Serikali yaendelea kuhimiza matumizi ya mashine za EFDs nchini.
Serikali yaendelea kuhimiza matumizi ya mashine za EFDs nchini.
Nashawishika,
natambua na nimejiridhisha kuwa elimu kwa mwanadamu ni mwanga na nuru ya
maisha, mwanga huo ni silaha imara ya kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa
kwa ujumla.
Ujio wa mashine
za kielekroniki za kutolea risiti za kodi (EFDs) nchini ni ukombozi wa ukusanyaji
wa mapato ya nchi ambayo yalikuwa yakipotea na kulinyima taifa mapato kwa maendeleo
yake, tofauti na mfumo wa zamani wa kukusanya mapato kwa risiti za vitabu vya
mauzo.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) iliwahakikishia Wafanyabiashara na Watanzania kwa
ujumla kuwa utaratibu wa kutumia Mashine za EFD ulianzishwa kwa lengo la
kumrahisishia mfanyabiashara utunzaji wa kumbukumbu za biashara za kila siku
pamoja na kuondoa usumbufu wakati wa ukadiriaji wa kodi. Kwa
mantiki hiyo ni wajibu wa Serikali na taasisi inayosimamia mapato ambayo ni TRA
kutoa elimu kwa wateja ambao ni wafanyabiashara wakubwa na wadogo juu ya mfumo
mpya wa ukusanyaji kodi.
Dhamira
ya TRA katika Mpango mkakati wake wa Nne wa kukusanya mapato nchini ni
“Kurahisisha ulipaji wa kodi na kuyafanya maisha yawe bora”. Kwa
dhamira hiyo, TRA imekuwa ikiendesha kampeni za kuwahamasisha walipa kodi na
jamii kwa ujumla umuhimu wa kutoa na kudai risiti sahihi za mashine za
kielekroniki za kutolea risiti za kodi (EFDs).
Kabla
ya kuanza utekelezaji wa mfumo huu, elimu ilitolewa kwa wafanyabiashara na
wananchi kwa ujumla kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na semina
ambazo zilitolewa kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara.
Ni
dhahiri kuwa elimu hiyo bado inaendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ambapo
kuhusu ununuzi wa mashine hizo kwa awamu ya pili, muda wa maandalizi ulisogezwa
hadi Desemba 31, 2013 na taarifa ilitolewa na bado zinaendelea kutolewa kupitia
vyombo vya habari.
Aidha,
Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa
elimu kuhusu matumizi endelevu na faida za Mashine za EFD kwa wafanyabiashara
na wanunuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali za kijamii.
No comments: