Ads Top

TAARIFA YA CHADEMA KUHUSU KUSISITIZA KUFANYA MAANDAMANO

  Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akimkaribisha Kigaila kuzungumza na wanahabari.
  Mwanasheria wa Chadema, John Malya akifafanua baadhi ya vipengere vya sheria kuhusu ruhusa ya kufanya maandamano.
  Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila akionesha barua za kuomba vibali vya kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali nchini.
  Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari.
  Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam, kuhusu maandamano ya chama hicho yatakayoanza kesho nchini kote kupinga Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma. Kulia ni Kada wa Chadema, Aron Mashuve na Mwanasheria wa chama hicho, John Malya.
  Mwanasheria wa Chadema, John Malya akiwa na kada wa chama hicho, Aron Mashuve. Imeandaliwa na mtandao wa habari za jamii.com-simu namba 0712-727062
 
Ndugu waandishi wa habari

Tunapenda kuanza mkutano huu kwa kutoa salaam za amani kwa Watanzania  wote, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Amani Kimataifa,  ambayo huadhimiswa Septemba 21, ya kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu  kama ilivyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ni  'The Right Of People's to Peace'. 


Tumekutana nanyi hapa siku hii mahsusi ya kuazimisha amani kimataifa,  tukiwa na ujumbe maalum kwa Watanzania kuwaeleza namna ambavyo  watawala wa Serikali ya CCM, wanavyohatarisha amani ya nchi yetu kwa  kuvunja haki za msingi za Watanzania huku pia wakififisha matumaini ya  wananchi. 


Tunataja maneno hayo mawili HAKI na MATUMAINI kwa makusudi kabisa kwa  sababu hayo ndiyo ndiyo msingi wa amani na utulivu wa kweli mahali  katika taifa ambalo linajali na kuzingatia maendeleo na ustawi wa  wananchi wake. 


Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake kali  kuonesha namna ambavyo walioko madarakani wanahatarisha amani na  utulivu wan chi, aliwahi kusema kuwa ni hatari sana iwapo wananchi  wakipoteza matumaini kwa viongozi wao huku pia hawaoni haki  ikitendeka. Mwalimu alikwenda mbali na kusema Watanzania watakuwa
'wapumbavu' wakikubali viongozi waendelee kwenda kinyume na maslahi au  matakwa ya wananchi wao. 


Kama wananchi hawapati haki na wanapoteza matumaini na viongozi wao,  hakuwezi kuwa na amani na utulivu. Itabaki amani inayoimbwa na CCM  majukwaani wakati haki za msingi ndani ya nchi zikiminywa na kukiukwa. 


Ni vigumu kuwa na amani au utulivu wa dhati iwapo haki za kisiasa (mf;  kukutana, kuandamana n.k), haki za kiuchumi (kuwa na maisha bora) haki  za kijamii (kupata elimu bora na bure, matibabu bora na bure, maji  safi na salama), n,k, huku ufisadi na ubadhirifu wa mali na rasilimali  za umma, ukiongezeka na UWAJIBIKAJI ukiwekwa kapuni. 


Ndugu waandisi wa habari, ninyi pia ni mashahidi wa namna ambavyo  utawala huu wa CCM ambao umeshapoteza kabisa ushawishi wa kisiasa kwa  wananchi, umezidi kuminya haki ya kupata taarifa huku pia ikiendelea  kutumia sheria za kikoloni kuminya uhuru wa habari nchini. 


Hali hii imewafanya waandishi makini wanaozingatia miiko na maadili ya  taaluma yao, kuwa wahanga wa vitendo viovu vya watawala, wakiwemo  askari polisi kama ilivyodhihirika hivi karibuni mbele kabisa ya  milango ya wakubwa wa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani. 

Ikiwa ni mwendelezo wa matukio ya namna hiyo ambayo yalifikia hatua ya  juu pale askari walipomuua kikatili Mwandishi Daudi Mwangosi, Septemba  2, 2012, huko Nyololo, Iringa 


Tungependa pia kutumia nafasi hii Siku ya Amani Kimataifa, kuwatia  moyo ninyi waandishi wa habari kuendelea kutekeleza wajibu wenu wa  kijamii (social responsible journalism) kwa kuzingatia maslahi na  matakwa ya wananchi, tukiungana na Watanzania wengine wanaothamini na  kutambua uhuru wa habari kama moja ya mihimili muhimu katika ujenzi wa   demokrasia na hatimaye maendeleo na ustawi wa wananchi wote. 


CHADEMA inaungana na Watanzania wote ambao wako sambamba nanyi katika  kuheshimu wajibu, majukumu na taaluma yenu, hususan katika kipindi  hiki ambapo vyombo vya habari na waandishi wanaojipambanua kwa umakini  wa kuwatumikia Watanzania, kama ilivyo kwa watu wengine makini kwenye  makundi mbalimbali ya kijamii, wanalazimika kupitia kwenye 'bonde la kifo' linalotengenezwa na watawala waliopoteza uhalali na ushawishi wa
kisiasa, wakikabiliwa na hofu ya anguko kubwa kutoka madarakani. 


Katika siku hii ya leo, tukiunganisha na mfululizo wa matukio ya  vyombo vya dola kugeuka kuwa adui wa raia na mali zao, ikiwemo  kushambulia waandishi wakiwa kazini, tunao wajibu wa kuwataka watawala  kutambua wajibu wa kitaaluma na uhuru wa waandishi wa habari kwa ajili  ya kuweka misingi ya amani na utulivu unaotokana na haki na matumaini. 

CHADEMA ni moja ya wadau wa habari ambao wameweka saini kukubaliana na  Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji  (DEFRI), ambalo iwapo Serikali ya CCM ingekuwa imelikubali,  kulithamini na kulizingatia, leo hii lingeweza kuwa moja ya nyaraka  zinazotutambulisha duniani kama taifa linalotukuza haki, matumaini,
uhuru na uwajibikaji kwa ajili ya wananchi. 


Tumeomba kukutana nanyi leo ili tuweze kutoa kauli juu ya Siku ya  Amani Kimataifa, sambamba na yanayoendelea kuhusu Azimio la Mkutano  Mkuu wa Chama; kufanya maandamano na migomo ya amani nchi nzima isiyo  na ukomo kupinga ufisadi unaofanywa na Bunge Maalum la Katiba, kupinga  uchakachuaji wa maoni ya wananchi unaoendelea kufanyika mjini Dodoma  na uvunjifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. 


Katika muktadha huo wa Siku ya Amani Kimataifa, tungependa kuelezea  uhalali wa maandamano na migomo hiyo ya amani kama ifuatavyo; 


Maandamano; Haki na Wajibu wa kikatiba; 


Kwanza kabisa, Watanzania wote wanawajibika kwa mujibu wa Katiba ya
Nchi, Ibara ya 27 (1)-(2), ambayo inasema; 


"(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya  Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa  pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine. (2) Watu  wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya  pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha  uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya  baadaye ya taifa lao." 


Azimio la Mkutano Mkuu wa Chama la kufanya maandamano na migomo ya  amani nchi nzima lilizingatia takwa hili la Katiba ya Nchi.  Kinachoendelea huko Dodoma ni uharibifu na ubadhirifu wa mali na  rasilimali za umma. Ule ni ufisadi. Kwa sababu Katiba Mpya
haitapatikana kwa namna ile bunge linavyoendelea Dodoma. Hata Rais  Jakaya Kikwete amekubali hilo mbele ya viongozi wenzake. Ni wajibu  wetu sote kupinga Bunge la Katiba kuendelea. 


Pamoja na ubovu wake ilionao, Katiba ya Nchi, katika Ibara ya 20 (1),  imetoa haki kwa mtu au watu kuwa huru kukutana, kuchanganyika na  kushirikiana na watu wengine kutoa mawazo hadharani. 


Mikutano ya hadhara, migomo na maandamano hayo ya amani ya CHADEMA ni
sehemu ya mikusanyiko, ambayo ni haki ya kikatiba ya kila mtu au  kikundi cha watu.


Mbali ya haki hiyo kuwekwa bayana kwenye Katiba ya nchi, upo utaratibu  ambao umewekwa wa kuhakikisha haki hiyo inatekelezwa na wanayoitaka  katika kuhakikisha wanatoa mawazo yao kupitia mikusanyiko ya aina  mbalimbali. 


Utaratibu ambao unavihusu vyama vya siasa mahsusi umefafanuliwa vizuri  kisheria, kupitia Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992, kifungu cha  11 ambacho kinasema hivi; 


"11. --(1) Every party which has been provisionally or fully registered  shall be entitled-a) to hold and address public meetings in any area  in the United Republic after giving notification to the police officer  in-charge of the area concerned for purposes of publicizing itself and
soliciting for membership;" 


"...(4) When a political party is desirous of holding a meeting or  procession in any open public place in any area it shall, not less  than forty eight hours before the meeting, submit a written
notification of its impending to the police officer in charge of the  area in which the meeting is to take place is situated. 


(5) The written notification referred to in subsection (4) shall  specify--a) the name of the political party submitting the  notification; b) the place in and time at which the meeting is to take  place; c) the agenda or purpose in general of the meeting;". 


Ndugu waandishi wa habari

Vipo vifungu vingine kwenye Police and Auxiliary Service Act ambavyo  navyo vinaweka utaratibu wa kisheria kwa makundi mbalimbali ya  kijamii, vikiwemo vyama vya siasa, kutekeleza haki hiyo, ambapo  kifungu cha 43 (1) kinasema; 


"Any person who is desirous of convening, collecting, forming or  organizing any assembly or procession in any public place shall, not  less than forty eight hours before the time when the assembly or  procession is scheduled to take place, submit a written notification
of his impending assembly or procession to the police officer in  charge of the area specifying; (a) the place and time which the  meeting is to take place, (b) the purpose in general of the meeting;  and (c) such other particulars as the Minister may from time to time,
by notice published in the Gazette, specify." 


Taarifa zote za CHADEMA ambazo zimetolewa kwa ajili ya mikutano,  migomo na maandamano ya amani kwa Jeshi la Polisi katika maeneo  mbalimbali kwenye ngazi za majimbo, wilaya na mikoa zimezingatia  wajibu wa kikatiba, matakwa ya kisheria. 


Wakati watu wetu wakitimiza matakwa ya kisheria, Jeshi la Polisi  kupitia barua mbalimbali, mbali ya kukiri kuwa maandamano yetu ni ya  amani, limekuwa likitoa amri ambazo hazina msingi wa kisheria kuzuia  mikutano na maandamano hayo. Raia mtiifu kwa nchi yake hawezi kutii  amri isiyotokana na msingi wa kisheria. Kwa sababu ni batili. 


Hivyo tunapenda kuwataarifu kuwa maandamano yetu ya kupinga ufisadi,
uchakachuaji kwenye mchakato wa Katiba na uvunjwaji wa Sheria ya  Mabadiliko ya Katiba yako pale pale kuanzia kesho Jumatatu, Septemba  22 na kuendelea itakuwa ni wiki ya maandamano. 


Ni vyema utaratibu huu tukaueleza na ueleweke vyema kwa sababu Jeshi  la Polisi nchini linatumia mamlaka lisilokuwa kikatiba wala kisheria,  kuzuia haki ya kikatiba ya wananchi kukusanyika na kuandamana dhidi ya  jambo ambalo linafanyika kinyume na maslahi au matakwa ya wananchi.


Wanachama wetu katika maeneo mbalimbali kama ambavyo tutawaonesha kwa
ushahidi hapa wa barua, wamefuata utaratibu huo wa kisheria ambao unawataka kuwasilisha barua za TAARIFA kwa Jeshi la Polisi,  kuwataarifu polisi kuhusu kusudio la kufanya mkutano au kuandamana. 


Tunaomba kusisitiza kuwa barua hizo ni za kutoa TAARIFA. Si kuomba KIBALI.

