Ads Top

POLISI WAWATAWANYA WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YA CHICCO WALIOANDAMANA WAKIDAI HAKI YAO KAGERA.

Jeshi la Polisi mkoani Kagera limelazimika kutumia nguvu katika kuwatawanya baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya CHICCO toka nchini China inayojenga barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita hamsini na tisa toka Kyaka hadi Bugene ambao ni miongoni mwa wafanyakazi zaidi ya mia tano wanaoidai kampuni hiyo zaidi ya shilingi bilioni moja.



Mkuu wa jeshi la polisi wa wilaya ya Karagwe Miki Makanja akitoa onyo kabla ya jeshi hilo kuwatawanya wafanyakazi hao kwa mabomu na maji ya kuwasha waliokuwa wakifanya maandamano kuelekea kwenye ofisi za kampuni hiyo kudai haki yao aliwaambia warudi majumbani mwao au warudi kwenye maeneo ya kazi kwa kuwa madai yao yanashughulikiwa na ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo kauli iliyopigwa vikali. 


Nao baadhi ya wafanyakazi walioongea na ITV wakati wakielezea sababu za kufanya maandamamo wameyataja madai yao ya tangu mwaka 2013 ambayo hayajalipwa na kampuni ya ukandarasi ya CHICCO kuwa ni pamoja na mapunjo ya mishahara, fedha za kuachishwa kazi, fedha za muda wa kazi ya ziada na fedha za likizo, pia wamelalamikia vitendo ambavyo hufanyiwa vya unyayasaji pale wanapodai haki yao ambavyo wamevitaja kuwa ni kuachishwa kazi bila sababu.


Kufuatia vurugu hizo meneja wa kampuni ya CHICCO aliamua kujificha na hakutaka kuongea na ITV iliyokuwa kwenye eneo la tukio, hata hivyo ITV ilifanikiwa kumpata mwakilishi wa kampuni ya TECU inayosimamia mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, mhandisi Mashubila Kamuhabwa, akizungumza amesema ya madai ya wafanyakazi hao kuwa ni halali na yanashughulikiwa, amesema kampuni hiyo iko kwenye mchakato wa kulipa madai ya wafanyakazi hao wakati wowote kuanzia sasa.
chanzo  ITV

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.