Ads Top

Dk Kamani apata mwarobaini wa mauaji ya walemevu wa ngozi albino


Na Antony Sollo  Busega
July 22.2014

MAUAJI ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) huenda yakabaki historia wilayani Busega,hii ni kufuatia juhudi zinazofanywana Mbunge wa jimbo hilo, Dk. Titus Kamani, kuanzisha ujenzi wa kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa Ngozi ikiwa ni pamoja na shule yao.

Hayo yamejiri kufuatia ziara ya Mbunge wa Jimbo la Busega Dk. Titus Kamani iliyoanza mapema mwezi huu ambapo aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari ujenzi wa kituo hicho umeshaanza katika Kijiji cha Lukungu, Kata ya Lamadi, jimboni hapa.

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Lamadi, Dk. Kamani alisema  kwamba,kituo hicho kitagharimu Sh bilioni 1.5, na kwamba kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuhudumia watoto zaidi ya 100 kwa wakati mmoja.

Dk. Kamani ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi alimshukuru Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kumuunga mkono Katika ujenzi huo kwa kuchangia Sh milioni tano.

Dk Kamani Alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni miongoni mwa mambo ambayo amedhamiria kuyatekeleza katika Jimbo la Busega kwa manufaa ya jamii nzima kwani jamii imezungukwa na makundi mbalimbali wakiwamo walemavu wa ngozi,wasioona nk huku kila kundi likihitaji huduma na kwamba ameguswa kusaidia makundi hayo kwa moyo wa dhati.

“Albino ni kundi maalum la watu ambao wamekuwa wakisahaulika katika jamii, ninamshukuru Waziri Mkuu ambaye pia ni mlezi wa walemavu hao kuguswa na jitihada zangu na kuniunga mkono kwa kunichangia kiasi hicho cha fedha,” alisema Dk. Kamani.

Aliomba taasisi mbalimbali na watu wenye uwezo kumuunga mkono kwa hali na mali Katika kulinda na kuokoa maisha ya walemavu hao.

Mratibu wa Kituo hicho, Moody Gimonge, alisema kitakapokamilika kitaanza kuchukua walemavu wa wilayani Busega wanaolelewa katika vituo vya Shule ya Msingi Mwisenge mkoani Mara, Buhangija mkoani Shinyanga na sehemu nyingineza wilayani.

“Tuna walemavu wa ngozi 22 wanaolelewa Mwisenge na wengine zaidi ya hao wako Buhangija, pindi kituo hiki kitakapokamilika tutaanza kwa kuwachukua kwanza hao walioko katika vituo hivyo ili vipate fursa ya kusaidia watoto wengine,” alisema.

Alieleza kusikitishwa kwake na watu wanaoanzisha vituo vya aina hiyo kwa
ajili ya maslahi kujipatia yao binafsi badala ya kuwa na dhamira ya dhati
ya kuwasaidia walemavu hao kama ambavyo Dk. Kamani ameonesha dhamira ya kweli kwa vitendo.

Mwisho

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.