Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimesema kuwa hutumia maiti 25 kwa kuwafundishia wanafunzi kila mwaka
Viungo vya Binadamu ambayo hutumika kufundishia madaktari.
Dar es Salaam. Wakati sakata la kuokotwa kwa viungo vya binadamu likiendelea kutikisa nchi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimesema kuwa hutumia maiti 25 kwa kuwafundishia wanafunzi kila mwaka.
Pia chuo hicho hakijawahi kuagiza maiti kutoka nje
ya nchi na kwamba ni mtu mmoja tu aliyewahi kutaka maiti ya mtoto wake
itumike kufundishia.
Kauli hiyo ya MUHAS imekuja siku chache baada ya
Serikali kuamua kuifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba
na Teknolojia (IMTU), baada ya kubaini kasoro kadhaa katika utendaji
wake.
Juzi, Serikali ilifanya ukaguzi wa kushtukiza
IMTU, baada ya hospitali hiyo kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya
viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, jijini Dar es Salaam
mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Hata hivyo, wakati Tume ya Watu 15 iliyoundwa na
Serikali kuchunguza suala hilo ikiendelea na kazi, Mkuu wa Kitengo cha
Anatomy MUHAS, Profesa David Ngassapa amebainisha kuwa chuo hicho
hutumia maiti 25 kwa mwaka.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana,
Ngassapa alisema kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza hutumia maiti 20,
huku madaktari wanaorudi chuoni hapo kwa ajili ya mazoezi wakitumia
maiti tano.
“Sheria ya mwaka 1963 inatutaka baada ya matumizi
tuondoe mwili kwa heshima zote na miongoni mwa vitu ambavyo wanafunzi
wanasisitizwa ni kuhakikisha wanaiheshimu miili hadi hatua za mwisho,”
alisema Ngassapa.
Alieleza kuwa pamoja na sheria kutoa ruhusa ya
kutumia maiti katika mafunzo, bado imeweka vipengele vinavyowataka
madaktari kuiheshimu miili ya watu, hadi hatua ya mwisho.
Ngassapa aliongeza: “Sheria inaruhusu kuhifadhi
mabaki ya miili kwa njia mbili; kuizika na kuichoma moto, pia hospitali
inaweza kuhifadhi mabaki hayo hata kwa miaka mitano.”
Hajawahi kuagiza miili kutoka nje
Akizungumzia utaratibu wa nchi kubadilishana maiti
kwa ajili ya mafunzo, Profesa huyo alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 30
aliyokuwa katika kitengo hicho, hawajawahi kuagiza maiti kutoka nje ya
nchi.
Alisema maiti zilizopo nchini zinatosha
kufundishia wanafunzi wote wa udaktari kwa kuwa siyo Hospitali ya Taifa
Muhimbili(MNH), pekee inayotegemewa kutoa miili hiyo.
Alisema kuwa siku za nyuma, Serikali ilikuwa ikiagiza mifupa
kutoka nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo, lakini sasa kila kitu
kinafanyika hapa nchini.
Ngassapa alisema kuwa miili iliyoharibika kwa
ajali au magonjwa haifai kutumiwa kwa kuwa mwanafunzi anatakiwa
kujifunza kwenye mwili uliokamilika.
Amkumbuka mtu aliyetoa maiti ya binti yake
Alisema kuwa historia ya Tanzania inaonyesha kuwa
ni mtu mmoja pekee ndiye aliwahi kujitolea maiti ya binti yake ili
itumike kufundishia.
“Alijitolea kwa kuwa binti yake huyo alianza
kuugua akiwa na umri wa miaka miwili hadi alipofikisha miaka 12, muda
mwingi akiwa amelazwa hospitalini hapa,” alisema.
“Alipofariki dunia mzazi alisema mtoto huyo ni wa
hospitali na anamtoa kwa ajili ya matumizi ya hapa. Ibada ya mazishi
ilifanyika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema Ngassapa.
Alifafanua kuwa hata baada ya kukabidhiwa maiti
hiyo, waliendelea kumhifadhi kwa miaka minne, hadi walipojiridhisha kuwa
wazazi hawatabadilisha mawazo.
Sheria inayotumika
Mkuu huyo wa kitengo kinachoshughulikia mwili na
viungo vyake, alisema kuwa sheria ya Serikali ya mwaka 1963, ndiyo
inayoruhusu chuo chochote cha afya kuchukua mwili kama umekaa katika
chumba cha kuhifadhia maiti kwa siku 14 bila ndugu kujitokeza.
Ngassapa alifafanua kuwa licha ya sheria kuwataka
kuchukua mwili uliokaa katika kipindi hicho, chuo huuhifadhi mwili huo
kwa siku 30, ili kujiridhisha pasipo shaka kwamba hakuna ndugu
anayejitokeza kuuchukua.
Alibainisha kuwa baada ya hapo, huuweka dawa ili
usiharibike, kisha huuacha kwa wiki mbili au tatu zaidi wakisubiri kama
ndugu wanaweza kujitokeza.
“Inapothibitika kuwa hakuna anayejitokeza, chuo huuchukua na kuutumia kwenye mafunzo,” alisema.
Alifafanua kuwa sheria pia inakitaka Kitengo cha Anatomy
kuandika barua kwa mkuu wa chuo na Mahakama Kuu, kutaarifu kuwa
wamechukua mwili kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk
Primus Saidia juzi aliliambia gazeti hili kuwa miili ni mali ya Serikali
na kwamba chochote kinachofanyika kwa binadamu lazima kifuate sheria
zilizowekwa na Serikali.
Pia alisema kwamba sheria inaruhusu nchi
kubadilishana maiti, lakini hana uhakika kama jambo hilo limewahi
kufanyika nchini, ingawa ana uhakika kuwa haiwezekani hospitali zikakosa
maiti za kufundishia.
No comments: