Ads Top

Wakati Rais Jakaya Kikwete akipiga marufuku vyama vya siasa na asasi za kiraia kufanya mapema kampeni za kuhamasisha wananchi kuhusu Katiba Inayopendekezwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umenasa waraka wa mkakati wa kutumia Sh2.5 bilioni za umma kuipigia debe katiba hiyo

 
Pamoja na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa jana wakati akilihutubia Taifa kupitia wazee wa Dodoma, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein jana hiyohiyo, aliwataka Wazanzibari kuipitisha Katiba Inayopendekezwa bila kufanya makosa.

Nyuma ya kauli hizo za marais, Ukawa umesema umeandaliwa mkakati kabambe wa kuvitumia vyombo vya habari kwa fedha za umma kutoka Ikulu kuwashawishi wananchi kupigia kura ya ‘ndiyo’ katiba hiyo.

Kauli ya Rais Kikwete
“Kwa sababu hiyo naomba Watanzania wenzangu tuzingatie mamlaka ya Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri lini kura ya maoni itafanyika na lini kampeni zitafanyika, lini wadau watatoa elimu naomba tuwe na subira. Tukizingatia sheria hii hakuna ugomvi.”

Aliongeza hadi Tume itakapotoa maelekezo ya utekelezaji, wakati wa kampeni na kutoa elimu kwa umma bado na kwamba sheria ipo na imezipanga siku maalumu za kufanya hivyo.

Alisema licha ya sheria kuruhusu kampeni kufanyika ndani ya siku 60 kabla ya kura za maoni kupigwa, kwa mamlaka yake akiwa kiongozi wa nchi, kura na kampeni vitafanyika ndani ya siku 30 tu.

“Kampeni zitaanza tarehe 30 Machi na kumalizika tarehe 29 Aprili ikiwa ni siku moja kabla ya kupiga kura ya maoni. Muda huo ndiyo utakuwa wa kufanya hivyo,” alisema Kikwete. 

Dk Shein aipigia debe
Wakati Kikwete akisema hayo, Dk Shein amesema Katiba Inayopendekezwa ni mwarobaini wa kero nyingi za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Wazanzibari wasifanye makosa kuikataa wakati wa kura ya maoni mwakani.

Akizungumza katika kongamano la kuadhimisha miaka minne ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Dk Shein alisema iwapo Katiba hiyo itapitishwa, itasaidia kuimarisha Muungano kwa kuwa imezingatia makubaliano ya Muungano ya kuwa na Serikali mbili.

Waraka wa wapinzani
Jana, viongozi wa Ukawa walieleza kunasa waraka wa mkakati unaofanywa na Ikulu kutaka kuidhinisha fedha za umma Sh2.5 bilioni kwa ajili malipo kwa vyombo vya habari vitakavyotumika kushawishi wananchi kuipigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa.

Tuhuma hizo ziliibuliwa jana kwa nyakati tofauti na Katibu Mwenza wa Ukawa, Dk Willibrod Slaa katika mkutano uliohusisha viongozi wenzake wa Ukawa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee katika moja ya mikutano yake Kanda ya Ziwa.

Viongozi wengine waliokuwapo kwenye mkutano wa Ukawa ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dk Slaa alisema mpango huo unaratibiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu.

Alisema Rweyemamu amepeleka dokezo hilo kwa Katibu wa Rais akitaka kuidhinishiwa kiasi hicho cha fedha ili kampeni za kushawishi wananchi zianze kupitia vyombo vya habari. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema kazi ya kuelimisha umma itafanywa na kamati mbili zitakazoundwa na tume hiyo.

Alisema kabla ya kupiga kura ya maoni, Tume itaunda kamati mbili, moja itakuwa kwa ajili ya kutoa elimu kwa kundi litakalopiga kura ya ‘ndiyo’ na ya pili kwa ajili ya elimu kwa kundi la ‘hapana’.

“Gharama za kamati hizo mbili zitakazoundwa maalumu kwa ajili ya kutoa elimu kwa makundi hayo zitatolewa na NEC,” alisema Jaji Lubuva.

