Tamko Rasmi la Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM Ndugu Paul Makonda
Katibu wa Hamasa na
Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Paul
Makonda akiwa anazungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa sekretarieti
uliopo Ofisi za makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi maarufu kama white house,
mjini Dodoma leo
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
“Demokrasia
bila mipaka ni ukichaa na demokrasia bila nidhamu ni uwendawazimu” Mwl Jk
Nyerere
Ndugu zangu Watanzania, naomba mfahamu
kuwa miongoni mwa wajumbe wote wa bunge la katiba takriban 600, wajumbe
waliofanya maamuzi haramu ya kugomea ni 79 ambao ni pungufu ya asilimia 15% ya
wajumbe wote, na sio kweli kuwa wao pekee ndio wenye tafsir sahihi ya rasimu.
Wajumbe wa makundi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa vyama vyote vya siasa
takriban 18 kati ya 22 bado wamo kwenye bunge, kati ya wajumbe wa kundi la 201
walioasi ni 15 ambapo bara ni 9 na zanzibar 6 lakini pia katika wanaojiita
UKAWA wapo wabunge ambao wameendelea kurudi bungeni kwa kuzingatia maslahi
mapana ya Taifa.
Takwimu hizi zinatuthibitishia kuwa UKAWA ni kikundi kidogo cha watu waliojipanga kuvuruga AMANI ya nchi, watu ambao hawataki KATIBA wala hawataki MUUNGANO.
Takwimu hizi zinatuthibitishia kuwa UKAWA ni kikundi kidogo cha watu waliojipanga kuvuruga AMANI ya nchi, watu ambao hawataki KATIBA wala hawataki MUUNGANO.
Ndugu zangu watanzania, naomba leo niwape
picha na kilichopo nyuma ya pazia ya kikundi hiki kiitwacho ukawa ambacho
kinaratibiwa na viongozi wachache na maslahi yake kujulikana kwa wachache zaidi
tena yaliyojikita katika misingi ya kibinafsi.
Mfano, ndoa ya CUF na CHADEMA
inayopelekea NCCR mageuzi kuwa bendera fuata upepo imejengwa katika misingi ya
kuvunja muungano, kwa makubaliano kuwa CUF kubaki na Zanzibar na CHADEMA kubaki
na Tanganyika. CUF inataka inufaike na mkakati dhalimu wa kunyonya rasilimali
za wazanzibar yakiwemo mafuta bila kushurutishwa na sheria za muungano kwani
wakiamini kubaki na muungano imara CUF na viongozi hao wachache katika chama
hicho wanakosa fursa za kupora rasilimali za wazanzibar. Ikubumbukwe Muungano
ndio unalinda mipaka na usalama wa raia katika kujiendeleza na kujinufaisha
bila ubaguzi wa kikundi cha watu wachache ambacho kinaenda kinyume na utawala
wa sheria.
Ikumbukwe kuwa rasimu ya CUF walioipeleka
kwa Mhe. Raisi mwaka 2011, mapendekezo yao ni tofauti na madai yao sasa ya
serikali 3, hapa inatosha kutupa picha kuwa nia yao ni kuvunja muungano ili
watuache katika mfarakano kama nchi nyingine zinazoteseka kwa sababu ya
wanasiasa uchwara.
Ifahamike ajenda ya CHADEMA ni kuvunja
muungano ndio maana CHADEMA hawahangaiki kuimarisha chama Zanzibar, nia yao ni
kubaki na Tanganyika ili waigawe Tanganyika katika vipande vipande kwa lugha ya
majimbo ili adhima yao ya ukanda na ukabila itimie. Moja ya kanda yao ambayo
wametangaza katika kanda 8 walizo nazo ni Kilimanjaro, tanga, arusha na
manyara. CHADEMA ina amini kanda hii inajitosheleza kwani ina bandari,bunga za
wanyama,madini, milima . Na hii imepelekea mbunge mmoja wapo wa CHADEMA kulazimika
kusema kaskazini ni nchi huru huku mwenyekiti wao Mbowe akiendelea kudai mapato
ya mlima Kilimanjaro yabaki Kilimanjaro.
Katika kipindi hiki ambacho wenzetu
wamegomea bunge la katiba ambalo lipo kisheria na madai yao yakibadilika kila
kunapokucha tena yakiwa na upotoshaji mkubwa kwa kufanya siasa chafu ili mradi
watimize azma ya kuisambaratisha Tanzania wakiwa makuwadi wazuri wa soko huria.
Ukihoji leo sababu iliyowafanya watoke bungeni ni tofauti kabisa na sababu
waliyoitoa siku wanatoka bungeni, eti msingi wao mkuu wao ni watetezi wa
wananchi. Lakini tumesikia katika vyombo mbalimbali wananchi hao wakiwaasa na
wakiwataka warejee bungeni ili kukamilisha kazi ya kisheria na tumaini la
watanzania la kuwapatia katiba mpya.