Pamoja na wanachama wetu katika maeneo mbalimbali ya nchi kutoa  taarifa kwa Jeshi la Polisi, bado wamekataliwa kutekeleza wajibu na  haki yao hiyo ya kikatiba kwa kisingizio cha kunyimwa KIBALI. 


Neno KIBALI, limekuwa likitumiwa na Jeshi la Polisi katika hali ile  ile ya matumizi mabovu ya madaraka na mamlaka wasiyokuwa nayo kisheria  wala kikatiba. Hakuna mahali popote kisheria ambapo wananchi au chama  cha siasa kinatakiwa kuomba kibali ili waweze kukusanyika au  kuandamana.


Jambo la pili ambalo tungependa kuzungumza hapa ni kusisitiza kuwa  tunaendelea na uratibu wa maandamano ya nchi nzima, ambayo sasa  tumepanga yaendelee kuanzia kesho Jumatatu. 


Tunafanya hivyo kwa sababu ni wajibu na haki yetu ya kikatiba, baada  ya kuwa tumefuata utaratibu wa kisheria ambao ni kutoa taarifa kwa  mamlaka husika. Tunapenda kuwaambia Jeshi la Polisi kuwa matumizi ya  neon hilo 'kibali' ni ubatili kisheria na si sahihi kutii amri
isiyokuwa na msingi katika sheria. 


Kulaani kupigwa waandishi wa habari

Tunatumia fursa hii, kwa mara nyingine tena, kutoa kauli ya chama  kulaani kwa nguvu zote kitendo cha Jeshi la Polisi kupiga waandishi wa  habari waliokuwa wakitimiza wajibu wao siku ya Alhamis wakati  Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe alipoitikia wito wa jeshi
hilo. 


Kitendo hicho cha askari wa Jeshi la Polisi kuwashushia kipigo  waandishi wa habari mbele ya macho, masikio na milango ya wakubwa wa  jeshi hilo na Wizara ya Mambo ya Ndani, ni wazi kimetupeleka hata  nyingine katika kutaka mabadiliko makubwa ya kimfumo na kisheria
kuhusu utendaji na usimamizi wa Jeshi la Polisi nchini. 


Kitendo hicho kinachopaswa kulaaniwa na kila mpenda demokrasia na  maendeleo, anayeamini katika uhuru wa maoni na fikra mbadala,  kilitokea siku moja tu baada ya Makamu wa Rais (mkuu wa nchi kwa  wakati huu) kuwa amekutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini  pamoja na Vyombo vya Dola, akitoa wito kuwepo na maelewano kati ya
pande hizo mbili wakati wa utekelezajiwa majukumu yao. 


Tangu juzi tumemtaka Makamu wa Rais kujitokeza hadharani kuuambia umma  wa Watanzania kama alitoa maelekezo mengine baada ya kuachana na  wanahabari, ambayo ndiyo yaliyotekelezwa na askari siku iliyofuata! 


Tumemtaka pia IGP Ernest Mangu kutoa kauli ya hatua zipi amechukua
hadi sasa dhidi ya matukio mbalimbali ya askari polisi kushambulia
waandishi wakiwa kazini, huku tukimkumbusha tukio la kuuwawa kikatili
kwa Daudi Mwangosi katika mazingira yale yale kama ya juzi Makao Makuu
ya Polisi. 


Ikiwa ni sehemu ya hatua za haraka, tunawashauri vyombo vya habari  nchini vikiwa kama mhimili wa nne, kuchukua hatua zifuatazo katika  kuupigania mhimili huo upate hadhi na heshima unayostahili; 


1. Kufuatilia na kuhakikisha kwa hatua za kinidhamu zimechukuliwa  dhidi ya wale wote waliohusika katika kuwashambulia na kuwapiga  waandishi wa habari walipokuwa kazini wakitimiza wajibu wao. 


2. Kufungua mashtaka; private prosecution kama sheria inavyoelekeza. 


3. Kukusanya ushahidi wa wazi uliopo na kufungua kesi za madai, kudai fidia. 


Imetolewa Septemba 21, 2014 na;
Kigaila Singo Benson
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.