Waraka
Katika dokezo hilo lenye kichwa cha habari ‘media plan kutangaza Katiba Inayopendekezwa,’ kutakuwa vituo saba vya televisheni ambavyo vitakuwa vikitoa matangazo mara mbili kwa wiki kwa muda wa wiki 22.


“Katika matangazo hayo kuna orodha ya wasomi 20 baadhi kutoka vyuo vikuu watakaokuwa wakishiriki kwenye mahojiano ambao kazi yao ni kueleza umuhimu kwa wananchi kuipigia kura ya ‘ndiyo’ Katiba Inayopendekezwa,” lilisema dokezo hilo huku likiwataja kwa majina baadhi ya wasomi hao.

Katika dokezo hilo, yametajwa majina ya watangazaji tisa wa televisheni ambao wataandaa vipindi kwa ajili ya `kuipigia debe’ Katiba Inayopendekezwa.

Lilisema kutakuwa na vituo vya redio 22 zikiwamo za kanda na mikoa ambazo zitafikisha ujumbe huo ili kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa.

“Umuhimu wa mpango huu ni kuiepusha Serikali na aibu ambayo inaweza kutokea endapo wananchi wataamua kuikataa Katiba Inayopendekezwa katika kura ya maoni,” Slaa alisoma sehemu ya dokezo hilo ambalo gazeti hili limeliona.

Alisema dokezo hilo linapendekeza kuwashirikisha wasanii wa kizazi kipya, makundi maalumu katika jamii, ngoma na vikundi vya utamaduni asili na magazeti yakiwamo ya udaku.

“Kundi la wahariri linaandaliwa kwa ajili kusaidia kuitangaza Katiba Inayopendekezwa kwa njia ya magazeti, bajeti itajulikana baada ya kukamilisha mazungumzo na wahariri hao,” alisema Slaa akirejea dokezo hilo.

Alisema huo ni ufisadi wa fedha za walipakodi kutumika kupitisha Katiba ambayo haina manufaa kwa wananchi, bali kwa wanachama wa CCM.

“Hizi si fedha za Rais Kikwete, ni fedha za walipakodi wa nchi hii. Ikulu kutumia fedha hizi kwa ajili ya kushawishi wananchi ni ufisadi,” alisema.

Akizungumzia hilo, Mbatia alisema wakati Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikikosa Sh8 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa, Sh2.5 bilioni zinatumika kupitisha Katiba yenye manufaa kwa wanaCCM na si wananchi.

Kauli ya Mdee
Awali, akiwahutubia mamia ya wananchi wa Kata ya Mwandoya, Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe alisema: “Ikulu inataka kuanzisha mpango wa kuupotosha umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa.


“Tutabanana na CCM, kulia, kushoto, mbele na nyuma hadi tuhakikishe Katiba yao haipiti, tutazunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi kilichomo katika Rasimu ya Katiba na kile kilichowekwa na CCM katika katiba yao lakini kubwa kwa nini wananchi wapige kura ya ‘hapana’ ndiyo itakuwa hoja yetu.”

Katiba Inayopendekezwa ilikabidhiwa kwa Rais Kikwete na Dk Shein na Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba Samuel Sitta Oktoba 8, mwaka huu katika hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Kauli ya Ikulu
Akizungumzia tuhuma hizo, Rweyemamu alihoji, “Kwani kuna ubaya gani kutoa elimu kwa umma? Kama wao wanapita huko wanawataka wananchi wapige kura ya ‘hapana’ ujue kutakuwa na upande mwingine utapita utasema pigeni kura ya ‘ndiyo’.

Kuhusu fedha za umma kuendesha mpango huo, Rweyemamu alisema:

 “Kila kitu kinakwenda kwa sheria, kwani hata hizo fedha zitatolewa na Serikali kama ambavyo ilitoa za kugharimia Bunge maalumu. Tatizo lenu ninyi mnachukulia mambo kijuu juu lakini hapa hakuna tatizo lolote na hicho alichowaonyesha (Mdee) ni proposal (mapendekezo) tu na wala siyo bajeti kamili.”

Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Raymond Kaminyoge, Mwinyi Sadallah, Suzan Mwillo, Andrew Msechu, Habel Chidawali.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.