Wataalamu wa afya wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakisimamia mazishi ya mgonjwa aliyedaiwa kufariki dunia kwa ugonjwa wenye dalili zinazofananishwa na ebola
Mwili wa Salome Richard (17)
aliyefariki dunia katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema mkoani
Mwanza akidaiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa ebola ulizikwa juzi katika
makaburi ya misheni mjini hapa chini ya uangalizi maalumu.
Mgonjwa huyo alifariki dunia Ijumaa saa 2 usiku
baada ya kufika hospitalini hapo akiwa na homa kali. Vile vile madaktari
waliokuwa wanatoa huduma kwa mgonjwa huyo wamewekwa kwenye chumba
maalumu kwa ajili ya uangalizi wakati uongozi wa hospitali hiyo
ukisubiri majibu ya sampuli kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Hata hivyo, uongozi wa hospitali hiyo ulisema
hakuna mgonjwa aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa ebola na kwamba mgonjwa
huyo aliyetoka katika eneo la Nyehunge, alikuwa akisumbuliwa na homa
kali.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Mary Jose
alisema Salome alifikishwa hospitalini hapo Ijumaa saa 4:30 asubuhi
akiwa na homa kali.
Alisema muda mfupi baadaye alianza kutokwa na damu
puani, mdomoni na sehemu ya haja kubwa, ndipo aliwekwa katika chumba
maalumu kwa uangalizi wa madaktari watatu.
“Jana (Juzi) tulichukua sampuli na kuzipeleka Dar
es Salaam Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa uchunguzi zaidi, lakini
hatuwezi kusema kwamba ana ugonjwa wa ebola hadi majibu yatakapokuja,
tuliamua kuchukua tahadhari. Tulimlaza kwenye chumba maalumu ili
kumfanyia uchunguzi wa kina,” alisema Dk Jose.
Wakati jana uongozi wa Wizara ya Afya
haukupatikana kwa simu kuzungumzia ugonjwa huo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza imeahidi kutoa tamko leo kuhusiana na kifo hicho.
Mwezi uliopita mgonjwa mwenye dalili kama hizo
aliwahi kupatikana katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, ambaye baada ya
wiki moja alifariki dunia na majibu ya vipimo vyake yalionyesha kwamba
alifariki kutokana na ugonjwa wa chikungunya.
No comments: