WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA, ANATARAJIWA KUFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
waziri mkuu Kasimu Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kufungua mkutano wa wadau wa uwezeshaji wananchi kiuchumi jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Dk. Hamisi Mwinyimvua, alisema mkutano huo ni sehemu ya utaratibu
na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji.
Alisema mkutano huo unaotayarishwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi (NEEC) na Ofisi ya Waziri Mkuu utahusisha wadau mbalimbali
ambao ni wizara, idara na taasisi za serikali, mamlaka za serikali za
mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa Dk. Mwinyimvua, pamoja na mambo mengine, mkutano huo
utajadili taarifa ya utekelezaji wa sera ya taifa ya uwezeshaji wananchi
kiuchumi na kutambua juhudi za wadau wanaotekeleza sera hiyo.
“Mkutano pia utajadili changamoto na kuibua mbinu bora za
utekelezaji wa mkakati wa taifa wa uwezeshaji wananchi kiuchumi,”
alisema na kuongeza kuwa mikutano kama hiyo itakuwa inafanyika kila
mwaka.
Naye Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa, alisema kupitia mkutano
huo, baraza hilo linatarajia kuanzisha rasmi dawati la uwezeshaji na
ushiriki wa wananchi kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, wizara na idara
katika kufuatilia masuala ya uwezeshaji, kuandaa taarifa na kuwasilisha
NEEC.
“Mkutano huu utasaidia kuratibu majukumu ya uwezeshaji kwa kuzingatia uwajibikaji, uadilifu, uaminifu na kujali,” alisema.
Beng’I aliongeza kusema kuwa, mkutano huo pia utachochea hamasa na
kuhakikisha wananchi wanapewa upendeleo wa kipekee kwa watoa huduma
mbalimbali katika zabuni na miradi mikubwa katika maeneo yao pale
wanapokidhi masharti ya zabuni husika.
Baraza hilo limesandaa mkakati wa taifa wa uwezeshaji wananchi
kiuchumi na mwongozo wake unaohusisha sekta zote nchini utazinduliwa
katika mkutano huo.
chanzo nipashe
No comments: