwa mmoja wa wahusika katika kuilinda haki hiyo atakuwa ameingia katika mhimili hatarishi. 
Mbunge huyo amemtaka  Mkuu wa Wilaya ya Muleba kufika katika eneo la mgogoro huo ili kuutatua kuliko kutoa matamko akiwa ofisini na kumuomba Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo  ya Makazi,ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Anna Tibaijuka alishughulikie suala hilo.


 Hata hivyo mbunge huyo ,alionyesha wasiwasi  wake kuwa huenda hata Waziri huyo akashindwa kutatua mgogoro huo kwa kuwa  ni mmoja  wa watuhumiwa wa uporaji wa ardhi, ambapo yeye anadaiwa kuhodhi eneo  linalokadiriwa kufikia ekari zaidi ya 1000  katika kijiji cha Kyamyorwa, huku yakiwepo madai ya mauaji ya watu wanne  wakati wa zoezi la kuwaondoa wananchi waliokuwa wanaishi katika eneo linalodaiwa kumilikiwa na waziri huyo.


 Aidha Viongozi hao wa CHADEMA wilayani humo, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kufuta hati miliki tata za ardhi  na zenye mashaka ili kuondoa hali ya migogoro ya ardhi iliyoshamiri nchini na kusababisha  mauaji ya raia jambo linaloelezwa kuwa  litaitumbukiza  nchi kwenye machafuko.

Tanzania daima lilimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Muleba kupitia simu yake ya Mkononi namba 0767 008 888 simu yake iliita bila kupokelewa ndipo alipotumiwa ujumbe kutaka ufafanuzi juu ya tuhuma hizo lakini hakuweza kujibu chochote.

Naye Mwenyekiti wa  CCM wilaya ya Muleba Muhaji Yusuf Bushako,alipoulizwa kwa simu ya mkononi  na gazeti hili kuhusu kuhusishwa kwakwe kwenye utapeli wa ardhi inayolalamikiwa na Ushirika wa Wafugaji, alidai hata yeye anausikia mgogoro huo na hahusiki kwa lolote.

Mbali na Mwenyekiti huyo wa CCM wa Wilaya ,mtuhumiwa anayedaiwa kuwa msimamizi wa ardhi hiyo ya marehemu Barongo, Hamisi Y Bilamata ,alipotafutwa kupitia simu zake za mkononi hazikuwa hewani (0756 783 625 na 0789 522 180). 

mwisho

 
 Dsc 00490 Diwani kata ya kasharunga akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara katika kijiji cha kiteme
Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA Conchester Mwamlaza akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara katika kijiji cha kiteme  

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.