UKAWA hawa bila haya wamekataa. Swali..?
wanamtumikia nani. Mpaka sasa imepelekea wananchi hao wanaosema wanawawakilisha
wameamua wenyewe kuja Dodoma kuendelea kusema kero zao na shida zao ili katiba
hii iweze kutoa majawabu, mfano tumeshuhudia makundi ya wakulima, jukwaa la
wahariri wa vyombo vya habari, wafugaji na makundi kadha wa kadha yameendelea
kutiririka Dodoma. Hii ni picha tosha kuwa UKAWA hawawatumikii watanzania na
wameamua kuwahadaa watanzania kwa mgongo wa kuwatetea huku ajenda yao ikiwa
maslahi binafsi.
Ndugu zangu watanzania tunapowaunga mkono
watu wanaoendelea kuligomea bunge la katiba wakati tunajua nchi inaongozwa kwa
utawala wa sheria, na wao ndio wamevunja sheria, tujue kabisa kuwa tunaenda
kinyume na utawala bora, ambao umejengwa kwenye msingi wa sheria na demokrasia.
Msingi wa demokrasia sio kususa baada ya kushindwa hoja, UKAWA hawataki hoja za
wengine na wanalazimisha hoja zao pekee ndizo zikubalike kinyume na msingi wa
demokrasia. Na bila haya watu hao wasiojua demokrasia wameendelea kuwashawishi
watanzania waingie barabarani huku wakijua kuwa Katiba haipatikani barabarani
kama wanahoja kwanini wanaikimbia Dodoma..? Mchakato huu ulianza kisheria na
utahitimishwa kisheria, sio matamko ya makuwadi wa soko huria.
Miongoni mwa madai yao matatu, (i) Rais avunje
bunge (2) kinachojadiliwa Dodoma sio rasimu ya warioba (3) Serikali tatu ndio
maendeleo
Kwa ujumla wake, UKAWA wanajua mamlaka ya
Rais kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011, sura namba 83
imempa Rais mamlaka ya kuunda tume, kuchagua wajumbe 201, kutangaza na kuitisha
bunge na kuzindua bunge la katiba, kupokea katiba inayopendekezwa na kuitangaza
kwenye gazeti la serikali.,kwanini wanataka kumlazimisha Rais kuvunja Sheria
kwani hayo niliyoyataja ndio ambayo Rais anayo mamlaka ya kisheria kuyafanya
katika mchakato huu wa Bunge la Katiba, na ndio maana hata wale wajumbe
aliowateua ambao wamegomea Rais hajawatengua.
,kinachojadiliwa bungeni ni Rasimu
ya jaji warioba na kiko wazi, kwa sababu msingi mkuu wa majadiliano ni Rasimu
inayotokana na tume tena kwa mujibu wa Sura namba 83 kifungu cha sheria namba
25/26 na kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu namba 33 (8). Wanajua mamlaka ya
bunge na waliohusika kutengeneza sheria hizi pamoja na kanuni waache kuwahadaa
watanzania.
Jambo la mwisho lenye kusikitisha zaidi ni
kung’ang’ania Serikali tatu kana kwamba ndio kilio kikubwa cha watanzania,
naomba niulize swali kati ya Muungano na migogoro ya ardhi ni jambo lipi
limepoteza maisha ya watanzania wengi na ambalo tunatakiwa kulifanyia kazi ili
watanzania wasiendelee kumwaga damu. Kati ya tatizo la ajira na muungano, kati
ya afya na muungano, kati ya maji salama na safi na muungano, kati ya elimu
bora na muungano, kati ya haki za binadamu na muungano eti watu hawa wanaojiita
ukawa kwao muhimu muungano kuliko chochote kile.Watanzania naomba tupime kama ni kweli kuwa hawa
ni watetezi wetu au ni makuwadi wa soko huria.
Kwa
niaba ya watanzania wazalendo, napenda kuiomba serikali kupitia vyombo vyake
vya ulinzi na usalama kuwatupia UKAWA jicho la pekee katika kuangalia na
kufuatilia kwa ukaribu zaidi nyendo za UKAWA na hata kutuambia ni nani wako
nyuma yao kiasi cha kuwa na kiburi cha kupindukia. Wito wa watanzania kwa
vyombo vya ulinzi na usalama ni kuwa amani, umoja na uhai wa nchi hii uko
mikononi mwao, kwani nia ya UKAWA sio nzuri kwa mustakabali wa taifa hili na
lazima wakumbuke USIPOZIBA UFA UTAJENGA UKUTA na pia MAJUTO NI MJUKUU NA HUJA
BAADAE. UKAWA wanataka kutengeneza Misri, Afrika ya Kati, Libya, Syria, Sudani
Kusini nyingine hapa Tanzania.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Katibu , idara ya Hamasa na chipukizi
Jumuia ya vijana chama cha mapinduzi
(UVCCM)
No comments: