Ads Top

Serikali kutoa Ruzuku kwa Vikundi vya Wavuvi


Na Antony Sollo Busega.
Julai 26 2014.
Serikali itaanza kutoa Ruzuku kwa wavuvi watakaokuwa katika vikundi vilivyosajiliwa, ambapo fedha hizo zitatolewa kwa ajili ya kununua zana za uvuvi ikiwamo mitumbwi ya kisasa pamoja na nyavu ili kuondoa tatizo la uvuvi haramu na kuwafanya wananchi wafanye kazi zao kihalali na kwa uhuru.

Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Busega ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dk Titus Kamani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika julai  21 mwaka huu katika kijiji cha Ijitu kata ya Kiloleli.

Akiwahutubia wananchi waliokuwa na hamu ya kujua ujio wa Mbunge wao Dk Kamani aliwaomba wananchi kuchangamkia fursa hii ili waweze kujiajili ,lakini pia waweze kujipatia mahitaji yao na kupambana na umaskini,
Alisema kuwa Serikali itatoa ruzuku ya asilimia arobaini huku wanakikundi wa ushirika wa wavuvi hao wakichangia asilimia sitini “ jamani ndugu zangu wananchi hii ni fursa iliyotolewa na Serikali ili muweze kupata ruzuku kwa ajili ya kununua zana za kisasa ili muondokane na zana ambazo zinaingizwa isivyo halali maana mtakuwa mnafanya kazi zenu mkiwa huru.

Akijibu swali aliloulizwa juu ya kulipa mapato mara mbili au zaidi wakati tayari alishakata leseni Dk Kamani aliwaambia tatizo hilo amelirithi toka kwa watangulizi wake akiwemo Waziri John Pombe Magufuli na kuahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo ili kuondoa urasimu huo
 “ ndugu zangu naomba muelewe,kila halmashauri nchini ina vyanzo vyake vya mapato,sasa huwezi kukata leseni Bunda ukaenda kufanya kazi mpaka Ukerewe kwa leseni ileilie, na suala hili limetuumiza sana kichwa hivyo Serikali inajitahidi kulitafutia ufumbuzi mapema iwezekanavyo”alisema Dk Kamani. 

Waziri Dk Kamani alitoa msaada wa baiskeli mbili za magurudumu manne kwa ajili ya walemavu, ili ziweze kuwasaidia kwenda sehemu mbalimbali na baada ya hapo aliwashukuru wananchi kwa kumchagua na kuwaomba ushirikiano ili waweze kuleta maendeleo jimboni humo.alikemea vitendo vya majungu na kusema kuwa kipindi hiki ni cha kazi maneno hayataweza kuleta maendeleo

Natambua kuwa walemavu nao ni binadamu kama ilivyo kwa binadamu wengine,ninatoa baiskeli hizi ambazo nimezipata kutoka kwa marafiki zangu wa shirika la Desk and Chair kwa ajili ya walemavu waliomo katika jimbo letu hivyo naomba mzitumie vizuri”.alisema Dk Kamani.
Mwisho.  

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.